Saturday, April 5, 2014

Kapombe: Bado nipo nipo kwanza

ALIYEKUWA beki wa timu ya Simba, Shomari Kapombe, amesema mipango yake ya kujiunga na Azam imekwama, akisubiri amalizane kwanza na AS Cannes ya Ufaransa.

Kapombe ameamua kurejea nchini na kujiunga na Azam kutokana na timu hiyo kutomlipa stahiki zake kwa kipindi alichoitumikia akitokea klabu ya Simba iliyokuwa imemtoa bure.

Akizungumza na Tanzania Daima juzi, wakati akijifua katika Uwanja wa TCC Chang’ombe, Kapombe alisema kwa sasa anajifanyia mazoezi tu bila ya kujua nini hatma yake.

Siku hiyo Kapombe alikuwa akifanya mazoezi jioni na vijana wenzake kwa lengo la kulinda kiwango chake kama ambavyo amekuwa akijifua na timu ya Azam FC.

Alisema hadi sasa mbali ya kufanya mazoezi Azam FC, hana mkataba na timu yoyote kwa hapa nchini.

“Nipo tu nyumbani, ndiyo maana unaniona hapa, japo nimekuwa pia nikifanya mazoezi na Azam FC, kwa saababu sijamalizana na timu ile ya Ufaransa,” alisema Kapombe.

Wakati Kapombe akisema hayo, mmoja wa viongozi wa Azam FC ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alidokeza kuwa wao wanamuhitaji nyota huyo, lakini kikwazo ni sheria.


“Kapombe anafanya mazoezi tu kwetu, bado hatujasaini naye mkataba, tunatambua bado ni mchezaji wa Simba na ana mkataba utakaomalizika mwakani,” alisema kiongozi huyo.

No comments: