BAADHI ya wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba wamewaonya wenzao ambao wamepanga kumzomea Rais Jakaya Kikwete wakati
akitarajiwa kulihutubia bunge hilo kesho.
Onyo hilo walilitoa jana mjini Dodoma
wakati wa semina maalum ya kupitia kanuni za bunge hilo, iliyofanyikia katika
ukumbi wa Bunge.
Akichangia katika semina hiyo mmoja
wa wajumbe hao, James Mbatia, alionya taarifa za kuwepo kwa mkakati wa kupanga
kumzomea Rais Kikwete, atakapolihutubia Bunge kesho.
Mbatia alisema, Rais anaongoza watu
wote, ingawa ana chama cha siasa kwa mujibu wa sheria hivyo ni lazima
asikilizwe.
“Tumesikia wapo wenye mkakati wa
kumzomea Rais atakapokuja hapa,” alisema Mbatia.
Aliwataka wajumbe wenzake waache
fitina, kuzomeazomea na badala yake wavumiliane ili waweze kuvuka salama huku
akisisitiza kuwa, kauli ya umma ni kauli ya Mungu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bunge
hilo, Samuel Sitta, alionya vinara wa fujo na kusisitiza kuwa hawataachwa
salama kwani kuna kamera maalumu ambazo zitatumika kukusanya ushahidi.
“Kamati ya Kanuni Madhubuti
zitafanyakazi na hatutakubali kuahirisha Bunge huku watu wakilipwa posho,”
alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema, ndani ya Bunge hilo kuna
kamera 12 ambazo zinanasa kila tukio, hivyo ushahidi huo utakusanywa na
kuupeleka kamati ya maadili kwa ajili ya uamuzi.
Mbali na hayo Mwenyekiti huyo
hakusita kutamka wazi kuwa ndani ya Bunge hilo kuna vinara wa vurugu ambao
watahakikisha wanashughulikiwa pindi watakapojitokeza wakati Rais Kikwete
akihutubia.
Naye Julius Mtatiro ambaye ni
miongoni mwa wajumbe wa bunge hilo alisema, hatarajii kama kuna mtu yeyote
anayetaka kufanya jambo lolote.
Alisema, Rais ana dhamira nzuri na
mchakato wa kuwapatia Watanzania Katiba Mpya, hivyo hatarajii jambo jingine
lolote zaidi ya kumsikiliza Rais Kikwete.
Wakati huo huo, Mtatiro alitolea
mfano alivyotukanwa matusi mabaya na mmoja wa wajumbe pale alipokuwa akisimama
na kupiga meza.
Alisisitiza kwamba, kila mmoja aelewe
kuwa wapo bungeni hapo kwa ajili ya kutunga Katiba ambayo ni tendo la
maridhiano na maelewano na wajumbe waweke hilo mbele.
Akijibu hilo, Mwenyekiti wa bunge
hilo, Sitta alisema kusimama na kupiga meza huo nao ni udikteta, kwani mjumbe
haruhusiwi kusimama bila kuruhusiwa.
Sitta, alisema hatavumilia udikteta
wa aina yoyote uwe wa wengi au wachache.
Wakati huo huo, Kada wa siku nyingi
wa CCM na Mjumbe wa Bunge la Katiba, Kingunge Ngombale Mwiru, amesema Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, imeshindwa kuweka
misingi ya kujenga muungano badala yake inataka kuuvunja.
Kingunge ametoa kauli hiyo ikiwa ni
siku moja baada ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba katika
Bunge la Katiba Mjini Dodoma, huku akiendelea kutetea msimamo wa Tume yake wa
kupendekeza muundo wa Serikali tatu.
Akihojiwa jana katika kipindi cha Jambo
Tanzania kinachorushwa na Kituo cha Utangazaji cha Televisheni ya Taifa (TBC1)
Kingunge, alisema mahali popote alipo binadamu lazima kuwepo kero na
changamoto.
Hata hivyo alisema changamoto hizo
haziwezi kuvunja muungano. Alitoa mfano akisema kwa nchi za Afrika, Tanzania ni
nchi ya kuigwa kutokana na kuwa kisiwa cha amani.
Kingunge alisema ameshangazwa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba kutoa mapendekezo bila kuangalia matokeo ya muundo
ambao utasambaratisha uzalendo.
"Tume wao wamemaliza kazi yao
wameandika maandishi mengi, lakini Bunge Maalum la Katiba ndilo linalochagua
Katiba ambayo itapendekezwa na wananchi," alisisitiza Kingunge.
Aliwataka wajumbe wa Bunge hilo
kutuliza vichwa vyao, kwani rasimu hiyo haiandikwi na wajumbe wala chama
chochote na kwamba hakuna mtu anayeweza kwenda Ikulu bila kuchaguliwa na
wananchi.
Kada huyo wa CCM aliwataka Watanzania
kuwa makini na watulivu na kuliachia Bunge tukufu kazi ya kutunga katiba kwani
ndilo linawakilisha wananchi na Serikali.
Alishauri Watanzania watulie na
kuangalia Katiba ambayo imeachwa na waasisi kwa miaka 50 imeleta mafanikio
gani. Alisema Tanzania ni Taifa kubwa na lengo la kupigania uhuru ni kuungana
kumuondoa mkoloni.
"Ka t i b a mp y a kwa n z a
tukubaliane si mradi kupata katiba, tuwe na lengo la kupata katiba iliyo bora
na kabla ya kupata hiyo mpya tuangalie katika miaka ya 50 tumeweza kupata
mafanikio makubwa kiasi gani kwa Katiba ya zamani chini ya mwasisi Mwalimu
Julius Nyerere," alisema.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bunge la
Katiba kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Pandu Amir Kificho, alisema kama
mwakilishi wa Serikali ya Zanzibar wanapendekeza Serikali mbili.
Kificho alisema jambo la Muungano
limedumu ndani ya miaka 50 na lengo kuweka muungano uliyo bora zaidi, lakini
changamoto zilizokuwepo ingetumika utaratibu wa kuziondoa kwa ajili ya
kuimarisha ushirikiano.
"Mimi kama mwakilishi kutoka
Zanzibar tunachagua Serikali mbili na katika Bunge hili kuna Wawakilishi kutoka
Zanzibar wa CCM na CUF wanataka Serikali mbili ziweze kuendelea kama msimamo
wao wa Baraza la Wawakilishi wa CCM," alisema.
Alisema kuundwa Serikali tatu ni
mzigo na zitaleta machafuko hatimaye kuyumba. Alisema katika nchi tatu moja
ikiyumba, lazima idondoshwe.
"Naitupia lawama Tume ya Rasimu
ya Katiba kwa kupendekeza na kuchagua Serikali tatu halafu katika rasimu yao
hawajaelezea faida ya kuchagua Serikali tatu au Serikali mbili, jicho lao
alijaangalia mbele,"alisema
Wakati huo huo, Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu nchini imeunga mkono muundo wa Serikali tatu zilizopendekezwa na Tume
ya Jaji Warioba katika Katiba mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari
Jijini Dar es Salaam jana, Msemaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Rajabu Katumba,
alisema ni vyema zikawepo Serikali tatu ya Tanganyika, Zanzibar na Serikali ya
Muungano.
Alisema kuwepo kwa Serikali hizo
kutatatua kero nyingi zinazojitokeza katika kipindi hiki cha uwepo wa Serikali
mbili. Alisema Serikali ya Tanganyika na Zanzibar zijitegemee wakati ile ya
Muungano iwe na Rais wa Muungano atakayeratibu na kusimamia makubaliano ya
muungano huo.
Aidha alisema Katiba Mpya ya Serikali
tatu ni muhimu pia izingatie kero za waislamu zilizodumu kwa miaka 50.
Alisema kama Waislamu walipendekeza
Katiba Mpya ya Serikali tatu, itambue uwepo wa Mahakama ya Kadhi ili kusimamia
kwa mujibu wa sheria za Kiislamu mambo yanayohusu Waislamu kama ilivyo nchi
zingine za Afrika, Asia na Ulaya.
Pia alisema walipendekeza rasimu hiyo
itambue rasmi siku ya Ijumaa kwamba wafanyakazi na wanafunzi wapewe fursa ya
kutosha kufanya ibada kama ilivyo kwa Wakristo.
"Tulipendekeza kwamba baada ya
Serikali kutambua uwepo wa muumba, isiegemee upande wowote wa dini bali iwepo
kwa ajili ya kulinda maslahi ya wenye dini," alisema Katumba.
Alisema wanaikumbusha Serikali kwamba
Waislamu ni wapenda amani na wapo tayari kusaidia kama wadau wakuu wa amani,
lakini wanatahadharisha kwamba amani ya kweli itapatikana tu pale ambapo haki
ya wote itapatikana.
"Ni muhimu kwa Serikali
kuyatafakari kwa kina mapendekezo yetu yakiwemo ya Katiba Mpya ya Serikali
tatu," alisema.
Chanzo: Majira
No comments:
Post a Comment