Waziri Wa Afrika Mashariki Mh. Sitta
Mtangamano wa Afrika Mashariki
umekuwapo kwa muda mrefu tangu wakati wa ukoloni, nchi ya Tanganyika, Kenya na
Uganda zikiwa makoloni ya Uingereza.
Uingereza ilirithisha nchi hizo kwa
kuwa na mipango yake kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Baada ya ukoloni mwaka 1967 nchi hizo
ziliungana ili kuendesha uchumi uliotakana na miundombinu iliyoachwa na
wakoloni.
Hata hivyo, kwa mara ya kwanza
muungano huo haukufika mbali kwani mwaka 1977 Jumuiya ya Afrika Mashariki
ilivunjika.
Sababu za kuvunjika kwa jumuiya hiyo
zilikuwa ni za kisiasa na kiuchumi. Kisiasa, kwanza itikadi za nchi hizo
zilitofautiana.
Kwa mfano, wakati Tanzania ilikuwa
ikifuata sera ya Ujamaa na Kujitegemea, Kenya ilifuata sera za kibepari na
Uganda ilikuwa ikifuata mfumo wa mchanganyiko.
Vilevile kulikuwa na tofauti kati ya
viongozi; Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere hakupatana na Rais wa
Uganda, Yoweri Museveni. Kuhusu sababu za uchumi, nchi za Uganda na Tanzania
hazikuridhishwa na mgawanyiko wa rasilimali hasa ikidaiwa kuwa Kenya ilichukua
sehemu kubwa ya uchumi hasa viwanda.
Baada ya kuvunjika kwa jumuiya hiyo,
ilipita miaka 22 ndipo wazo la kuifufua likarejeshwa tena. Mwaka 1999, nchi
hizo zilitia saini mkataba wa kuanzisha upya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Jumuiya hiyo ililenga kufikia hatua
kadhaa ikiwa ni pamoja na umoja wa forodha, soko la pamoja na, umoja wa sarafu
na shirikisho la siasa. Mwaka 2007, wanachama wa jumuiya hiyo waliongezeka
baada ya nchi za Rwanda na Burundi kujiunga.
Licha ya changamoto za hapa na pale,
lengo ni kuhakikisha kuwa jumuiya hiyo haipasuki kama ilivyotokea mwaka 1977.
Nafasi ya Tanzania kung’ara
Licha ya nchi hizo kuwa chini ya
mtawala mmoja wa kikoloni (mbali na Rwanda na Burundi), bado inaelezwa kuwa
Tanzania ina nafasi kubwa ya kuendelea kiuchumi kuliko wanachama wengine wa
Afrika Mashariki.
Akizungumza katika mjadala wa bajeti
za Afrika Mashariki ulioandaliwa na taasisi ya utafiti wa jamii na uchumi
(ESRF) juzi jijini Dar es Salaam, mwakilishi kutoka Wizara ya Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dk Abdulla Makame anasema Tanzania ina kila sababu ya
kuendelea kupitia ushirikiano huo.
“Tunazo fursa nyingi tu za kuendelea;
tunayo ardhi kubwa na yenye rutuba, tunazo rasilimali ingawa kwa sasa kuna
janga la ujangili wa meno ya tembo. Tuko pia kwenye eneo zuri la kijiografia.
“Tofauti na nchi nyingine za Afrika
Mashariki, Tanzania inapakana na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Malawi na Msumbiji. Hakuna nchi nyingine
ya Afrika Mashariki inayopakana na nchi wanachama wote kwa wakati mmoja,” Dk
Abdulla.
Bajeti Jumuiya ya Afika Mashariki
Pamoja na kuwapo kwa fursa hiyo
anasema bado bajeti ya Serikali hailingani na matakwa ya maendeleo ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki.
“Bajeti ya Taifa hailingani na
malengo na mipango ya maendeleo ya Afrika Mashariki. Tungetarajia kuwa bajeti
za maendeleo ya jumuiya ziwekwe moja kwa moja kwenye wizara husika,” anasema Dk
Makame.
Anashauri waandaaji wa bajeti
kuangalia vipaumbele vya jumuiya hiyo na kukamilisha sera yake.
“Tunayo Reli ya Kati iliyojengwa na
Wajerumani wakati wa ukoloni. Ilitakiwa reli hii itumike kuleta maendeleo ya
uchumi kwa Tanzania, lakini bado haina viwango vya kimataifa,” anasema Dk
Abdulla.
Akijibu hoja hizo, Kamishna Msaidizi
wa bajeti kutoka Wizara ya Fedha, Emmanuel Tutuba anasema tayari bajeti ya
Serikali imeanza kutekeleza mahitaji ya jumuiya hiyo.
“Nikiangalia kwenye bajeti yetu naona
kuna mambo mengi yameanza kutekelezwa na mengine yako ngazi ya kimataifa. Kwa
mfano, sekta ya umeme, ukiangalia takwimu na uwekezaji wa Serikali utaona lengo
ni kuuza umeme kwa nchi za Afrika Mashariki. Maendeleo ni mazuri hasa kwa umeme
wa gesi kutoka Mtwara. “Hata ukiangalia upande wa kilimo, wenzetu wa NRFA
walinunua mahindi mengi na kuyauza nchini Kenya, wanategemea kupata Sh8
bilioni.
“Hata ukiangalia viwanja vya ndege
kwa mfano, wa Kigoma, umejengwa mahsusi kwa ajili ya kuunganisha Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo, Rwanda na Burundi. Kwa hiyo tayari kuna utekelezaji wa
bajeti kwa maendeleo ya Afrika Mashariki.”
Biashara imeongezeka zaidi
Naye Ofisa wa Shirikisho la Chama cha
Wafanyakazi, Kilimo na wenye Viwanda (TCCIA), Adam Zuku anasema: “Tangu
tumejiunga, ukubwa wa biashara umeongezeka tofauti na zamani, haijaridhisha,
lakini inakwenda vizuri.
“Tunapozungumzia mtangamano huu wa
sasa ni tofauti na wa zamani.
Mtangamano wa sasa ni wananchi zaidi
kuliko zamani ambapo ilikuwa kwa viongozi pekee. Siku hizi mambo yanafanywa na
wataalamu,” anasema. Anatoa mfano wa ukuaji wa biashara akisema hata mashirika
ya viwango ya jumuiya hiyo sasa yanatambuana na kutoa maagizo yanayofanana.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment