UCHAGUZI mdogo wa ubunge Chalinze,
Bagamoyo, mkoani Pwani unaofanyika leo ambapo jumla ya vituo 288 vya kupigia
kura vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 vitatumika tena.
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi
huo jana, msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Bagamoyo, Samuel Salianga, alisema maandalizi yamekamilika kwa
asilimia 95 na vifaa muhimu vimesambazwa kwenye vituo hivyo.
Alivitaja vyama vitano vinavyoshiriki
uchaguzi huo kuwa ni CCM, CHADEMA, CUF, NRA na AFP huku akibainisha idadi ya
wapiga kura kuwa ni 92,939.
Kwa upande mwingine Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa Chalinze
kuhakikisha vinawatumia mawakala wanaotoka eneo la vituo ili wawatambue wapiga
kura wa eneo hilo.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti
wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema sheria haikatazi vyama hivyo kuteua
mawakala kutoka majimbo mengine ya uchaguzi lakini ni vema kuwateua wale
wanaotoka eneo lenye wapiga kura wanaowafahamu.
Licha ya kuwepo kwa idadi hiyo ya
waliojiandikisha katika daftari la kupiga kura lakini kuna wasiwasi wa wapiga
kura kutofikia idadi hiyo kutokana na miundombinu ya baadhi ya maeneo
kuharibiwa na mvua zinazonyesha mkoani hapa.
Kufanyika kwa uchaguzi huo kunatokana
na kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Said Bwanamdogo, ambaye alifariki dunia
Januari 22, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment