BENCHI la Ufundi la Kagera Sugar,
limeweka wazi kuwa limemwandalia ulinzi mkali kiungo wa Yanga, Athuman Iddi
‘Chuji’ wakati timu hizo zitakapocheza Jumamosi mjini Bukoba.
Yanga ambayo inasafiri leo Alhamisi
kuelekea Bukoba ikiwa na kiungo wake Haruna Niyonzima aliyeunguliwa na nyumba
yake hivi karibuni, imecheza mechi mbili nje ya Dar es Salaam dhidi ya Mbeya City
na Prisons. Zote ilitoka sare ya bao 1-1.
Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Mlage
Kabange, aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Tahadhari yetu kubwa ambayo tutaingia
nayo kwenye mchezo huo ni kuhakikisha Chuji (Athuman) hatembei.
“Kuna vijana watatu wameandaliwa kwa
ajili ya kufanya kazi hiyo ya kumwekea ulinzi mkali na kuhakikisha hapati
nafasi ya kupiga zile pasi zake kwa (Mrisho) Ngassa wala (Simon) Msuva.
“Tunaamini kwa kufanya hivyo Yanga
hawatatembea kabisa. Chuji amekuwa akitumika sana kuwachezesha Ngassa na Msuva, hata
ukiangalia mechi walizoshinda mipira mingi imekuwa ikianzia kwake.”
Alifafanua kuwa wameifuatilia Yanga
na kugundua inatengeza mashambulizi yake kupitia winga za kulia na kushoto
ikiwatumia Ngassa na Msuva.
“Hata ukifuatilia matokeo yao katika ushindi wa mechi mbili zilizopita dhidi ya Ruvu
na Mtibwa utabaini hilo.
Chuji amekuwa akiwachezesha vizuri Ngassa na Msuva, lengo letu kumwekea Chuji
ulinzi wachezaji watatu ni kwamba Ngassa pamoja na Msuva wasipate mipira,
nafikiri tukifanikiwa kwa hilo
tutakuwa tumewamaliza kabisa.”
Hata hivyo, Kabange amegoma kuweka
hadharani majina ya wachezaji walioandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Hatuwezi kuwataja majina, nafikiri
hii ni kama vita, huwezi kumpa mpinzani wako
mbinu zako,” alisema.
Yanga itakuwa ikicheza kwenye Uwanja
wa Kaitaba huku ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza
msimu uliopita ingawa ilisawazisha makosa hayo na kulipa kisasi kwenye mchezo
wa marudiano jijini Dar es Salaam.
Bao la Kagera likifungwa na Themi
Felix wakati Nizar Khalfan akifunga la Yanga.
Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz
No comments:
Post a Comment