Monday, October 21, 2013

Waziri wa Kikwete afanya uchochezi



•  Apinga kauli yake aliyoitoa Septemba 26

na Mwandishi wetu, Mbeya
WAZIRI wa Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, amewatia hofu wananchi wa Mbeya, akidai kuwa viongozi wa vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi wana mpango wa kuvuruga amani kwa kuwa kuna mataifa makubwa yanataka kuwatumia kuanzisha vurugu nchini ili yaweze kuuza silaha.

Simba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (UWT) alitoa kauli hiyo ya kichochezi juzi jijini Mbeya wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Manga.

Septemba 26, mwaka huu, Waziri Simba aliitisha mkutano na waandishi wa habari wizarani kwake, akiwataka wananchi kupuuza kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kwenye mkutano wao wa Septemba 21, Jangwani jijini Dar es Salaam, akidai ziliashiria uvunjifu wa amani.

Alidai kuwa katika mkutano wao, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF walitoa kauli za uchochezi na zenye kuhatarisha amani ya Watanzania.

“Kauli ya Lipumba kuwa vijana msikubali, wakati wa kufanya mazoezi umefika, na kauli ya Mbowe kuwa Oktoba 10 ni siku maalumu ya kitaifa ya ‘Civil Disobedience’, hizi ni kauli za kichochezi na Watanzania msikubaliane nazo,” alisema.
Kwamba, iwapo machafuko yakitokea waathirika wakubwa ni wanawake, walemavu, wazee na watoto, hivyo kama Waziri wa Maendeleo ya Jamii, anayo haki ya kulizungumzia hilo.

Hata hivyo, juzi Waziri Simba alisahau kauli yake hiyo kuhusu uchochezi, badala yake akawatia hofu wananchi, kwamba viongozi wa vyama hivyo vitatu waligomea muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, kutokana na kuwa na ajenda ya siri.

Akiwa ameongozana na Mbunge wa Viti Maalumu Mbeya, Mary Mwanjelwa (CCM), Simba aligusia mauaji yanayoendelea katika mataifa ya Libya, Misri na Syria akidai wapinzani wanataka kuifikisha nchi hapo.

“Si mnaona Libya, Misri na Syria, mataifa tajiri kabisa yanagombana kila kukicha. Nina wasiwasi huenda hawa wakubwa wanataka kuwatumia viongozi wa upinzani ili kuvuruga amani ya nchi na kulitumbukiza taifa kwenye mauaji,” alisema.
Mbali na kauli hizo za hofu kwa wananchi, Waziri Simba na Mwanjelwa walitumia muda mwingi kumkashifu Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu (CHADEMA) wakidai ana mapepo.

Alisema tukio la mbunge huyo kupigana na askari wa Bunge ndani ya ukumbi wa Bunge, lilitokea kwa kuwa hakukuwa na mtu wa kuombea ‘mapepo’ siku hiyo baada ya kumkumba ghafla.

“Siku ile tukio linatokea bahati mbaya Mchungaji Lwakatare (Mbunge wa Viti Maalumu - CCM, Getrude Rwakatare) hakuwemo ukumbini maana angeweza kuyaombea, na hivyo naomba wananchi wa Mbeya msituletee ‘mapepo’,” alisema.

Naye Mwanjelwa akihutubia mkutano huo, alidai kuwa hali hiyo ya mapepo mara kadhaa imekuwa ikimsababishia Sugu kujiingiza kwenye vitendo vya vurugu, likiwemo tukio la hivi karibuni kupigana bungeni badala ya kuibua hoja za maendeleo.
Alisema anashangaa tabia ya mbunge huyo ambaye alidai anatumia muda mwingi kuhamasisha vurugu na yeye kuwa kinara badala ya kuutumia kushughulikia matatizo ya wananchi wa Mbeya waliomchagua.

“Serikali ya CCM ndiyo mlezi, yenye familia na yenye uchungu, inatengeneza miundombinu. Barabara zote za lami hapa nyie ni mashahidi, mpango wake ulianza tangu 2006 kabla ya sisi kuwa wabunge, halafu leo anaibuka Sugu anasema amejenga barabara,” alisema.

Alisema utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa mtandao wa barabara za ndani kwa urefu wa kilomita 29 uliokamilika hivi karibuni kwa ufadhili wa sh bilioni 83 za Benki ya Dunia ni mkakati wa muda mrefu wa Serikali ya CCM na si nguvu ya Sugu.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments: