KIUNGO wa Simba, Henry Joseph,
ameondolewa katika kambi ya Simba huku Ramadhan Chombo ‘Redondo’ akirudishwa
kikosi cha pili.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti
imezipata, zinasema Henry ambaye amesajiliwa na Simba msimu huu huku akilipwa
mshahara wa Sh1.5 milioni, alikorofishana na kocha wake, Abdallah Kibadeni,
Jumatatu wiki hii katika mazoezi ya asubuhi yaliyofanyika katika Uwanja
wa Kinesi, Dar es Salaam.
Henry anayemudu kucheza nafasi ya
ulinzi na kiungo, alirudi nchini mwaka huu akitokea klabu ya Kongsvinger ya Norway
iliyoshuka daraja. Kurejea kwake kumetokana na kukataa mkataba mpya wa
klabu hiyo wenye pesa kiduchu baada ya timu kuyumba kiuchumi.
Jumatatu wiki hii, wakati Simba ikiwa
katika mazoezi ya asubuhi kabla ya kuondoka jioni yake kwenda kambini Bamba Beach,
Henry alifanya mazoezi ya kukimbia pekee yake na baadaye wachezaji wote
walipofika uwanjani Kibadeni aliwataka wakimbie kwa pamoja, lakini Henry
inadaiwa aligoma kwa madai kuwa alikuwa tayari ameshafanya mazoezi ya peke
yake.
Hata hivyo, Henry alipozungumza na
Mwanaspoti jana Jumatano, alikanusha vikali madai hayo na kusema kuwa hawezi
kufanya kitendo kama hicho maishani mwake
kwani anaheshimu wajibu wake.
“Sijawahi kufanya utovu wa nidhamu
kwa kocha. Nilifika pale saa 11 alfajiri, nilikuwa wa kwanza. Nikafanya mazoezi
ya kukimbia pekee yangu ili kujiweka fiti kwa sababu muda mwingi nilikuwa
majeruhi. Baadaye wenzangu walipofika nikajumuika nao, lakini Julio (Jamhuri
Kihwelu) akaniambia nipumzike kwani nimechoka,” alisema Henry.
Alisema alivyoambiwa hivyo alimfuata
Kibadeni kumwambia kuwa ameambiwa na Julio apumzike na baada ya hapo akawa
amekaa nje ya uwanja huku wenzake wakiendelea na mazoezi.
“Nilishangaa wakati Kibadeni
anatangaza kikosi cha kuingia kambini Bamba Beach,
alisema sitakwenda na timu, badala yake nikafanye mazoezi ninayoyajua mimi na
kwamba akinihitaji ataniita,” alisema Henry.
Alisema anamheshimu kila mtu na
kwamba katika maisha yake amejitahidi kufuata misingi na nidhamu ya soka na
ndio maana bado haelewi kisa kilichotokea mpaka Kibadeni kuamua kumuacha.
Henry alisema ili kujiweka fiti,
ameendelea kufanya mazoezi asubuhi na jioni na wakati mwingine amekuwa akienda
gym, lakini kwa sasa hayupo katika mazoezi ya Simba.
Mwanaspoti ilimtafuta Kibadeni
kuzungumzia hilo na alilisukuma suala hilo kwa Kocha Msaidizi,
Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ambaye majibu yake hayakuwa ya moja kwa moja, lakini
yalitosha kuthibitisha.
Julio alisema kila mchezaji anatakiwa
kuwa na nidhamu na kujituma katika mazoezi na kwenye mechi na asiyefanya hivyo
hurudishwa kikosi cha pili.
“Mbona hamsemi kuhusu Redondo, wiki
mbili sasa yupo katika kikosi cha pili, mnauliza mambo mengine tu, hapa nidhamu
na kiwango kwanza mengine yanafuata,” alisema Julio.
“Mchezaji ukiwaridhisha makocha kwa
kiwango chako, utabaki katika kambi hii na mechi utacheza, lakini
usipoturidhisha unarudi kikosi cha pili, hiyo ndio falsafa yetu.
“Lakini huyo aliyekwambia Henry
kasimamishwa ni mnafiki na mzandiki, anataka kuleta chuki tu miongoni mwetu
kwani sisi hatusimamishi mtu. Mchezaji mwenyewe anajisimamisha kwa kiwango
chake kibovu na nidhamu mbovu.”
Simba imeanzisha mtindo mpya katika
siku za hivi karibuni kwa kuwaweka kambini Bamba Beach, Kigamboni wachezaji 20
tu ambao wanaonyesha kiwango kikubwa kwenye mazoezi na kwenye mechi.
Chini ya utaratibu huo, mchezaji yeyote
atakayeonyesha kiwango kibovu, hubaki kwenye kikosi cha pili cha timu hiyo
ambacho huwa kinafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi.
Hata hivyo hali ndani ya Simba
imekuwa si shwari katika siku za karibuni kutokana na wachezaji wazoefu
kutuhumiwa kucheza chini ya kiwango jambo linalowakosesha amani makocha wa timu
hiyo.
Chanzo:
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment