OPERESHENI ya kusafisha jiji ili
kuwaondoa wafanyabiashara wadogo (wamachinga) kwenye maeneo yasiyo rasmi,
imewageukia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na ombaomba.
Operesheni hiyo inaendeshwa na
Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Jeshi la
Polisi.
Akizungumza na Tanzania Daima,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema uongozi wa
Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na
Jeshi la Polisi wanaendesha operesheni hiyo kwa ajili ya mkazi wa wilaya hiyo
kufanya kazi zake kwa kufuata sheria.
Alisema hatua ya kuwaondoa
watoto hao na ombaomba imetokana na
ongezeko la watu hao, ambao wengi wao wamekuwa wakifanya vitendo hivyo huku
wakiwa wanajiweza kifamilia.
“Sisi ni wasimamizi wa operesheni
hiyo, wahusika wakuu ni halmashauri. Hata hivyo, wanapowaondoa mitaani yapo
maeneo ya kuwahifadhi,” alisema Minangi.
Alisema operesheni hiyo ya safisha
jiji kwa utaratibu ulivyopangwa ni kwamba haitabakiza chochote na kusema kuwa
kila anayejijua kuwa anakiuka sheria ni vema akajiepusha na vitendo hivyo kabla
ya kufikiwa na mkono wa sheria.
Kamanda Minangi alisema operesheni
hiyo inakwenda sambamba na zuio la pikipiki, bajaji na guta kuingia katikati ya
jiji.
Jiji la Dar es Salaam sasa
linaonekana kuwa safi ikiwemo hifadhi ya barabara kurudi kwenye hali ya kawaida
na kuondoa msongamano, kutokana na operesheni hiyo iliyoanza siku mbili
zilizopita.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment