• Ahudhuria kikao cha
madiwani kwa mara ya kwanza
na Grace Macha, Arusha
KWA mara ya kwanza tangu kuzuka kwa
mgogoro wa umeya jijini Arusha, mbunge wa jimbo hilo, Godbless Lema (CHADEMA),
jana alishiriki kikao cha Baraza la Madiwani ambacho kiliongozwa na mwenyekiti
wa muda, Diwani wa Kata ya Daraja Mbili, Prosper Msofe (CHADEMA).
Mgogoro wa umeya jijini Arusha,
ulichukua sura mpya baada ya madiwani wa CCM kuwazunguka wenzao wa CHADEMA
mwaka 2010 na kumchagua Gaudence Lyimo kuwa meya, jambo lililozua tafrani
kubwa.
Baadaye mgogoro huo ulikua, huku CHADEMA
wakiendelea kutomtambua meya huyo, jambo ambalo lilisababisha madiwani wao
watano kuvuliwa uanachama baada ya kufikia muafaka hewa na CCM.
Katika uchaguzi mdogo wa kata hizo
nne Julai mwaka huu, CHADEMA iliibuka kidedea na hivyo kuzua hofu kuwa huenda
ikatumia wingi wake kumng’oa meya, hatua ambayo Lema alisema si ajenda yao kwa
sasa bali kuwatumikia wananchi.
Jana wakati baraza hilo lilipokutana,
Diwani wa Kata ya Sokon 1, Michael Kivuyo (TLP), alikieleza kikao kuwa Meya
Lyimo amesafiri, hivyo amemkaimisha ofisi kutokana na halmashauri hiyo kutokuwa
na naibu meya.
Taarifa hiyo iliibua mjadala huku
madiwani wakitaka kanuni zifuatwe, ndipo Diwani wa Kata ya Levelos, Ephata
Nanyaro (CHADEMA), alimpendekeza Msofe awe mwenyekiti wa muda wa kikao hicho.
Katika kura zilizopigwa, Msofe
alipata 13 za kumkubali huku nne zikimkataa.
Kikao hicho kiliibua hoja ya upotevu
wa zaidi ya sh milioni 14.8 ambapo kati yake fedha taslimu ni zaidi ya sh
milioni 8.6 zilizodaiwa kwisha kutokana na makato ya benki ya kuhudumia
akaunti.
Matumizi mengine ni vifaa kwa ajili
ya ujenzi wa tarafa ikiwemo saruji na mchanga vyenye thamani ya zaidi ya sh
milioni 6.3 ambavyo vilichangwa na wananchi.
Madiwani hao walimuagiza kaimu
mkurugenzi wa jiji, Afwilile Lamsy, kuhakikisha kwenye kikao kijacho analeta
taarifa za kibenki za akaunti iliyowekwa fedha hizo mwaka 2004 ili kuona namna
zilivyokatwa hadi zikaisha. .
“Tunataka kuonyeshwa taarifa za benki
tujue namna fedha hizo zilivyotumika, hatutaki kuona barua za mawasiliano ya
mkurugrnzi na mkuu wa wilaya, tunataka wale wote waliohusika waletwe hapa hata
kama walihamishwa watafutwe waletwe.
“Hii ni fedheha kubwa, haiwezekani
wananchi wachange fedha halafu zipotee hivi hivi tu, tunataka tuletewe hapa
taarifa za benki na tupelekwe tukaone mchanga na saruji vilivyonunuliwa,”
alisema Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Doita Isaya (CHADEMA). .
Pia madiwani hao waliwaagiza
wataalamu kupima maeneo muhimu ikiwemo mito, hifadhi za barabara na maeneo ya
milima na kuyawekea alama ili kuyalinda yasivamiwe kama hali inavyoonekana
kwenye maeneo mengi ya jiji la Arusha.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment