NA MWANAHIBA RICHARD
EMMANUEL Okwi ndiye mchezaji pekee
anayewafunika wachezaji wote wanaocheza Ligi Kuu Bara kwa kuwa na mshahara
mnono sawa na wachezaji wa klabu maarufu ya Afrika ya TP Mazembe. Mshahara
anaolipwa straika huyo unatosha kumlipa Haruna Niyonzima na Mrisho Ngassa kwa
mwezi.
Achana na hao njoo Simba, ukichukua
fungu la dola 4,000 sawa na Sh 6.4 milioni za Kitanzania anazolipwa fowadi huyo
zinatosha kulipa mishahara ya wachezaji watatu muhimu wa Msimbazi, Amissi
Tambwe, Joseph Owino na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Kiasi hicho anacholipwa Okwi ni zaidi
ya fedha aliyokuwa akilipwa pia mshambuliaji wa zamani wa Simba, Felix Sunzu
ambaye alikuwa analipwa Sh 5 milioni kwa wakati huo akiwa ndiye mchezaji pekee
ghali kuliko wote.
Mshambuliaji huyo wa Yanga raia wa
Uganda alisajiliwa na mabingwa hao wa soka nchini wakati wa usajili wa dirisha
dogo akitokea SC Villa ya Uganda baada ya kutofautiana na timu yake ya Etoile
du Sahel ya Tunisia alikouzwa na Simba msimu uliopita.
Usajili wa Okwi ulileta utata mkubwa
ambao ulisababisha akose baadhi ya mechi mpaka ulipotolewa ufafanuzi kutoka
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa kile kilichokuwa kinadaiwa kuwa ana
mkataba na Etoile du Sahel.
Hivi sasa Okwi ameonekana kuanza
usumbufu ndani ya klabu hiyo baada ya kudaiwa kuondoka kambini bila ya kutoa
sababu za kufanya hivyo huku akiwa ameifungia Yanga mabao matatu pekee tangu
ajiunge nayo.
Mbali na mchezaji huyo wachezaji
wengine wanaofaidi mishahara minono kutoka Azam FC ni Kipre Tchetche, Kipre
Balou, John Bocco, Agrey Morris, Briany Omony na Haruna Niyonzima wa Yanga
ambao wanapata Sh 4 milioni.
Beki Mbuyu Twite wa Yanga yeye
anapata Sh 3.6 milioni huku beki wa Simba Joseph Owino ndiye anayeingiza fedha
ndefu ndani ya klabu hiyo kwa kupokea mshahara wa dolla 2,000 sawa na Sh 3.2
milioni.
Yanga imeonekana kuwafunika wachezaji
wa Simba kwani wachezaji wake wengi wanapata mishahara ya kuanzia Sh. milioni
moja kupanda juu huku wachezaji wa Simba wengi wao wakianzia shilingi milioni
moja kushuka chini.
Mwanaspoti limebaini kuwa wachezaji
wazawa hakuna anayelipwa mshahara wake zaidi ya Sh 5 milioni walio wengi
mishahara yao haizidi Sh 1 milioni ingawaje wachache wamefikisha Sh 4 milioni.
Chanzo: Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment