Homa ya Ebola yatishia kuenea Afrika Magharibi
Nchi kadhaa za Afrika magharibi
zimepania kuipiga vita homa hatari ya Ebola iliyoangamiza maisha ya zaidi ya
watu 80 nchini Guinea,siku moja tu baada ya homa hiyo kuripotiwa Mali,baada ya
Liberia na Sierra Leone.
Mali nchi inayopakana na Guine
imesema jana usiku,kadhia tatu za homa ya Ebola zimegunduliwa nchini humo na
walioambukizwa kuwekwa karantini.
"Watu hao watatu hali yao hivi
sasa ni nzuri,hakuna tena dalili ya kuvuja damu-mojawapo ya ishara za homa ya
Ebola" amesema waziri wa afya na usafi wa jamii Ousmane Koné.Kwa mujibu wa
Dr. Omar Sangaré,wa idara ya afya watu hao wote watatu ni raia wa Mali
waliokuwa wakifanya kazi katika eneo la mpakani kati ya Mali na Guine.
Serikali ya Mali imewaonya raia
wasifike katika maeneo ya maambukizi.
Nchi iliyoathirika zaidi ni Guine ya
Conacry ambako homa hiyo inayosababisha watu kuvuja damu imeshaangamiza maisha
ya watu 86 toka jumla ya watu 137 walioambukizwa tangu january mwaka huu-wengi
wao ni wa kutoka eneo la kusini-kwa mujibu wa ripoti ya serikali.
Ishara za matumaini mema
Kadhia 45 kati ya hizo
zimethibitishwa kuwa ni za homa ya Ebola,maradhi hatari yanayoambukiza na
ambayo hadi wakati huu hayana tiba wala chanjo."Lakini wagonjwa wawili
waliokuwa wamewekwa karantini wamethibitishwa wamepona mjini
Conacry"-serikali imesema.
Matumaini finyu yamechomoza katika
wakati ambapo shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka ,linaloendesha shughuli
zake nchini Guine linazungumzia juu ya "mambukizi yasiokuwa na
mfano".
Liberia inazungumzia kisa cha msasi
mmoja ambae hakuwa na maingiliano na mtu yeyote aliyeambukizwa homa ya Ebola na
wala hakuwahi kwenda Guinea.Liberia imewataka wakaazi wake wasinunue nyama
yoyote inayotokea vijijini.Kadhia 14 za homa ya Ebola zimeripotiwa nchini
Liberia-sabaa ya wagonjwa hao wameshakufa.
Nchi zinazopakana na Guinea zimetuma
wataalam wa afya katika maeneo ya mpakani.Katika nchi ambako maradhi hayo ya
kuambukiza yameshaingia maafisa wa serikali wanawapa mwongozo wa kuishi
wananchi ili kuepukana na balaa la kuenea maradhi hayo.
Wataalam wa kimataifa wanawajibika
Wataalamu tangu wa ndani mpaka wa nje
ya bara la Afrika wameingia mbioni kupambana na maradhi hayo
hatari."Ugonjwa huu wa kuambukiza ni hatari kwasababu bado haujadhibitiwa
na walioambukizwa wameenea sehemu tofauti" amesema tabibu mmoja wa
kifaransa Sylvain Baize anaeongoza kituo cha utafiti wa homa zinazosababisha
watu kuvuja damu mjini Lyon kusini mwa Ufaransa.
"Nimeingiwa na wasi wasi
kwasababu haijulikani bado viruusi vya maradhi ya Ebola vimefika vipi katika
eneo la Afrika magharibi na hakuna ajuaye watu wangapi hasa wameambukizwa"
amesema kwa upande wake Thomas Geisbert,ambae ni mtaalam wa homa zinazopelekea
watu kuvuja damu ,anaefanya kazi na kituo cha utafiti cha chuo kikuu cha Texas
nchini Marekani.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir /AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
No comments:
Post a Comment