Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976
MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka
Tanzania bara wanatarajia kushuka dimbani jumapili ya wiki hii kuwakabili
maafande wa JKT Ruvu kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kikosi cha Yanga chini ya kocha mkuu,
Mhoalanzi Hans Van der Pluijm kimeingia kambini jana jioni katika Hoteli ya
Kiromo, huku kikiendelea kufanya mazoezi katika Uwanja wa Boko Beach Veterani.
Yanga waliopo nafasi ya pili kwa
kujikusanyia pointi 46, pointi 7 nyuma ya Azam fc wenye pointi 53, watakuwa
wanacheza mechi ya raundi ya 23 jumapili, huku wakisubiri kiporo chao dhidi ya
Kagera Sugar aprili 9 mwaka huu uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.
Mechi iliyopita jijini Tanga, Yanga
walipoteza mchezo kwa kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wao, Mgambo JKT na
kuweka rehani ubingwa wao msimu huu.
Yanga wamebakisha mechi nne na kama
watashinda zote watafikisha pointi 58 ambazo Azam fc pekee ndio wataweza
kuzifikia kama watashinda mechi zao tatu zilizosalia.
Hata hivyo taarifa njema kwa
mashabiki wa Yanga ni kuwa Mlinda mlango Deoragtias Munish "Dida"
aliyekuwa majeruhi kwa takribani wiki mbili, ameshapona majeraha na ameungana
na wenzake kambini tayari kwa maandalizi ya mchezo huo.
Katika hatua nyingine, Yanga kupitia
tovuti yao rasmi wamekanusha taarifa zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya
habari kwamba wachezaji wake, kiungo, Athuman Idd, beki Kelvin Yondani na
Mlinda mlango, Juma Kaseja wamesimamishwa kutokana na timu kufungwa na Mgambo
JKT.
"Taarifa hizo hazina ukweli,
wachezaji hao hawajafukuzwa na wapo wanaendelea na mazoezi pamoja na
wenzao". Alifafanua taarifa ya Yanga.
Pia Yanga wameviomba vyombo vya kutoa
taarifa za ukweli na sio kupotosha jamii na mwisho wa siku kuwapa usumbufu
viongozi kufanya kazi ya kukanusha.
Mchezo wa jumapili utakuwa mgumu kwa
timu zote kutokana na kusimama maeneo mawili tofauti kwenye msimamo wa ligi
kuu.
Yanga wapo nafasi ya pili na
wanapambana kutetea ubingwa wao walioutwaa msimu huu.
Wataingia katika mchezo huo wakiwa na
kumbukumbu ya kuwafunga JKT Ruvu mabao 4-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza mwaka
jana.
Haitakuwa kazi nyepesi kwa Yanga
kumfunga aliyekuwa kocha wake msaidizi ambaye kwasasa ni Kocha mkuu wa JKT
Ruvu, Fredy Felix Minziro.
Minziro na kikosi chake wapo nafasi
ya 9 kwa kushuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 28 kibindoni.
Maafande hao wataingia uwanjani
wakiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 mechi iliyopita dhidi
ya Vibonde, Rhino Rangers kwenye uwanja wa Azam Complex.
Mechi ya jumapili ni muhimu kwao
kwasababu wanahitaji zaidi pointi ili kujiweka mazingira mazuri ya kubakia ligi
kuu.
Uzoefu unaonesha kuwa timu zilizopo
katika hatari ya kushuka daraja huwa zinacheza kwa kujituma zaidi, na ndio
maana Mgambo JKT walipambana na Yanga ndani ya dakika zote 90 na kushinda.
Kwa jicho la harakaharaka, unaweza
kuwapa asilimia kubwa Yanga kuwa watashinda mchezo huo, kutokana na mazingira
yao.
Kupoteza au kutoa sare kutazidi
kuwaweka Yanga mazingira magumu zaidi ya kutetea ubingwa wao.
Matokeo yanayowafaa pekee ni ushindi,
kwasababu moto wa Azam fc kueleka kutwaa ubingwa ni mkali sana.
Itakuwa mechi muhimu kwa Yanga, na
kocha mkuu Pluijm atahitaji kutuliza akili zake kwani sasa matokeo
hayatabiriki.
Haikuwa rahisi kuamini kama Mgambo
wangewafunga Yanga waliokamilika pale Mkwakwani, lakini mpira una matokeo ya
ajabu wakati fulani.
Yanga wanatakiwa kuingia jumapili kwa
tahadhari kubwa kwasababu kiwango cha sasa cha JKT Ruvu si cha kubeza. Wanaweza
kufanya lolote na kuwaharibia zaidi wanajangwani.
Chanzo:Shaffihdauda.com
No comments:
Post a Comment