SIKU mbili baada ya Ikulu kutoa
taarifa ya kejeli dhidi ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba, wanasiasa, wasomi, viongozi wa dini na wanaharakati wameitaka
Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete kumwomba radhi yeye pamoja na wajumbe wa tume
yake.
Akizungumza na Tanzania Daima jana,
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,
alisema ukirejea kauli ya Rais Kikwete wakati akizindua Bunge la Katiba na
kauli ya Ikulu juzi dhidi ya Warioba, utabaini kuwa kuna hila na chuki kubwa
kati ya Ikulu, Warioba na tume yake.
Dk. Slaa alisema anaamini Jaji
Warioba anasema ukweli kwani katika mazingira ya kawaida, isingewezekana baada
ya kuwasilisha hotuba yake bungeni, usiku ule ule wakiwa mjini Dodoma, yeye na
wajumbe wa tume yake wangekabidhi ofisi na kunyang’anywa magari.
“Nikirejea kauli ya Rais Kikwete
bungeni ambapo jina la Jaji Warioba alilitaja zaidi ya mara sita, ukiunganisha
na kauli ya Ikulu na msimamo wa CCM, utabaini kwamba kuna hasira kubwa dhidi ya
Warioba kutokana na maoni aliyokusanya kutoka kwa wananchi. Rais na CCM
wanaonyesha wazi kwamba hawaitaki katiba mpya,” alisema Dk. Slaa.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema Ikulu ikubali kwamba ilitumia
lugha ya kejeli na dharau kwa Jaji Warioba, hivyo iangalie namna ya kumuomba
radhi.
“Kwa wananchi waliofuatilia
majibishano ya Ikulu na Jaji Warioba, watakubaliana nami kwamba wamemdhalilisha
mzee wetu Warioba, hivyo msemaji wake ni vyema akaangalia namna ya kuyamaliza
kuliko kuendelea kulumbana hadharani,” alisema
Dk. Bana.
Alisema Ikulu ilipaswa itoe maelekezo
ya makabidhiano kwa katibu mtendaji wa tume hiyo na siyo kuwadhalilisha wajumbe
hao mjini Dodoma mara baada ya Mwenyekiti wao, Jaji Warioba kuwasilisha rasimu
ya pili ya katiba mbele ya wajumbe wa Bunge hilo linaloendelea.
“Ikulu haikuwa na sababu ya kutoa
kauli ya kashfa dhidi ya Jaji Warioba, hata kama alikosea. Wananchi wengi
wanaofuatilia mchakato wa katiba, wanafahamu kazi yake nzuri akisaidiana na
wajumbe wenzake. Kimsingi walistahili sifa na siyo kuwakejeli,” alisema Dk.
Bana.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, alisema
kitendo cha Ikulu kutoa taarifa yenye maneno ya kejeli kwa Jaji Warioba ni sawa
na kumvua nguo za ndani hadharani.
“Nimejisikia vibaya niliposikia
taarifa ya Ikulu, ni kama imemvua nguo za ndani hadharani… hakupaswa kufanyiwa
hivyo. Ikulu ilipaswa kutumia burasa ya kufanya makabidhiano kutokana na kazi
nzuri aliyoifanya kwa Watanzania,” alisema Askofu Bagonza.
Askofu Bagonza alisema kama Ikulu
ilivyomuamini, kumteua na kufanya hafla ya kumwapisha Warioba na wenzake 30,
vivyo hivyo siku ya makabidhiano ya kuhitimisha kazi hiyo ingefanywa kulingana
na umuhimu wa kazi yao.
“Hakuna jambo kubwa la historia
linalomalizwa kwa kejeli ama malumbano, tumezoea kuona katika harusi na misiba
baada ya kufanyika ama kumalizika, watu huvunja kamati zake kwa sherehe ndogo
za kumalizia mabakia, ndivyo ambavyo tulitarajia Ikulu ifanye hivyo kwa Jaji
Warioba. na kuongeza
“Nimesoma katika mitandao ya kijamii
namna baadhi ya watu wakipinga hoja za Jaji Warioba kuhusu rasimu aliyoitoa, na
hata malalamiko yake ya kutupiwa virago… hivi haiwezekani kupinga hoja zake
bila ya kumtukana?” alihoji Askofu Bagonza.
Alisema Ikulu na Watanzania wanapaswa
kufahamu kwamba hakuna mzalendo aliyebakia nchini zaidi ya Jaji Warioba, hata
kama wapo wanaomkejeli.
“Sina shaka na uzalendo wa Jaji
Warioba anaouonyesha katika nchi yake, tena ndiye mfano wa kuigwa kwa wote
wanaotaka kuwa wazalendo,” alisema Askofu Bagonza.
Katika hatua nyingine, Kaimu
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Hebron Mwakagenda, alisema
kinachofanyika sasa ni kuwatoa watu kwenye mawazo ya Bunge la Katiba.
Mwakagenda alisema kila kunapokuwa na
jambo la msingi, kuna watu wanaingiza mambo yasiyofaa.
“Walianza na posho, mara kura ya
wazi, mara saini imeghushiwa, sasa suala la Warioba na majibizano yasiyo na
tija na Ikulu, mwacheni Warioba ameshamaliza kazi yake, lakini Salva akumbuke
watu wazima hawapaswi kunenewa maneno yasiyo na msingi, Ikulu kutoa maneno
makali sio uzalendo,” alisema.
Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu
(Tahliso), pia imeeleza kusikitishwa kwake na kauli za Ikulu za kumdhalilisha
Jaji Warioba.
Rais wa Tahliso, Musa Mdede, alisema
jana kuwa jumuiya hiyo haijafurahishwa na kilichosemwa na Ikulu dhidi ya Tume
ya Jaji Warioba.
Mdede alisema kumdhalilisha Warioba
kwa kazi aliyoifanya ni sawa na kumtusi, kwani hakufuata maoni ya chama, mtu,
bali alifanya kazi kutokana na maoni ya wananchi.
Juzi, taarifa ya Kurugenzi ya
Mawasiliano Ikulu iliyosainiwa na Salva Rweyemamu, ilisema Jaji Warioba ni
mnafiki kwa kujifanya hajui ukomo wa tume yake.
Awali katika taarifa yake kwa vyombo
vya habari jana, Jaji Warioba alisema ameiona taarifa ya serikali kuhusu Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, lakini ameshangazwa na maudhui na lugha iliyotumiwa na
Ikulu dhidi yake.
Warioba alisema tume yake ilikuwa
haijamaliza kazi wakati inakabidhi ripoti kwa Rais Kikwete kwani iliendelea na
kazi ya kuandaa Randama ya Rasimu, Bango Kitita la Rasimu na maelezo aliyoyatoa
kwenye Bunge Maalumu.
Alisema serikali ilijua tume ilikuwa
inafanya kazi hiyo na nyaraka hizo zilikabidhiwa bungeni siku ya kuwasilisha
rasimu.
Kuhusu madai kwamba wajumbe wa tume
hiyo wanadai walipwe sh milioni 200 kila mmoja, Jaji Warioba alisema hakuna
mjumbe aliyetoa dai kama hilo na serikali inajua.
Alisema alichozungumza ni muda wa
kuandaa makabidhiano na kuandaa safari ya wajumbe kurudi makwao kwani
aliwasilisha rasimu Machi 18, 2014, tume ilivunjwa Machi 19, 2014 wakati
wajumbe wako Dodoma.
“Pamoja na lugha ya kejeli
iliyotumiwa na serikali na kuniita mnafiki, busara ya kawaida ingeonyesha
umuhimu wa serikali kujipa muda wa kufanya maandalizi ya kuwarudisha wajumbe
nyumbani. Hata kama sheria ilitaja muda
wa kuvunja tume, bado ilikuwa ni wajibu serikali kufanya mipango ya safari ya
wajumbe baada ya kumaliza kazi. Sheria haikuizuia serikali kufanya hilo. Huo ni
wajibu wa serikali na utaratibu wa kawaida unaotumiwa na serikali kwa tume zote
inazoziunda,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment