Rais Obama amesema yuko tayari kuzungumza na wajumbe wa chama cha Republican kuhusu kitu chochote, lakini baraza la wawakilishi linatakiwa kwanza lipitishe mswaada kuzifungua tena shughuli za serikali.
Rais wa Marekani, Barack Obama,
ameonya kwamba viongozi wa dunia wana wasiwasi wabunge wa chama cha Republican
nchini humo huenda wakauvuruga kabisa uchumi wa taifa na kuapa kutotetereka
katika msimamo wake wa kutaka kiwango cha fedha Marekani inazoweza kukopa
kulipa madeni yake kiongezwe bila masharti yoyote.
Akizungumza kwenye mkutano na
waandishi wa habari katika ikulu yake mjini Washington hapo jana, rais Obama amewataka
wabunge wa chama cha Republican waache vitisho na waupigie kura muswaada wa
sheria kuidhinisha fedha kwa ajili ya serikali, ambao ikiwezekana huenda
ukapitishwa leo.
"Baraza la wawakilishi
linatakiwa kupiga kura leo. Kama wanasiasa wa
chama cha Republican na spika Boehner wanasema hakuna kura za kutosha. Basi
wanatakiwa wathibitishe. Acha muswada upigiwe kura halafu tuone kitakachotokea.
Wasiwasi wangu mkubwa ni kwamba kuna kura za kutosha."
Boehner akataa kujisalimisha bila
masharti
Spika wa bunge la Marekani, John
Boehner, amesisitiza hakutakuwa na 'kujisalimisha bila masharti' kwa chama cha
Republican. Boehner amesema bunge litairuhusu Marekani ikope fedha zaidi kama rais Obama atakubali kubana matumizi. Hata hivyo
kulikuwa na ishara ya matumaini ya kuutanzua mgogoro mkali wa bajeti ambao
umesababisha baadhi ya shughuli za serikali kufungwa kwa zaidi ya wiki moja na
hivyo kuibua hofu kwamba Marekani huenda ikashindwa kulipa madeni yake kama kiwango hicho hakitaongezwa kufikia tarehe 17 mwezi
huu.
Obama amesema kukiwa na haja
atakubali makubaliano ya muda mfupi kuongeza kiwango cha fedha serikali
inazoweka kukopa na kufungua tena shughuli zilizofungwa, hatua ambayo
itauahirisha mkwamo huo kwa wiki kadhaa. Wakati huo huo, rais Obama
amewashutumu wabunge wa chama cha Republican kwa kuutumia mkwamo wa bajeti kama chombo cha shinikizo kwa lengo la kuyahujumu mageuzi
ya bima ya afya.
Wachambuzi wanasema hiyo ni mbinu
mpya ya chama cha Republican kumbana Obama. Mwanauchumi Steven Ricciuto
anasema, "Nadhani huo utakuwa mkakati wa chama cha Republican ambao kwa
kiwango fulani unaweza kukubalika na Wamarekani; kwamba hupaswi kushindwa
kulipa madeni. Lakini katika miswaada yote ya bajeti huenda kuna masharti
yaliyofungamanishwa, ambayo huenda yakauendeleaza mkwamo uliopo."
Lakini rais Obama ameshikilia msimamo
wake kwamba katu hatokubali makubaliano yoyote kuhusu kukakataa kuzikubali
nadharia za chama cha Republican ili apate mamlaka zaidi kukopa fedha
kugharamia kifedha majukumu ya Marekani.
Obama amesema bunge lina kazi mbili za
msingi - kupitisha bajeti na kuhakikisha Marekani inalipa madeni yake. Ameonya
kwamba wabunge hawakudai walipwe fidia na kusisitiza msimamo wake kuwa atafanya
mazungumzo na Warepublican mara tu kiwango cha fedha kitakapoongezwa na
shughuli za serikali zilizofungwa zitakapofunguliwa.
Spika Boehner alijitokeza kwenye
televisheni muda mfupi baada ya Obama kumaliza mkutano wake na waandishi wa
habari na kusema mazungumzo yatafanyika. Spika huyo pia ameukosoa msimamo wa
Obama akisema sivyo serikali ya Marekani inavyofanya kazi. Obama ambaye
alizungumza na Boehner hapo kabla kwa njia ya simu, anahoji kuongeza kima cha
fedha serikali inazoweza kukopa ni muhimu kwa uaminifu wa taifa hilo kuweza
kukopa fedha na hakupaswi kuvurugwa na wasiwasi wa kisiasa.
Mwanamke wa kwanza kuingoza benki kuu
ya Marekani
Wakati mzozo wa bajeti ukiendelea,
rais Obama leo atamteua Janet Yellen kama mwanamke wa kwanza kuiongoza benki
kuu ya Marekani. Obama atampendekeza Yellen kwa awamu ya miaka minne kuchukua
mikoba kutoka kwa Ben Bernanke, ambaye sera zake za miaka minane zilihusishwa
na kukabiliana na mzozo wa kiuchumi ulioikabili dunia na kutafuta njia za
kuufufua uchumi.
Afisa wa Marekani amesema tangazo hilo litafanywa katika
ikulu ya Marekani leo usiku katika tukio litakalohudhuriwa na Bernanke, na
hivyo kufungua mlango kwa mchakato wa kuthibitishwa katika nafasi hiyo. Yellen,
mwenye umri wa miaka 67, amekuwa akishikilia nafasi ya pili ya uongozi wa benki
hiyo.
Yellen alizaliwa New York na ameolewa na mshindi wa tuzo ya
uchumi ya Nobel, profesa George Akerlof na ni mama wa profesa wa uchumi, Robert
Akerlof. Alisomea uchumi katika chuo kikuu cha Brown na baadaye katika chuo
kikuu cha Yale, ambako alipata shahada yake ya uzamili. Yellen amekuwa profesa
katika chuo kikuu cha Havard na hivi karibuni katika chuo kikuu cha California, Berkeley,
ambako mume wake pia hufundisha na kufanya utafiti.
Mwandishi: Josephat Charo
No comments:
Post a Comment