na Salim Said Salim, Maswa
DIWANI wa Viti Maalumu, Mary Misanga
(CCM), ametiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu na
kuhukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani.
Misanga (53) alipatikana na hatia ya
wizi na kuhifadhi mali za wizi; mifuko miwili ya saruji na bati, mali ya
Kampuni ya Kahama Oil Mill.
Akisoma hukumu hiyo juzi, hakimu wa
mahakama hiyo, Thomson Mtani alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa
mbele ya mahakama hiyo.
Alisema kuwa kitendo kilichofanywa na
mshitakiwa ambaye pia ni kiongozi si cha kiungwana na hakileti picha nzuri
kwa jamii.
Hakimu Mtani aliongeza kuwa
mshitakiwa alipatikana na mali ya wizi ambayo ni mifuko miwili ya saruji
kati ya 100 iliyoibwa mara baada ya kuvunja stoo ya kiwanda hicho.
Pia mshitakiwa alikiri kupokea na
kuhifadhi nyumbani kwake bati moja na mifuko miwili ya saruji, vyote vikiwa na
thamani ya sh 146,000, mali ya Kiwanda cha Kahama Oil Mill.
Awali, mshitakiwa alifikishwa
mahakamani hapo akikabiliwa na makosa hayo ambayo inadaiwa aliyatenda Juni 18
mwaka huu, saa 10:00 jioni katika Kijiji cha Hinduki wilayani Maswa.
Katika hatua nyingine, mahakama hiyo
imewaachia huru watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa huku
ikiwahukumu wengine wawili kulipa faini ya sh milioni tano kila mmoja au
kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kula
njama na kuisababishia hasara halmashauri hiyo kiasi cha sh 29,197,780.
Walioachiwa huru na hakimu Mtani
baada ya kuonekana hawana hatia, ni Jackson Mashimba ambaye alikuwa
boharia wa halmashauri hiyo, Sophia Alexender ambaye ni mtunza stoo na Omari
Yahya ambaye ni fundi wa Idara ya Maji.
Mahakama hiyo iliwatia hatiani
mhasibu wa halmashauri hiyo, Samson Sogoyo na Azimio Machibya ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilalo General Makandaras ya mjini Bukombe mkoani
Geita iliyopewa kazi ya kusambaza mabomba katika mradi wa maji ya Bukigi,
Jihu na Malamapaka.
Washitakiwa kwa pamoja walifikishwa
mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Aprili 14
mwaka 2011, wakidaiwa kula njama na kuwasilisha nyaraka za uongo kwa lengo la
kumuibia mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa sh 29,197,780.
Washitakiwa wote walikuwa wakitetewa
wa wakili George Hezron huku upande wa mashitaka ukiongozwa na Mwanasheria
Mwandamizi wa Serikali, Hashim Ngole.
Chanzo: Tanzania daima
No comments:
Post a Comment