Benki ya Dunia imeridhia kutoa dola
milioni 73 kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mpango wake wa
ujenzi wa bwawa la Inga, ambalo ndilo kubwa kabisa duniani la kuzalisha umeme
kutumia nguvu ya maji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Benki ya Dunia, fedha hizo dola milioni 73 zikichanganywa na zengine dola
milioni 33 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, zitasaidia kufadhili utafiti wa
kiufundi kuchunguza hali ya mazingira karibu na eneo la bwawa na kuhakikisha
mradi huo ni endelevu.
Fedha hizo pia zitasaidia kuzindua
usimamizi wa maendeleo ya Inga unaojitegemea ambao unatarajiwa kufuata mfumo
mzuri wa Kimataifa katika kuuendesha mradi huo, na hata kuteua mashirika
binafsi yatakayosaidia katika kuufadhili zaidi mradi wa bwawa la Inga.
Hata hivyo, Benki ya Duinia
imeiorodhesha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kama moja ya maeneo 10 yaliyo
magumu kufanyia biashara. Kwa miongo kadhaa sasa miradi ya kulipanua bwawa hilo
la Inga imeshidnwa kutokana na migogoro na vita vinavyotokea mara kwa mara
nchini humo, huku wanamazingira wakionya kuwa mipango ya mabwawa makubwa
inajulikana kwa kucheleweshwa kwa muda mrefu na kuwa na gharama kubwa.
Benki ya Dunia inakadiria kuwa Kongo
itakuwa na uwezo wa kutoa takribani jigawati 100 ya nguvu za umeme, ikiwa ni ya
tatu duniani baada ya China na Urusi. Lakini ni asilimia 9 pekee ya idadi ya
raia wa Congo milioni 65 walio na uwezo wa kupata umeme huku katika sekta ya
madini inayochangia kiwango kikubwa cha uchumi wa nchi hiyo uhaba wa umeme
ukisalia kikwazo kikubwa.
Ramani hii inaonyesha njia ndefu ya
kusafirisha umeme kutoka Inga hadi Afrika Kusini
Ramani hii inaonyesha njia ndefu ya
kusafirisha umeme kutoka Inga hadi Afrika Kusini
Lakini kwa sasa mpango wa Afrika
Kusini kununua umeme kutoka Inga, umefufua mazungumzo ya mradi huo mkubwa. Kwa
sasa mashirika matatu makubwa ya kimataifa yanapigania kandarasi ya kujenga
bwawa hilo linalojulikana kama Inga ya tatu, na kuuza nguvu ya umeme
inayopatikana inayokadiriwa kuwa megawati 4,800.
Hii ni takriban mara tatu ya nguvu ya
umeme iliyokuwa inatolewa kwa mabwawa mawili ya Inga, yalioko kwa muda mrefu
sasa na yalioharibiwa kutokana na madeni ya serikali ya Congo na
wafanyabiashara walioogopa kuwekeza katika miradi hiyo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Congo,
Augustin Matata Ponyo, ametoa taarifa akisema kuwa mradi wa Inga ni mradi
unaoweza kuibadilisha Afrika katika karne hii ya 21.
Wakati huo huo kundi moja liitwalo
International Rivers limeukosoa mpango huo kwa kutokuwa na manufaa zaidi kwa
raia wa nchi hiyo na kutoa wito kwa Benki ya Dunia kufadhili mipango midogo ya
kawi kama ya umeme wa kutumia jua ambayo limesema haitadhuru mazingira kwa
kiwango kikubwa.
Mwandishi: Amina Abubakar/ Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef
DW.DE
No comments:
Post a Comment