Saturday, March 15, 2014

Yanga, Azam kikaangoni

Dar es Salaam. Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, inaendelea leo kwa mechi mbili zitakazopigwa kwenye viwanja viwili tofauti, Jamhuri Morogoro na Azam Complex Jijini Dar es Salaam.

Kwenye Uwanja wa Jamhuri, Yanga iliyotolewa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Al-Ahly, inaanzia kwenye uwanja huo kuumana na Mtibwa Sugar ya Morogoro huku Azam FC ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani kupambana na Coastal Union ya Tanga.

Yanga iliyoaga mashindano ya Afrika kwa penalti 5-4, ina fursa ya kupora madaraka ya uongozi wa ligi lakini endapo tu itaifunga Mtibwa Sugar.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo, wakiwa na pointi 38 nyuma kinara Azam FC yenye pointi 40 kileleni. Mbeya City inakamata nafasi ya pili ikiwa na pointi 39.

Endapo itaibuka na ushindi katika mchezo wa leo, Yanga itafikisha pointi 41 na kuishusha Azam hadi katika nafasi ya pili sanjari na kuisukuma Mbeya City katika nafasi ya tatu.

Hata hivyo, Yanga inajivunia  faida ya kuwa na  mechi nyingi mkononi tofauti na Azam na Mbeya City , kwani imeshuka uwanjani mara  17 na ushinda mechi 11, sare tano na kufungwa mchezo mmoja.

Azam tayari  imecheza mechi 18, kati ya hizo imeshinda 11, sare saba na haijapoteza mchezo, wakati Mbeya City imeshuka uwanjani mara 21, imeshinda mechi 10, sare tisa na imenyukwa mara mbili.

Kocha wa  Yanga, Hans Van Der Pluijm ambaye atamkosa winga wake, Mrisho Ngasa aliyeumia wakati wa mechi dhidi ya Al-Ahy ametamka kwamba anataka kutwaa ubingwa ili iwe zawadi ya kuwafuta machozi mashabiki wa timu hiyo wenye majonzi ya kuondolewa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Naye kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa alisema kuwa wanaelekeza nguvu hizo katika mchezo na Mtibwa Sugar ili kuhakikisha wanaondoka na ushindi.

“Mtibwa Sugar wamekuwa wakiisumbua Yanga katika Uwanja wa Jamhuri, lakini hiyo ni hali ya mchezo. Ninachoweza kusema baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa tumeelekeza nguvu katika michezo ya Ligi Kuu,”alisema Mkwasa.

Kwa upande wake, Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime amekiri kwamba mechi hiyo itakuwa ngumu kwa upande wake, lakini amejiandaa kwa mapambano.

Naye, nahodha wa Coastal Union, Juma Nyoso amesema wanaiheshimu Azam kama timu nje ya uwanja lakini si ndani ya uwanja, hivyo dakika 90 ndizo zitatoa jibu nani mbabe kati ya timu hizo.
Chanzo: Mwananchi


No comments: