Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 24 leo (Aprili 5 mwaka huu)
kwa mechi mbili ambapo Kagera Sugar itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa
Kaitaba mjini Bukoba.
Mechi nyingine itakuwa kati ya Mbeya
City ambayo itakuwa mgeni wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Azam Complex
uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam. Ashanti United inayofundishwa na Abdallah
Kibaden ipo katika mkakati wa kukwepa kushuka daraja.
Kesho (Aprili 6 mwaka huu) kutakuwa
na mechi kati ya Coastal na Mgambo Shooting Stars (Mkwakwani, Tanga), Oljoro
JKT na Tanzania Prisons (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Rhino Rangers na
Mtibwa Sugar (Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na Yanga dhidi ya JKT Ruvu (Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam).
Raundi hiyo itakamilika Aprili 9
mwaka huu kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Azam itakayochezwa Uwanja wa
Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
NI MWADUI AU STAND UNITED VPL MSIMU
UJAO
Ni ipi kati ya timu za Mwadui na
Stand United, zote za Shinyanga itakayocheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu
ujao itajulikana kesho (Aprili 5 mwaka huu) baada ya kundi C kuhitimisha mechi
za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu.
Mwadui yenye pointi 28 ndiyo
inayoongoza, na itacheza na Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini
Dodoma. Nayo Stand United yenye pointi 26 itaikaribisha Toto Africans kwenye
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Mechi nyingine zitakuwa kati ya Pamba
na Kanembwa JKT itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Polisi
Mara na Polisi Tabora zitakwaruzana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini
Musoma.
Timu ambazo tayari zimepanda daraja
kutoka FDL kucheza VPL msimu ujao ni Ndanda SC kutoka kundi A na Polisi
Morogoro ya kundi B.
21 ZA KUCHEZA RCL ZAJULIKANA
Timu 21 kati ya 27 zitakazocheza Ligi
ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kutafuta tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) msimu ujao tayari zimejulikana.
Timu hizo ni Abajalo SC (Dar es
Salaam), AFC (Arusha), African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Geita
Veterans (Geita), JKT Mafinga (Iringa), JKT Rwamukoma (Mara), Kariakoo SC
(Lindi), Kiluvya United (Pwani), Milambo SC (Tabora) na Mshikamano FC (Dar es
Salaam).
Nyingine ni Mvuvumwa FC (Kigoma),
Navy SC (Dar es Salaam), Njombe Mji (Njombe), Pachoto Shooting Stars (Mtwara),
Panone FC (Kilimanjaro), Singida United (Singida), Tanzanite (Manyara), Town
Small Boys (Ruvuma), Ujenzi FC (Rukwa) na Volcano (Morogoro).
WATANO WAFANYA MTIHANI WA UWAKALA WA
WACHEZAJI
Watanzania watano wamefanya mtihani
wa uwakala wa wachezaji wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
ambao ulifanyika jana (Aprili 3 mwaka huu) duniani kote.
Watahiniwa katika mtihani huo ambao
ulikuwa na maswali kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
walikuwa Godlisten Anderson, Jesse Koka, Lutfi Binkleb, Rwechungura Mutahaba na
Silla Yalonde.
No comments:
Post a Comment