Friday, October 11, 2013

ICC:Mawakili wa Kenyatta wataka kesi ifutwe



Mawakili wa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, wameitaka mahakama ya kimataifa ya jinai kusimamisha mashtaka ya Rais huyo kabla ya kesi yake kuanza mwezi ujao.
Wanasheria hao wamesema mashahidi wa utetezi wamekuwa wakitishwa, na kwamba wanao ushahidi wa kutosha kuthibitisha ukiukwaji wa taratibu za mahakama hiyo.

Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto, wanatuhumiwa kuchochea wimbi la vurugu za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Takriban watu1,200 walifariki na wengine laki sita kuachwa bila makao wakati wa ghasia hizo.

Kesi dhidi ya Kenyatta inatarajiwa kuanza tarehe 12 mwezi Novemba.
Naibu Rais pia yuko mbele ya mahakama hiyo na yeye ndiye afisaa mkuu wa kwanza wa serikali kufikishwa mbele ya mahakama ya ICC.

Mawakili wa Kenyatta waliwasilisha nyaraka za kurasa 38 siku ya Alhamisi kwenye mahakama hiyo wakiitaka kesi hiyo kutupiliwa mbali.
Nyaraka hizo zilisema kuwa upande wa utetezi una ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa mahakama imekua ikiendelea kukiuka taratibu zake.

Pia zilisema kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa mashahidi wa upande wa mashitaka na mwengine mmoja walihusishwa na njama ya kutaka kuhujumu sheria.
Mawakili wa uetetzi aidha walituhumu upande wa mashitaka kwa kuwasilisha kesi ambayo ni ya kifisadi na sio ya haki dhidi ya Rais Kenyatta.

Upande wa mashitaka sasa unatarajiwa kujibu madai hayo na mahakama ya ICC huenda ikaamuru jopo la kusikilizwa kwa madai hayo kuyathibitisha.
                                                        Chanzo: Mjengwablog

No comments: