Ni saini ya Msekwa, lakini vijana wa chamber kwa AG
waliongeza neno “Msekwa” kwa kompyuta. Ni mtu asiyejua thamani na uhalisia wa
saini ni kubaki ilivyo hata kama kwa miaka 100 hata mtu aje kuisoma kwa
darubini,”.PICHA|MAKTABA
Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge la
Katiba, Samuel Sitta amekiri “kuchezewa” kwa saini ya hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere na sehemu ya saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la
Tanganyika, Pius Msekwa zilizopo kwenye hati ya sheria ya kuridhia Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
Akizungumza na gazeti hili jana,
Sitta alisema ni kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22 ya 1964,
iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa.
Alisema katika saini ya Nyerere
kumeongezwa herufi “us” kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa
kumeandikwa neno “Msekwa” kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema
walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini
walifanya makosa.
“Wale vijana walipoona document
(nyaraka) haisomeki waliongeza “us” mwisho kwa kompyuta kwenye saini ya
Nyerere, ila walifanya makosa maana bora kitu kionekane kufifia hivyo hivyo
lakini kibaki na maana yake,” alisema.
Hata hivyo, Sitta alisema kwa
waliofanya kazi na hayati Baba wa Taifa wanatambua saini iliyopo kwenye hati ya
sheria hiyo ipo sawa ukiondoa makosa ya kuwekwa herufi hizo.
Kuhusu saini ya Msekwa, alisema pia
kulifanyika makosa katika sehemu ya saini hiyo, kuandikwa kwa kompyuta
“Msekwa”.
“Ni saini ya Msekwa, lakini vijana wa
chamber kwa AG waliongeza neno “Msekwa” kwa kompyuta. Ni mtu asiyejua thamani
na uhalisia wa saini ni kubaki ilivyo hata kama kwa miaka 100 hata mtu aje
kuisoma kwa darubini,” alisema.
Hata hivyo, alisema maudhui ya hati
ya sheria hiyo, iliyosainiwa rasmi Aprili 25, 1964 ni sahihi kama ambavyo
walikubaliana waasisi wa Muungano, Nyerere na Karume.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alisema kwamba
hafahamu kama ofisi yake inahusika na kuchezewa kwa saini hizo, tofauti na
madai ya Sitta.
Sheria iliyopitishwa Z’bar
Sitta alisema ili kuondoa utata,
ameagiza kupatiwa hati ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume
(Presidential Decree) aliyotoa kusaini makubaliano kwani wakati huo, hakukuwa
na Bunge.
“Karume alitumia Baraza la Mapinduzi
akatumia amri ya Rais akasaini. Tunatarajia kuipata hiyo, sasa tutakuwa
tumepata nyaraka za Bara na Zanzibar,” alisema Sitta.
Hata hivyo, alisema kisheria
kilichopitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Zanzibar ni
yaleyale yaliyopo kwenye mkataba wa Muungano.
“Unajua kuhoji sasa mambo haya ni
kupoteza muda, ni kama kuulizana na mke wako cheti cha ndoa baada ya kuishi
pamoja miaka mingi, jana (juzi) nilikuwa nawaomba wajumbe kujua tunachotakiwa
ni kutengeneza Katiba ambayo, inajibu matatizo yetu,” alisema Sitta.
Hati ipo UN
Akizungumzia hati ya Muungano,
alisema kuwa ni kweli kupata hati hiyo kuna umuhimu, lakini mambo yote muhimu
yanayohusu Muungano yamewekwa katika sheria hizo mbili zilizoridhiwa na pande
zote.
Alisema kwa muda walionao wajumbe wa
bunge hilo, lazima wautumie vizuri kuliko kwenda hadi Umoja wa Mataifa (UN) kwa
ajili ya kuchukua hati hizo.
“Bunge la Tanganyika lililetewa
muswada unaoonyesha mambo waliyokubaliana Nyerere na Karume, na Baraza la
Mapinduzi likapelekewa hivyohivyo,” alisema na kuongeza: “Sasa ubishi wa hiyo
hati ya kwanza kabisa ambayo wengi wanasema ipo Umoja wa Mataifa ilikopelekwa
kuthibitisha nchi imebadili jina, hiyo ni ya nini? Ni ubishi wa bure tu.”
Sitta alisema kisheria
kilichopitishwa na Bunge kinatambua yaliyomo katika hati hiyo na hali ndivyo
ilivyo pia kwa Baraza la Mapinduzi.
Kwa takriban siku tatu, kamati kadhaa
za Bunge zinazojadili Rasimu ya Katiba, zimekuwa na mgongano juu ya hati za
muungano na uhalali wa saini za Nyerere na Msekwa.
Kanuni kutenguliwa
Alisema pia, Bunge la Katiba itabidi
kubadili kanuni na ratiba yake katika kikao cha leo.
Sitta alisema kwa utaratibu
uliokuwapo, leo kamati ndio zilipaswa kuanza kuwasilisha taarifa zake, lakini
imeonekana haiwezekani.
“Ni kamati moja tu Namba 5, kati ya
kamati 12 ndio ambayo ilikuwa imekamilisha kujadili na kupiga kura walau Sura
ya Kwanza tu ya Rasimu, hivyo kwa hali ilivyo lazima tupitie upya kanuni zetu,”
alisema Sitta.
“Tuliweka siku moja kwa ajili ya uandishi
na kuandika ripoti, lakini haiwezekani, imebidi tuongeze siku nyingine moja ili
wajumbe waweze kuipitia tena taarifa ya kamati ambayo itasomwa bungeni,
vinginevyo itasababisha ubishi,” alisema.
Alisema marekebisho yote ya kanuni,
yatafanyika leo bungeni na baadaye ndio itatolewa Ratiba ya Bunge katika siku
zijazo.
Hata hivyo, alisema katika ratiba
hiyo, kutakuwa na mapumziko ya Bunge Aprili 7, kupisha maadhimisho ya Siku ya
Karume, baadaye Ijumaa Kuu, Sherehe za Pasaka na pia maadhimisho ya Sokoine na
Muungano.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment