Na Hudugu Ng'amilo
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia
(Chadema), Dk. Willibroad Slaa, amewataka Watanzania kutambua kuwa hakuna chama
cha upinzani ambacho kina lengo la kuvunja Muungano bali yanayoelezwa ni njama
ya kudhoofisha msimamo wa kuwapo kwa serikali tatu.
Alitoa kauli hiyo jana katika viwanja
vya Tangamano, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa jiji la Tanga, baada ya
kuongoza timu ya viongozi wa juu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mjini
hapa na kuwataka wakazi wa jiji hilo kukataa hadaa zinazofanywa kwa lengo la
kukanyaga rasimu ya katiba, ambayo waliitolea maoni yao.
Alisema kilichofanywa na Rais Jakaya
Kikwete, wakati akilihutubia Bunge Maalumu la Katiba kuiponda rasimu ya katiba
ni kumdhalilisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba, ambaye ni kiongozi mwenye heshima Tanzania na nje ya nchi na
kwamba, Ukawa itazunguka nchini kote kumtetea.
Dk. Slaa ambaye ni Mwenyekiti wa
Ukawa nje ya Bunge hilo, alisema Rais Kikwete anawahadaa wananchi anaposema
wanaotaka serikali tatu wana lengo la kuvunja Muungano na kusisitiza kuwa
hakuna chama chochote cha upinzania, ambacho kinataka Muungano uvunjike.
"Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na
wananchi wote wa Tanzania Bara na hata visiwani, hakuna anayetaka Muungano
uvunjike, bali kinachofanywa na CCM ni kuwachonganisha kwa wananchi ili
waonekane ni maadui wa Muungano," alisema Dk. Slaa.
Alisema inasikitisha kuona kuwa kuna
baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar ndani ya Bunge hilo wakidanganywa kuahidiwa
kupewa fedha za kuwasomesha ili waunge mkono msimamo wa kupiga kura ya serikali
mbili jambo ambalo ni kinyume cha malengo ya uwakilishi wao kwa Watanzania.
"Chini ya Umoja wao wa Ukawa
wanachofanya ni kutetea maoni ya wananchi yaliyotolewa kwenye Tume ya Katiba
kwa kuwa Tanzania ni nchi ya wote na hakuna, ambaye akifa atazikwa nje ya nchi
hii. Hivyo, ni lazima kutetea maslahi ya wananchi," alisema Dk. Slaa.
KAIMU KATIBU MKUU WA CUF ANENA
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF), Shaweji Mketo, alisema Tume ya Maridhiano ya Zanzibar
inayoundwa na viongozi kutoka CCM na CUF ikiongozwa na Nassoro Moyo, imetoa
tamko la kumtaka Rais asidhani Watanzania ni watu wa kuhadaiwa, bali watatetea
serikali tatu kwa kuwa ina lengo la kuimarisha Muungano uliopo.
CHANZO: NIPASHE.
No comments:
Post a Comment