WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Dk Fenella Mukangara, amerudia kutoa onyo kwa wamiliki wa gazeti la
Mtanzania na Mwananchi.
Katika onyo hilo alilolitoa jana,
amemtaka mmiliki wa Mtanzania kuzingatia ratiba yao ya kutoa gazeti lao kila
siku ya Alhamisi, la Rai na mmiliki wa Mwananchi, kuacha kuchapisha gazeti lao
katika mtandao kama amri ya kufungiwa ilivyoainisha.
“Wamiliki wa gazeti la Mtanzania
baada ya kufungiwa, wameamua kuligeuza gazeti la kila wiki la Rai kuwa la kila
siku bila ya kibali cha Msajili wa Magazeti. Kwa mujibu wa ratiba, gazeti la
Rai linapaswa kutoka kila siku ya Alhamisi,” alieleza Dk Mukangara katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Wakati huo huo, Dk Mukangara amepokea
maombi kutoka kwa wamiliki wa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania wakiomba
kupunguziwa adhabu au kusamehewa adhabu wanazozi tumikia kuanzia 27 Septemba,
2013.
Hata hivyo, Dk Mukangara amesema
wakati anatafakari maombi hayo, amesikitishwa kuona kwamba magazeti haya mawili
yamekiuka masharti ya adhabu walizopewa na kumlazimu kutoa onyo kwa mara
nyingine.
Katika hatua nyingine, Kampuni ya
Magazeti ya Mwananchi, imedai kupata hasara ya Sh milioni 400 kwa wiki mbili
ambazo gazeti lake la Mwananchi lilikuwa limefungiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo,
Tiddo Mhando, alisema hayo jana alipokuwa akizungumzia kurejea kwa uchapishaji
wa gazeti hilo
baada ya kumaliza kifungo hicho kilichotolewa na Serikali Septemba 27 mwaka
huu.
Mhando alisema mbali na kiasi hicho
kilichotokana na mauzo ya matangazo na magazeti, pia hasara ya Sh milioni 75
imetokea kwa watu mbalimbali waliopo nje ya kampuni hiyo.
“Tunatambua kuwa ndani ya majuma
mawili haya jumuiya ya wafanyabiashara, taasisi na watu mbalimbali wameathirika
kwa kukosa habari pamoja na fursa ya kutangaza nasi. Tunaahidi kuendelea pale
tulipoishia kwa uzi ule ule kwa madhumuni ya kuwahabarisha wananchi,” alisema
Mhando.
Alisema wiki mbili walizofungiwa, kwa
kiasi zimeathiri maendeleo ya gazeti hilo pamoja
na wafanyakazi wake na familia zao kutokana na mategemeo yao
kwa gazeti hilo.
Aliiomba Serikali kuangalia kwa
makini madhara ambayo jamii imepata kwa kufungia magazeti kulingana na sababu
mbalimbali na kuongeza kuwa dhamira ya kampuni hiyo ni kuwapatia wananchi kile
wanachostahili kwa namna wanayostahili kupata.
Source:Habarileo
No comments:
Post a Comment