Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amesema hana mpango wa kuwahoji Wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na chama hicho kwa sababu ya misimamo yao
inayokinzana na miongozo ya chama, kwa kuwa anawafahamu wote kwa majina na
idadi yao haizidi kumi.
Kauli hiyo ya Kinana inafuatia
taarifa zilizoripotiwa na gazeti hili hivi karibuni kuwa, CCM kimeanza kuwahoji
baadhi ya wabunge wake, ambao ni Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu
ya kupingana na maelekezo ya chama hicho kuhusu Muundo wa Serikali mbili.
“Sisi (CCM) hatuhoji mtu kwa sababu
ya kuwa na msimamo tofauti, kwani hawa wenye msimamo tofauti na chama hawazidi
kumi ama siyo zaidi ya 15,” alisema Kinana na kuongeza;
“Hawa watu mimi nawajua kwa majina,
mmoja (jina tunalo) ni hatari zaidi kwa sababu anaweza kuwakusanya wengine na
kuwashawishi wafuate msimamo wake, lakini waliobaki wote, hawatishi kwa kuwa
wanabaki na misimamo yao wenyewe.”
Kwa mujibu wa habari hiyo, wajumbe
waliohojiwa ni wale wanaotokana na Ubunge wa Jamhuri ya Muungano na ambao
wanataka Muundo wa Serikali tatu. “Ni kweli hata mimi niliitwa na akaniambia
(mwakilishi wa chama) ametumwa aniletee ujumbe kuwa niko kwenye orodha ya watu 90
na nikiendelea na msimamo wangu nitachukuliwa hatua,” alieleza mmoja wa wajumbe
waliodai kuwa wamehojiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Maelezo ya Kinana
Kinana aliliambia gazeti hili kuwa,
kulingana na muundo wa chama hicho tawala, viongozi wanaoweza kuwahoji watu ni
yeye Katibu Mkuu, Makamu Mwenyekiti, Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Waziri Mkuu
na Mwenyekiti wa chama Taifa. “Tena tunafanya hivyo kwenye vikao maalumu na kwa
sababu ambazo haziwezi kuwa siri.”
Kinana alieleza kuwa taarifa kwamba
CCM imewahoji watu 90 kutokana na kuwa na misimamo tofauti na chama hicho
kuhusu Serikali mbili na kura ya wazi, siyo za kweli na anaamini imesambazwa na
watu kwa malengo yao binafsi. Kinana anafafanua kuwa CCM kama chama kikubwa
nchini chenye wafuasi karibu nchi nzima, hakiwezi kudhibiti mitizamo ya watu na
kimsingi tofauti za mitazamo ndiyo msingi wa demokrasia.
Novemba 20 mwaka 2012 akizungumza
katika kipindi cha Jenerali on Monday kinachorushwa na Kituo cha Televisheni
cha Channel Ten, Kinana alitoa onyo kwa makada wasaliti kuwa atasimamia
utekelezaji wa uamuzi wa Halmashuari Kuu ya CCM (Nec) ya kuwabaini na kuwaondoa
viongozi wanaokwenda kinyume na matakwa ya chama na kukipaka matope.
Kura ya wazi na Serikali mbili
Katika hatua nyingine, Kinana
alizungumzia msimamo wa chama hicho wa kura ya siri na muundo wa Serikali
mbili, akieleza kuwa siyo jambo la ajabu, kwani katika mchakato wa kutunga
katiba, kila kundi lina maoni na mtazamo wake na kuutetea kwenye mijadala.
“Wanaosema kuna vyama havina msimamo
pale bungeni ni waongo. Siyo vyama tu, kila kikundi kina msimamo unaotokana na
uchambuzi wao wa hali ya siasa nchini na wanachofikiri kina masilahi kwa nchi
na watu wanaofuata mtazamo wao. Hawawezi kuniambia kama Lipumba (Profesa
Ibrahim) na Mbowe (Freeman), hawana wanachosimamia kwenye mjadala huo wa Bunge
Maalumu,” alisema na kusisitiza:
“Watanzania wasitarajie miujiza,
lazima mivutano ya aina hiyo iwepo, kwani kila kundi linajitahidi kupenyeza
mawazo yake na wanaoitetea misimamo hiyo ni watu. Kikubwa hapa sasa ni
uvumilivu, watu wavumiliane na wazungumze kwa hoja na mwisho wa yote wafikie
mwafaka.”
Alipoulizwa kama ni kweli CCM imekuwa
ikiwashinikiza wajumbe wake kusimamia matakwa ya chama hicho, alijibu “Siyo CCM
tu, CUF wanakutana na Chadema wanakutana, tena kila siku. Hili ni jambo la
kawaida.”
Anasema tatizo siyo chama kuwa na
msimamo, bali chama kutokukubali kubadili misimamo yake hata kama haikuwa sawa.
Unaweza kuwa na msimamo wako, lakini ukaja mbele ya wenzako, ukagundua kuwa
hauko sahihi, ikifikia hapo unapaswa kulegeza kamba ili uingize mawazo ya
wenzako pia kwenye hoja zako, alisema.
Wito kwa Wajumbe wa Bunge la Katiba
Kinana ametoa wito kwa Wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba akiwataka watambue kuwa Tanzania siyo nchi ya kwanza
kutengeneza katiba.
Alisema zipo nchi nyingi duniani,
ikiwamo India, Indonesia, Columbia, Kenya na Pakistan ambazo zilitumia muda
mrefu zaidi kutunga katiba zao.
“Sisi kutumia majuma matatu
kutengeneza kanuni za kuongoza Bunge Maalumu la Katiba, ni hatua nzuri
tunayopaswa kujivunia,” alisema.
Kinana aliendelea kueleza kuwa pamoja
na tofauti zinazojitokeza katika mijadala ya Bunge hilo Maalumu, makundi
yanayounda Bunge hilo yanapaswa kutambua utaifa na uzalendo na ikilazimika
waache tofauti zao ili wawe na mwelekeo wa pamoja katika kufikia mwafaka
unaokusudiwa.
“Kwa hali hiyo pamoja na tofauti
zetu, tusiondoke kwenye lengo. Mimi naamini katiba tunayoitaka itapatikana ila
safari ya kuipata ni ndefu na ngumu.”
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment