Amwachia msalaba
Filikunjombe
na Mwandishi wetu
WAKATI Oktoba 25 mwaka huu, Kamati ya
Hesabu za Serikali (PAC), ikitarajia kuwaweka kikaangoni viongozi wa vyama vya
siasa vya CCM, CHADEMA na CUF, walioshindwa kuwasilisha hesabu za ukaguzi wa
fedha za ruzuku kwa miaka minne, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe
hatakuwepo.
Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Zitto
alimuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, kutovipa ruzuku ya serikali vyama vya
siasa vinavyostahili hadi pale ukaguzi wa mahesabu utakapofanywa.
Zitto alifikia hatua hiyo baada ya
Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), kuieleza kamati hiyo kuwa hajapokea ripoti
yoyote ya mahesabu kutoka kwa vyama hivyo tangu mwaka 2009.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo,
shilingi bil. 67.7 hazijakaguliwa kwa vyama vyote vya siasa kwa miaka minne
sasa tangu mwaka 2009.
Kutokana na kadhia hiyo, Zitto pia
alimuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa kuwaandikia barua ya kisheria makatibu
wakuu wa vyama vinane vinavyopata ruzuku ya serikali kufika kwenye kamati yake
Oktoba 25, mwaka huu kujieleza kwanini hawakuwasilisha ripoti zao.
Miongoni mwa makatibu wakuu hao ni
Abdulrahman Kinana (CCM), Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA), Maalim Seif Sharif
Hamad (CUF) na Sam Ruhuza (NCCR-Mageuzi).
Vyama vingine vinavyopokea ruzuku
nchini ni TLP, DP, UDP na APPT- Maendeleo.
Zitto aenda Uswisi
Zitto amealikwa Uswisi na Shirika la
Kimataifa la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo (Eurodad) kufanya ziara ya
kiuchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi hizo kuanzia leo
hadi Novemba 5.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Zitto, uchunguzi huo utaendeshwa na wataalamu waliobobea wa masuala ya kodi na
maendeleo.
Eurodad ni mtandao wa mashirika
yasiyo ya kiserikali yapatayo 48 kutoka nchi 19 za Ulaya ambayo yanajihusisha
na masuala ya kufutia madeni nchi zilizoendelea, misaada yenye maana na kodi za
haki.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa
mashirika hayo yamekuwa kwenye kampeni ya kupinga utoroshwaji wa fedha kupitia
ukwepaji kodi unaofanywa na mashirika ya kimataifa kwa nchi zinazoendelea.
Zitto amekuwa mmoja wa wabunge
wanaosimamia hoja ya kutaka Watanzania waliotorosha fedha kwenda nje (Uswisi)
warejeshe na kufunguliwa mashitaka.
Mwaka 2012 aliwasilisha hoja binafsi
bungeni na kupitishwa kuwa Azimio la Bunge ya kutaka uchunguzi kuhusu
utoroshwaji wa fedha na kufichwa nje.
Kikosi kazi cha serikali kwa ajili ya
kutekeleza azimio hilo la Bunge kinatarajia kuwasilisha taarifa yake katika
Mkutano wa 16 wa Bunge.
Zitto alibainisha kuwa kesho
atakutana na Waziri wa Fedha wa Uswisi na maofisa wa mabenki na asasi zisizo za
kiserikali zilizopo jijini Geneva.
Alibainisha kuwa atahudhuria mkutano
wa Kamati ya Kodi ya Umoja wa Mataifa katika kampeni ya kubadili mfumo wa kodi
za kimataifa ili kuzuia unyonyaji wa nchi za Kiafrika unaofanywa na kampuni
kubwa za kimataifa.
Zitto pia atatembelea Luxembourg na
Brussels kabla ya kwenda Norway ambako atamalizia ziara yake kwa jopo la
wataalamu wa masuala ya kodi na maendeleo kuandika taarifa maalumu yenye
mapendekezo kuhusu kuzuia utoroshaji wa fedha kutoka Afrika.
Pia kiongozi huyo atakwenda London
kutoa mada kuhusu masuala ya kodi za kimataifa katika mkutano wa uwazi (Open
Government Partnership).
Mwenyekiti huyo wa PAC Tanzania
atafanya mazungumzo na Mwenyekiti wa PAC Uingereza kuhusu masuala mbalimbali ya
ushirikiano wa mabunge mawili.
Aacha gumzo
Wakati Zitto akiwa safarini, gumzo
kubwa limetawala maeneo mbalimbali juu ya hatua yake ya kuvisulubu vyama vya
siasa kikiwemo CHADEMA ambacho yeye ni mmoja wa viongozi wake, akiwa Naibu
Katibu Mkuu bara.
Mijadala hiyo inatokana na hatua ya
CHADEMA kukana na kuweka wazi nyaraka za ukaguzi wa fedha kwa mwaka 2010/2011
walizoziwasilisha ofisini kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Kutokana na Zitto kuwa safarini,
viongozi hao wa vyama vya siasa sasa watakutana na Makamu Mwenyekiti wa PAC,
Deo Filikunjombe.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment