Watalaamu wa mambo ya hali ya hewa
wanasema athari za mabadiliko ya tabia nchi tayari zinatokea katika mabara yote
na baharini, na ulimwengu haujajiandaa kupambana na hatari inayosababishwa na
mabadiliko hayo.
Jopo la Kimataifa kuhusu Mabadiliko
ya Tabia Nchi – IPCC linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa limekamilisha ripoti
yake kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa maisha ya binaadamu na mfumo
asilia wa mazingira ya dunia, pamoja na mbinu zinazoweza kutumiwa kukabiliana
na hali hiyo. Mkutano wa wataalamu hao ulifanyika wiki iliyopita katika mji wa
Yokohama nchini Japan.
Ripoti hiyo inasema athari za majanga
ya karibuni yanayohusiana na hali ya hewa, kama vile ongezeko la joto
kali,ukame, mafuriko, vimbunga na moto wa misituni zinadhihirisha hatari kubwa
iliyopo kwa binaadamu na mifumo ya asili.
Vicente Barros, mwenyekiti msaidizi
kwa jopo hilo linalowajumuisha mamia ya wanasayansi na wawakilishi wa serikali,
amesema ulimwengu unaishi katika enzi ya mabadiliko ya tabia nchi
yanayosababishwa na binaadamu.
Mabadiliko ya tabia nchi ni kitisho
kinachoongezeka kwa usalama wa binadamu kwa sababu yanasababisha uharibifu kwa
makaazi na mali, yanavuruga upatikanaji wa chakula na maji na kushurutisha watu
kuzihama sehemu zao za asili.
Mwenyekiti wa jopo hilo la IPCC
Rajendra Pachauri amewaambia waandishi wa habari leo kuwa hakuna yeyote duniani
ambaye atanusurika kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Hatari ya
mabadiliko ya tabia nchi yatakuwa ya kiwango cha “juu hadi kupindukia” iwapo
joto litaongezeka zaidi ya nyuzijoto nne juu ya viwango vya kabla ya ustawi wa
kiviwanda, ambako ulimwengu sasa unaelekea.
Pachauri anasema kitu muhimu
walichoafikiana ni kuhusu umuhimu wa kuwa na mbinu za kuweza kukabiliana na
hali hiyo kwa sababu ndiyo njia pekee ambayo ulimwengu unaweza kupunguza hatari
ya mabadiliko ya tabia nchi. Ripoti hiyo inasema wazi kuwa bado upo muda wa
kuchukua hatua. Samantha Smith kutoka Shirika la mfuko wa kutunza mazingira ya
dunia, World Wide Fund for Nature Campaign hata hivyo anasema bila hatua
madhubuti na za haraka, dunia inakabiliwa na kitisho cha kufika mahali ambako
itakuwa haina la kufanya kuhusu hali hii ya mabadiliko ya tabia nchi.
Mnamo mwezi Septemba mwaka jana, jopo
la IPCC lilionya kuwa binaadamu ndio kimsingi wanaosababisha ongezeko la joto
duniani, ambalo limesababisha kuongezeka kwa kina cha bahari kwa kiwango
ambacho hakikufikiriwa hapo awali, na kuyeyuka barafu kwa kasi.
Ripoti ya tatu itakayoangazia mbinu
za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi itazinduliwa mwezi wa Aprili mjini
Berlin. Mkutano wa kilele mjini Paris mwaka wa 2015 utaangazia kuundwa kwa
mkataba mpya wa kimataifa kuhusu hali ya hewa, ili kuchukua nafasi ya muafaka
wa Kyoto wa mwaka wa 1997, ambao awamu ya kwanza ilikamilika mwishoni mwa mwaka
wa 2012.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Daniel Gakuba
D.E
No comments:
Post a Comment