Picha Hii Imechukuliwa Maktaba Yetu
• Wabunge wavimbia
marekebisho ya Katiba
na Mwandishi wetu
HOFU kubwa imetanda ndani na nje ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), juu ya upatikanaji wa katiba mpya, hasa baada ya
Rais Jakaya Kikwete kusaini muswada ambao sasa ni Sheria ya Marekebisho ya
Mabadiliko ya Katiba.
Mkutano kati ya Rais Kikwete na
viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni uliofanyika Ikulu Oktoba
15, 2013 umeongeza mpasuko ulioanza kujitokeza baina ya makada wa CCM na
wapinzani.
Katika mkutano huo, rais na viongozi
wa upinzani waliafikiana vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na
mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini ili ifatutwe namna ya
kuyashirikisha katika marekebisho ya sheria hiyo.
Walikubaliana kwamba vyama vya siasa
nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa katiba mpya, viangalie namna ya
kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja
vitakavyosukuma mbele mchakato huo kwa masilahi mapana ya nchi yao na
mustakabali wa taifa.
Awali kabla ya mkutano huo, makada wa
CCM wakiwamo mawaziri kadhaa waliweka wazi kuwa milango ya Ikulu imeshafungwa
kwa wapinzani kuzungumzia suala hilo, lakini Rais Kikwete alipotangaza kukutana
nao iliwaweka njia panda.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa
kuwa baadhi ya makada wa CCM wamekuwa wakimshutumu Rais Kikwete kwa
kuwabembeleza wapinzani huku akikiumiza chama chake.
Hoja wanayoijenga ni kuwa Rais
Kikwete anataka kujijengea kitu cha kukumbukwa, hasa katika suala la katiba
mpya bila kujali athari zinazokipata chama chake.
Makada hao wanaweka bayana kuwa hali
hiyo itakiacha chama katika wakati mgumu wa kukabiliana na wapinzani
wanaoonekana kuimarika kadiri siku zinavyoyoyoma.
Baadhi ya wabunge wa CCM wanamuona
Kikwete kama msaliti kwa wabunge wake waliopitisha muswada huo, ambao sasa ni
Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba, ukiwa na upungufu ulioainishwa
na wapinzani.
Mmoja wa watu waliohudhuria
mazungumzo ya Ikulu anasema rais aliridhia marekebisho hayo na alibainisha kuwa
yajikite katika masuala kadhaa, likiwamo suala la Tume ya Warioba kuwapo kwenye
Bunge Maalumu la Katiba, marekebisho katika suala la uteuzi wa wajumbe 166 ili
idadi iongezeke na hoja ya Zanzibar kushirikishwa kabla ya muswada wa sheria ya
kura za maoni kuanza.
Tayari Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, alishatoa tamko kuwashangaa
wabunge wa CCM kwa kupotosha kifungu kilichokuwa kinasema Tume ya Mabadiliko ya
Katiba itavunjwa na rais mara tu baada ya kuwasilisha rasimu kwenye Bunge
Maalumu la Katiba, msimamo ambao unaungwa mkono na Mbunge wa Nzega, Hamis
Kigwangala (CCM).
Mbunge huyo katika andiko lake
alilolisambaza katika vyombo vya habari, anakiri kuwa moja ya upungufu
alioubaini katika muswada ule ambao sasa ni sheria, ni kuiua Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kabla ya mchakato kufikia mwisho.
“Kiukweli, lina mantiki ndani yake.
Tukiwa kwenye Bunge la Katiba hakutakuwa na serikali, sasa ni nani atakayejibu
na kuweka sawa hoja za wabunge? Hili kwa kweli wabunge tuliopitisha muswada ule
hatukuliona vizuri,” alisema Kigwangala.
Wakati Kigwangala akiona upungufu
huo, Naibu Spika Job Ndugai, aliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa haoni
udharura wa suala hilo kurejeshwa bungeni.
Ndugai amebeza suala la urejeshwaji
wa sheria hiyo bungeni, akihoji kuwa suala hilo halina udharura.
“Ni ishu gani hasa ambayo wapinzani
walienda kumwona rais ambayo inahitaji udharura huo? Je, kanuni za Bunge
zinaruhusu suala hilo?” alihoji Ndugai.
Akizungumza na gazeti hili wiki hii,
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye, alisema Bunge ni muhimili tofauti. Wabunge kama wataona kuna kitu cha
kubadilisha watabadilisha, lakini wakiona hakuna cha kubadilisha itabaki
ilivyo.
Kauli hiyo imeungwa mkono jana na
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, ambaye alinukuliwa na gazeti moja
nchini (si Tanzania Daima), akisema: “Serikali haikusudii kufanya marekebisho
yoyote kwenye Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba iliyosainiwa na
Rais Kikwete hivi karibuni.”
Mmoja wa wabunge wa CCM aliyehojiwa
na gazeti hili na kutoa msimamo wake baada ya rais kusaini muswada kuwa sheria
ni aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Hamad Yusuf Massauni, ambaye sasa ni Mbunge
wa Kikwajuni.
“Mimi ningekuwa rais nisingepoteza muda
kuongea na wapinzani, na hata kama sheria hii itarejeshwa bungeni, sioni sehemu
yoyote ya kufanyia marekebisho, iwe ya kuondoa koma wala kuweka nukta,”
alisema.
Kabla ya muswada huo kusainiwa kuwa
sheria, Nape alinukuliwa na gazeti hili akisema: “Hofu yangu ni kuwa rais
asiposaini muswada huo, ataingia katika mgogoro kikatiba, itabidi arejeshe
muswada bungeni aeleze kwanini hajasaini, na ukirejeshwa bungeni wabunge wa CCM
wakakataa kufanya mabadiliko, rais angelazimika kuvunja Bunge.”
Aliongeza kuwa: “Mimi ninaona
afadhali rais asaini muswada huu ili kama kuna upungufu uwekwe mezani kama
ilivyokuwa mwanzo, ila nakubali kabisa mzee Warioba ana hoja katika suala la
kutovunjwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya kutetea rasimu mbele ya Bunge
Maalumu la Katiba.”
Alisema wabunge wa CCM ni asilimia 74
ya wabunge wote, hivyo wakishikilia hoja ya kutobadilisha jambo lolote katika
muswada huo baada ya kurejeshewa na rais, matokeo yake ni kuvunjwa kwa Bunge na
nchi kuingia kwenye uchaguzi kabla ya 2015.
Nape alisema CCM haiko tayari kuingia
kwenye uchaguzi kabla ya 2015, hivyo akawataka wanaopinga na kuunga mkono hoja
hizo watumie busara na hekima kufikia maridhiano yatakayolijenga taifa.
Alisema kuwa muswada wa mabadiliko ya
sheria wa mwanzo nao ulipitishwa ukiwa na kasoro mwaka 2011, lakini Chama cha
Demokrasia na Maendeleo walienda kwa rais wakajadiliana wakakubaliwa, na kwamba
viongozi wa CCM walilazimika kwenda Dodoma kuwaeleza wabunge msimamo wa Rais
Kikwete na kuwashawishi waukubali.
“Tulipoona kuna hoja tulilazimika
kwenda Dodoma kuwaomba wabunge wetu wakubali hoja za CHADEMA ili marekebisho
yafanyike, ingawa suala hilo lilifanyika kwa taabu sana, sasa zamu hii wabunge
wa CCM wanaweza wasikubali hoja za wapinzani, na likiendelea vile rais
atalazimika kuvunja Bunge, hili suala limetuweka pabaya sana CCM, sijui hatima
yetu,” alisema.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa
kuwa iwapo serikali itaridhia marekebisho yaliyotajwa na wapinzani, mvutano
mkubwa utazuka bungeni kati ya washindi na washindwa.
Jambo hilo linadaiwa halitakubaliwa
na wabunge wa CCM ambao mara kwa mara wamekuwa wakishutumiwa kupitisha mambo
kwa kuangalia zaidi masilahi ya chama kuliko taifa.
Kumekuwa na mipango ya CCM kumuandaa
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, kuwa Spika wa Bunge la Katiba.
Inadaiwa Chenge ndiye atakayebeba
jukumu la kudhibiti baadhi ya hoja zinazopingwa na CCM zilizotolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba.
Miongoni mwa mambo yaliyomo ndani ya
rasimu ya katiba ni serikali tatu.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment