Picha kwa hisani ya millardayo.com.
SIMBA na Yanga zimetoka sare. Ni sare
ambayo haikutegemewa na mashabiki wa Yanga waliokuwa wanaamini timu yao
ingeweza kupata ushindi wa mabao mengi baada ya (MNYAMA).
kuongoza kwa mabao 3-0 hadi timu
zinakwenda mapumziko.
Lakini kitendo cha Simba kurudisha
mabao yote matatu katika kipindi cha pili, siyo tu kimedhihirisha kwamba ngome
za timu zote ni mbovu na kwamba timu zetu hazina utamaduni wa kulinda mabao
yao, bali kimewakumbusha wengi sare ya ajabu ya 'funga-nirudishe' kama ile ya
mwaka 1996 mjini Arusha.
Yawezekana wengine wamesahahu mechi
hiyo, ambayo ilikuwa ya pili kwa timu hizo kukutana mjini Arusha. Ngoja
niwamegee uhondo.
Wapenzi wa soka wa mikoa ya Singida,
Dodoma, Mara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Dar es Salaam na nchi jirani ya
Kenya walianza kuwasili mjini Arusha kuanzia Novemba 7 kushuhudia pambano la
soka la marudiano la Ligi Kuu ya Muungano kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga,
ambalo lilipangwa kufanyika Jumamosi, Novemba 9, 1996 kwenye Uwanja wa Sheikh
Amri Abeid.
Timu hizo zilipambana baada ya miaka
sita tangu zilipopambana kwa mara ya kwanza mjini humo mwaka 1989 katika kuwania
Kombe la Bonanza lililoandaliwa na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha
(AICC) na Yanga kunyakua ubingwa huo kwa ushindi wa goli 1-0 lililofungwa na
Joseph Machella.
Mashabiki hao waliwasili sambamba na
timu hizo zilizoondoka Jijini Dar es Salaam siku hiyo ya Alhamisi, Novemba 7
kwa mabasi kufuatia msaada wa tiketi 30 ambazo kila moja ilipewa na Chama cha
Soka Tanzania (FAT) baada ya chama hicho kukosa shilingi milioni moja za kuipa
kila timu kwa ajili ya maandalizi. Simba iliwasili kwa basi la Super Star
wakati Yanga ilikwenda kwa basi la Tawfiq na kupelekwa na mfadhili wao wa mjini
humo 'kula maraha' katika hoteli ya kitalii ya Sakina.
Pambano hilo, lilichezeshwa na
mwamuzi Bakari Mtangi wa Tanga aliyesaidiana na washika vibendera Aggrey Mnzavas
wa Kilimanjaro na Sudi Abdi wa Arusha. Kiingilio katika pambano hilo, ambalo
mgeni rasmi alikuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa iliyokuwa inashughulikia
mauaji ya Rwanda Leonnart Aspegren, kilikuwa Shs. 5,200 kwa Jukwaa A, Shs.
2,200 mzunguko na Shs. 500 kwa yosso.
Hata hivyo, bao lililofungwa na Dua
Said dakika za majeruhi siku hiyo liliiokoa Simba kuepuka janga la kuendelea
kuwa mteja wa Yanga mwaka huo na kuzifanya timu hizo zitoke sare ya magoli 4-4
katika pambano lililopooza.
No comments:
Post a Comment