Wednesday, April 9, 2014

Matapeli wajipenyeza TCRA

MAMLAKA ya Mawasiliano imebaini kuwa uwepo wa mtandao wa matapeli wanaotumia jina la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutumia tovuti iitwayo “TCRA Foundation”, inayodanganya kutoa mikopo kwa maendeleo kwa watu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Prof. John Nkoma, tovuti inayotumika ni http://tcra-foundation.wix.com/tcrafoundation.

Alisema mtandao huu umetengenezwa kwa kutumia picha zilizopo kwenye mitandao mbalimbali  zikiwaonyesha Rais Jakaya Kikwete, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makawe Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Prof. John Nkoma.

Aidha mtandao huu unadai kuwa mamlaka kwa kushirikiana na kampuni za simu za Vodacom na Tigo pamoja na Benki ya CRDB na NMB zinashirikiana kuendesha foundation hiyo.

“Mamlaka ya Mawasiliano inawatahadharisha wananchi kuwa haina “Foundation” yoyote ya kutoa misaada ya fedha. Mtandao huu unatumika kuwalaghai wananchi na kuwaibia fedha zao kwa kuwataka watume fedha za kujiunga na mtandao huo kwa namba za simu za Tigo na Vodacom zinazoonyesha kusajiliwa kwa jina la Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania. Sio kweli na ni wizi na udanganyifu,” alisema.

Prof. Nkoma alisema Mamlaka ya Mawasiliano inawataka wananchi kuwa na tahadhari na watu hawa ambao hutumia mitandao ya mawasiliano ya simu na intaneti kufanya utapeli kwa kutotuma fedha wala kujiunga na mitandao ya namna hiyo.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: