Ukraine imetia saini vifungu vya
kisiasa vya mkataba vya ushirikiano katika mkutano wa viongozi wa Umoja huo
mjini Brussels huku mgogoro wa Crimea ukizidi kupalilia mvutano kati ya Moscow
na nchi za magharibi.
Kwa namna hiyo Umoja wa Ulaya
unabainisha uungaji mkono thabiti kwa Ukraine inayowakilishwa mkutanoni na
waziri mkuu Arseniy Yatsenyuk.
"Kutiwa saini vifungu vya
kisiasa vya mkataba wa ushirikiano ni "thibitisho kamili la mshikamano
pamoja na Ukraine" amesema rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy na
kuongeza tunanukuu" mkataba huo utawapatia wananchi wa Ukraine matumaini
ya hali bora ya maisha wanayoistahiki." Mwisho wa kumnukuu
Wakati huo huo Umoja wa ulaya
unafungua njia ya kuondowa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoagiziwa kutoka
Ukraine ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuinua shughuli zinazozorota za kiuchumi.
Brussels pia inazingatia uwezekano wa kuipatia Ukraine msaada wa kiuchumi wenye
thamani ya Euro bilioni 11.
Umoja wa Ulaya waionya Urusi
Kansela Angela Merkel akihudhuria
mkutano wa kilele wa Umoja wa ulaya mjini Brussels
Wakati wanainyooshea mkono
Ukraine,viongozi wa Umoja wa ulaya wanaokutana mjini Brussels wanazidisha
shinikizo kwa Urusi kufuatia uamuzi wake wa kuimeza Crimea.Jana viongozi hao
wameongeza marufuku ya safari na kuzuwiliwa milki za maafisa wa serikali za
Urusi na Ukraine na kufikia watu 33.
Majina ya watu 12 zaidi ya wale
waliotangazwa awali,kwa mujibu wa mwenyekiti wa Umoja wa ulaya Van Rompuy
yatatangazwa baadae .
Viongozi wa Umoja wa ulaya
wameufutilia mbali mkutano wa kilele uliopangwa kuitishwa June tatu ijao pamoja
na Urusi.Hata hivyo wamejizuwia kutangaza vikwazo vya kiuchumi.Viongozi hao
wameonya lakini hatua kama hizo zitafuata ikiwa Urusi itazidi kupalilia mgogoro
wa Crimea ."Tumaweka wazi kabisa,tuko tayari bila ya shaka kwenda mbali
zaidi ikiwa hali itazidi kuwa mbaya -vitakavyofuata wakati huo ni vikwazo vya
kiuchumi."Anasema kansela Angela Merkel
Mbali na viongozi wa Umoja wa
Ulaya,Marekani pia imezidisha idadi ya warusi na waukrain waliowekewa vikwazo
na kufikia 16 na kufungua njia ya vikwazo pia kuwekwa dhidi ya sekta muhimu za
uchumi nchini Urusi ikiwa Moscow haitabadilisha mkondo wa mambo kuhusu Ukraine.
Baraza la juu la bunge la Urusi laidhinisha Crimea iwe sehemu ya Urusi
Mjini Moscow kwenyewe lakini baraza
la juu la bunge la Urusi limeidhinisha hii leo mpango wa kuijumuisha Crimea na
Urusi.Mpango huo ulikwisha idhinishwa kwa wingi mkubwa hapo jana na bunge.Na
rais Vladimir Putin amesema nchi yake itajizuwia kwa sasa kutangaza vikwazo
kujibu vile vilivyowekwa na Washington.
Mwandishi: Hamidou
Oummilkheir/dpa/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef
Chanzo: DW swahili
No comments:
Post a Comment