WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kikiendelea kumwandama kwa kejeli Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba, mmoja wa makamishna wa tume hiyo naye ameonja ‘joto ya
jiwe’ kwenye kamati za Bunge Maalumu la Katiba.
Mjumbe huyo ni Al- Shymaa Kweigyir
(mbunge), ambaye jana alishulutishwa na
wajumbe wenzake wa CCM kupiga kura ya wazi ili kukataa kuafiki ibara ya kwanza
ya sura ya kwanza ya rasimu.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Kwegyir
alikumbana na zahama hiyo wakati wa kupiga kura katika kamati yake namba 12
inayoongozwa na Paul Kimiti.
Ingawa Kimiti ambaye amekuwa mgumu
kutoa taarifa za kamati yake kwa waandishi hakupatikana kuthibitisha tukio hilo,
gazeti hili lilidokezwa kuwa Kwegyir aliomba kupiga kura ya siri ambayo CCM
wanaikwepa akitaka kulinda uhuru wake kwa sababu ana masilahi na tume.
Kwa kawaida, Kwegyir kama mmoja wa
wajumbe wa tume iliyoandaa rasimu lazima
angepiga kura ya kuunga mkono mapendekezo yao.
Kamati namba 12 ina wajumbe 53 ambapo
36 wanatoka Bara na 17 Zanzibar na ili kufikia theluthi mbili ya kura kwa Bara
zilitakiwa 24 na Zanzibar 12.
Kwa mujibu wa chanzo hicho,
zilipopigwa kura za kuamua ibara ya kwanza ya sura ya kwanza, theluthi mbili
haikupatikana kwa pande zote, ndipo CCM wakaaza kusaka ‘mchawi’ anayekwamisha.
Tanzania Daima lilidokezwa kuwa
baadhi ya wajumbe wa CCM wakiwemo mawaziri walianza kumzomea Kwegyir wakimwita
msaliti kwa sababu ndiye alipiga kura ya siri tofauti na msimamo wa chama chao.
“Hali hiyo ilimkasirisha Kwegyir hadi
akafikia hatua ya kutoa machozi, akishangaa kuona ananyimwa haki yake wakati
kanuni zinaruhusu mjumbe kupiga kura aitakayo kati ya wazi na siri.
“Baada ya hali kuwa mbaya, wajumbe wa
upinzani waliingilia kati wakipinga kitendo hicho ingawa CCM waliendelea
kumwandama wakitaka atamke wasikie kama anakubali pendekezo la ibara hiyo au
hapana,” alisema msiri wetu.
Hata alipolazimishwa kupiga kura ya
wazi kwa kutamka, inadaiwa kuwa Kwegyir alilikubali pendekezo la tume kuhusu
muundo wa muungano wa serikali tatu.
Mjumbe Edward Lowassa (Mbunge wa
Monduli) ndiye anadaiwa kuokoa jahazi hilo baada ya kuingilia kati na kuwasihi
wajumbe wenzake kutulia, hivyo shughuli ya upigaji kura kusimama kwa muda.
Miongoni mwa viongozi wakubwa wa CCM
wanaounda kamati hiyo ni, Prof. Anna Tibaijuka (waziri), Pandu Ameir Kificho
(Spika Zanzibar), Binilith Mahenge (naibu waziri) na Aden Rage (mbunge).
Wapo pia Michael Laizer (mbunge),
Ahmed Shabiby (mbunge), Amos Makalla (naibu waziri), Seleman Jaffo (mbunge),
Henry Shekifu (mbunge na mwenyekiti wa CCM Tanga), Jesca Msambatavangu (mjumbe
na mwenyekiti wa CCM Iringa) na wengine.
Theluthi mbili Zanzibar utata
Theluthi mbili ya kuamua ibara na
sura za rasimu ya Katiba imekuwa kikwazo kwa kamati nyingi za Bunge Maalumu la
Katiba hususan upande wa wajumbe wa Zanzibar.
Hali hiyo ilijitokeza jana wakati
kamati hizo 12 zilipopiga kura ya kuamua vifungu vya ibara za sura ya kwanza na
sita huku ibara ya kwanza inayopendekeza muundo wa serikali tatu ikileta
mgawanyiko.
Katika ibara ya kwanza ya sura ya
kwanza (1), rasimu inapendekeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na
Shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na Jamhuri ya Tanganyika na
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya hati ya makubaliano ya muungano ya
mwaka 1964, zilikuwa nchini huru.
Wakizungumza na waandishi wa habari
jana, baadhi ya wenyeviti wa kamati hizo walisema kuwa licha ya wajumbe
kuafikiana katika baadhi ya ibara, lakini katika suala hilo la shirikisho
waligawanyika kulingana na pande za muungano.
Hadi jana mchana hakuna kamati hata
moja iliyokuwa imepata theluthi mbili kwa pande zote za muungano katika suala
hilo la shirikisho ambapo wajumbe wengi wa CCM wanataka pendekezo hilo lifutwe
kwa madai inakwenda kinyume cha hati ya makubaliano ya Muungano.
Ili kufikia theluthi mbili kwenye
kamati yenye wajumbe 52 au 53, upande wa Tanzania Bara wenye wajumbe kati ya 33
hadi 37 unatakiwa kupata kura zaidi ya 23 za ndiyo na upande wa Zanzibar wenye
wajumbe kati ya 15 hadi 19 zinahitajika kupata zaidi ya 10.
Kwa upande wa Bara ni rahisi kwa CCM
kupata theluthi mbili kwa sababu ina wajumbe kati ya 23 hadi 28 kila kamati
bila kutegemea za wajumbe wa kundi la kuteuliwa lakini kwa Zanzibar ni vigumu
kwani idadi ya wajumbe wake inalingana na ile ya CUF.
Kutokana na msimamo wa vyama hivyo
kuwa tofauti katika suala la muundo wa muungano ni vigumu kupata theluthi hiyo
ya kura kwa upande wa Zanzibar.
Ibara ya pili kuhusu eneo la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na ile ya tano kuhusu tunu za taifa zilizua ubishano
mkali katika kamati nyingi kiasi cha baadhi ya wajumbe kuleta majedwali ya
marekebisho wakiongeza na kupungua baadhi ya vitu.
Mwenyekiti wa kamati namba moja, Ummy
Mwalimu, alisema kuwa katika sura ya kwanza yenye ibara tisa, ni ibara mbili za
sita na tisa ambazo zilipata theluthi mbili ya kukubalika kwa pande zote.
Mwenyekiti wa kamati namba tano,
Hamad Rashid Mohammed, alisema kwa sura ya kwanza, ibara ya pili, tano na saba
zilikataliwa kwa theluthi mbili huku ibara ya kwanza ikikosa idadi hiyo ya kura
kwa upande wa Bara.
Naye Anna Abdallah, mwenyekiti wa
kamati namba 10, alisema hawakukubaliana kwa ibara nyingi na hivyo kufanya
theluthi mbili kushindikana hasa upande
wa Zanzibar.
Hali kama hiyo ya wajumbe
kutofautiana kuhusu muundo wa muungano ilijitokeza pia kwa kamati namba 11
inayoongozwa na Anne Killango Malecela na nane ya Job Ndugai, ambazo wajumbe
wake walitarajiwa kupiga kura jana jioni.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment