Thursday, October 10, 2013

CHICHARITO ATAJA SABABU KWA NINI ATAONDOKA MAN U



MSHAMBULIAJI Javier Hernandez amesema anaweza kuondoka ManchesterUnited ili kusaka timu ambayo atapata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza. 


Mshambuliaji huyo anayefahamika kama Chicharito hapewi nafasi kubwa katika klabu ingawa mwezi uliopita aliifungia timu hiyo bao la ushindi katika Kombe la Ligi, maarufu kama Capital One dhidi ya Liverpool na zaidi ya mechi hiyo alianza katika mechi nyingine moja tu, United ikifungwa nyumbani na West Brom.

Hernandez amesema kwamba wakati akiwa ana furaha kuchezea klabu kubwa kama hiyo, pia anataka nafasi zaidi za kucheza na anaamini anaweza kuwa nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza iwe Old Trafford au katika klabu yoyote.

"Nasotea hiyo [kuanza katika mechi zaidi],"alisema Hernandez akihojiwa na kituo cha Televisheni cha Mexico, Deportes Telemundo.
"Nafanyia kazi hilo- kupata nafasi kikosi cha kwanza. Nafahamu kwamba kiwango changu uwanjani kitaniruhusu kutimiza lengo hilo siku fulani, aidha hapa [Manchester] au popote katika klabu yoyote.

"Naelekea kutimiza miaka minne hapa [Manchester United] na kweli, kama ambavyo wakati wote nimesema, nina furaha kuwa tayari nimechezea moja ya klabu bora duniani, nafanya vizuri kila siku kutafuta muda zaidi uwanjani,".

"Nahitaji kupewa nafasi zaidi kuonyesha uwezo wangu, kwa sababu kati yetu sote tunataka kutoa mchango wetu ili hii timu ishinde ubingwa,".
Hernandez amekuwa akisotea namba kikosi cha kwanza United kutokana na kuzidiwa kete na akina Wayne Rooney, Robin van Persie na Danny Welbeck, lakini Mmexico huyo amesema hiyo inaweza kuwa nzuri kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu England.

"Ushindani ndani ya timu wakati wote umekuwa mkubwa na ninafikiri hiyo inaisaidia timu kwa kiasi kikubwa, kwa sababu kuna wachezaji wengi bora ambao kila mmoja kati yao anataka nafasi kikosi cha kwanza,".

"Mazoezi na mechi zinazokuja zitatulazimisha kusimama imara kuisaidia timu kuimarika kwa vyote, kwa uchezaji binafsi na kitimu kwa ujumla,".
Chanzo: sportmail

No comments: