HALI ya hewa baina ya mshambuliaji wa
Yanga, Emmanuel Okwi na uongozi wa timu hiyo, si nzuri na Mganda huyo ameamua
kugomea mazoezi akishinikiza kumaliziwa chake.
Picha lilianza hivi; Okwi alisajiliwa
na Yanga kwa usajili uliogharimu Dola 100,000 (Sh162 milioni) katika usajili wa
dirisha dogo, lakini uongozi wa timu hiyo haukumpatia fedha zote na walikuwa na
makubaliano maalum. Walimkatia dola 60,000 tu kwa kuanzia.
Okwi ameshaichezea Yanga mechi sita
za Ligi Kuu Bara na juzi Jumanne aligoma kufanya mazoezi yaliyofanyika katika
viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam akitaka kulipwa fedha
zake zilizosalia, jambo ambalo limewakera mabosi wa Yanga ingawa wanafanya siri
kubwa.
Katika mazoezi hayo, Okwi alifika
mapema na kukaa nje jambo ambalo si kawaida huku wenzake wakijifua chini ya
kocha, Hans Pluijm, ambaye jana Jumatano aliliambia Mwanaspoti kuwa sababu za
Okwi kushindwa kufanya mazoezi zipo nje ya uwezo wake.
“Siwezi kuzungumzia hilo tatizo la
kutofanya mazoezi kwa Okwi, nadhani lipo juu ya uwezo wangu, lakini ninachoweza
kusema ni kwamba tangu nilipofika Yanga nimekuwa na uhusiano mzuri na Okwi,
nafikiri hicho ndicho ninachoweza kukwambia,” alisisitiza kocha huyo.
Lakini Okwi alipotakiwa kutoa
ufafanuzi hakuzungumza lolote mazoezini hapo.
Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu,
alikiri Okwi kutofanya mazoezi, lakini akadai kwamba anahitaji muda kukaa na
mchezaji huyo kujua tatizo ila akasisitiza hawadai.
“Nimepata taarifa kwamba Okwi
hakufanya mazoezi, lakini nitaongea naye kujua tatizo lake. Ila si kweli kwamba
anadai fedha zozote,” alisema Njovu.
Mmoja wa viongozi wazito na mwenye
ushawishi mkubwa ndani ya Yanga, alizungumza na Mwanaspoti jana Jumatano na
kuonekana kukerwa na tukio hilo, lakini akakiri kwamba mchezaji huyo anawadai.
Bosi huyo aliyeonekana kuwa mkali,
alisema mpaka sasa Okwi ameshafunga mabao mawili pekee katika mechi za ligi
alizocheza ambapo ukiacha hata wachezaji wenzake kwa ujumla wameshindwa kucheza
kwa kujituma wakielekeza akili zao katika kupata fedha pekee.
“Hapa Yanga hakuna tatizo la fedha
lakini tunawezaje kutoa fedha wakati wenyewe hawajitumi? Fedha tunazowapa
hazilingani na mchango wao kwenye timu, imefikia hatua wanakubali kufungwa na
wachezaji 10 wa Mgambo ambao mishahara yao ni sawa na posho tu kwa Yanga,”
alisema bosi huyo kwa hasira.
“Hivi tumpe dola 40,000 Okwi kwa kipi
cha kutufariji alichotufanyia? Nataka nikwambie kama Okwi anataka fedha zake
jibu ni rahisi sana, aonyeshe kwenye mechi aone kama atazikosa tena zitakuja
bila ya kuomba na hilo si kwa Okwi pekee, bali ni kwa wachezaji wote, fedha
tunazo lakini hawatutendei haki.
“Tunatumia fedha nyingi kuwalipa
mishahara mikubwa, lakini angalia mchezo wetu uliopita wanakubali kufungwa
kirahisi na hata haiwaumi, tena kwa timu ambayo wanalipwa malipo madogo na tatu
wakiwa pungufu, sasa wanakuja wachezaji hao hao eti wanadai fedha, hatuendi
hivyo.”
Alidai kwamba Okwi hajafanya kile
walichokitegemea wakati wanamsajili na kwamba anapaswa kuwa muungwana pia kwa
vile uongozi uligharamia fedha nyingi kukamilisha usajili wake kuliko
walivyotarajia.
Chanzo: Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment