Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
linakutana kwa dharura kulipigia kura azimio dhidi ya kura ya maoni mkoani
Crimea linaloungwa mkono na Magharibi, huku Marekani na Urusi zikishindwa
kukubaliana juu ya Ukraine.
Kikao hicho cha dharura ambacho
kinapangwa kuanza saa 5:00 asubuhi kwa saa za New York hivi leo (tarehe 15
Machi 2014), kimeitishwa kwa ombi la serikali ya Marekani. Wanadiplomasia
wanasema wanatarajia Urusi kulipigia kura ya veto azimio hilo, lakini bado
haijafahamika ikiwa China nayo itafanya hivyo hivyo au la.
Kawaida Urusi na China huwa na
msimamo mmoja kwenye Baraza hilo la Usalama, hasa kuhusiana na suala la Syria.
Chanzo chengine cha kidiplomasia kimesema kuwa lengo pekee la azimio hilo ni
kuifanya China ijizuwie kupiga kura na hivyo kuitenga zaidi Urusi.
Inasemekana kuwa azimio hilo
limeandikwa kwa lugha ambayo itaishawishi China, kwani haliitaji moja kwa moja
Urusi, halitishii vikwazo na wala kuitaka Urusi kuondoa wanajeshi wake mkoani
Crimea, ambako kawaida imekuwa na kituo cha kijeshi. Msimamo wa China umekuwa
ni kuheshimu uhuru na mamlaka ya taifa na kujizuia kuingilia mambo ya ndani ya
nchi husika.
Kerry, Lavrov washindwa kupata
muafaka
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya
Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, na mwenzake wa Marekani, John Kerry, wameshindwa
kutatua tofauti zao juu ya mkoa huo wa Crimea, hata baada ya mazungumzo yao ya
masaa nyumbani kwa balozi wa Urusi nchini Uingereza hapo jana (tarehe 14 Machi
2014).
Wakizungumza kwa pamoja na waandishi
wa habari baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao, mawaziri hao walionesha wazi
kutokufikia makubaliano yoyote katika suala hilo tete linalozidi kuzigawa
serikali zao, licha ya wote kusema kuwa yalikuwa mazungumzo ya kuridhisha.
Hata hivyo, Lavrov alirejelea msimamo
wa nchi yake kwamba haina nia ya kuingilia kijeshi nchini Ukraine, ingawa
hakuonesha uwezekano wowote wa pande hizo mbili kuwa na msimamo wa pamoja juu
ya hali ya mambo kwenye mkoa wa Crimea.
Kwa upande wake, Kerry alisema baada
ya mazungumzo hayo marefu, mwenzake Lavrov aliweka wazi kwamba "Rais Putin
hayuko tayari kuamua chochote juu ya Crimea hadi kura ya maoni
itakapofanyika", akiongeza kwamba msimamo wa Marekani juu ya kura hiyo ya
maoni unabakia kuwa ule ule kuwa "inakiuka katiba ya Ukraine, na sheria za
kimataifa na tunaamini si halali."
Kwa mara nyengine, Lavrov alizionya
nchi za Magharibi dhidi ya kuiwekea nchi yake vikwazo vya kidiplomasia au vya
kiuchumi kutokana na msimamo wake juu ya Ukraine. Wakaazi wa Crimea watapiga
kura ya maoni ya ama kujiunga na Urusi au kuwa taifa huru hapo kesho, baada ya
bunge la mkoa huo kuamua wiki iliyopita kujiunga na Urusi. Kesho hiyo hiyo pia,
wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wataamua hapo kesho juu ya orodha ya Warusi
watakaolengwa na vikwazo hivyo.
Marekani yawaonya raia wake
Wakati hayo yakiendelea, Wizara ya
Mambo ya Nje ya Marekani imewaonya raia wake juu ya uwezekano wa mapambano ya
kijeshi kwenye mpaka wa Ukraine na Urusi na pia vuguvugu la kuipinga Marekani
nchini Urusi, huku Crimea ikijiandaa na kura hiyo ya kujiunga na Urusi.
Licha ya kusema kwamba haina taarifa
yoyote ya mgogoro wa kijeshi ndani ya Urusi kutokana na wasiwasi uliopo kwenye
eneo hilo au kitisho chochote kwa raia wake, Marekani imesema kupitia
"onyo la safari" kwamba raia wake walio kwenye eneo hilo na wale
wanaopanga kwenye huko wanapaswa kuwa na tahadhari.
Katika kile kinachoonekana kama
makabiliano mabaya kabisa tangu kuanza wakati wa Vita Baridi, Urusi ilituma
wanajeshi zaidi mkoani Crimea siku ya Ijumaa na kutishia kupeleka wanajeshi
kwenye maeneo mengine ya Ukraine kufuatia ghasia zilizotokea usiku wa Alhamis
kwenye mkoa wa Donetsk.
Mwandishi: Mohammed
Khelef/Reuters/AFP/dpa
Mhariri: Amina Abubakar
Chanzo: DW Swahil
No comments:
Post a Comment