Dodoma.Uamuzi wa kupiga kura umepita
kwa makubaliano ya kupiga kura mseto utakaoruhusu mjumbe kupiga kura kwa aina
anayoitaka; kupiga kura ya wazi au ya siri.
Uamuzi huo ni wa kihistoria kwa kuwa haujawahi kutumika
kokote duniani. Baadhi ya wajumbe wameonyesha kufurahishwa nao na wengine
kuupinga.
Kwa sehemu kubwa kura ya wazi ilikuwa
ni msimamo wa wajumbe wanaotoka kundi la wanasiasa hasa wanaotoka Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, miongoni mwa wajumbe hao
wa CCM, wapo ambao walipinga tangu mwanzo suala hilo, wakisema mfumo huo
unawakandamiza na hauna tija kwa taifa.
Miongoni mwa wajumbe ni Alli Keissy,
Kangi Lugola, Deo Filikunjombe, Esther Bulaya, Juma Kapuya na James Lembeli.
Hatua ya wajumbe hao kupingana
hadharani na matakwa ya chama chao, inaweza kuchukuliwa kama ujasiri wa
kipekee, kwani wanafanya hivyo, wakijua ndani ya chama chao baadhi ya wajumbe
wameadhibiwa kutokana na kutofautiana kimtazamo na chama.
Kura ya mseto ilipitishwa kwa kila
mjumbe kuitwa jina lake na kueleza kukubali au kukataa. Hapo ndipo misimamo ya
wengi ilionekana.
Wabunge Kangi Lugola na Deo
Filikunjombe walionyesha misimamo yao hadharani baada ya kupingana na matakwa
hayo ya chama kwa kupinga kura ya wazi. Wakati kura hiyo inapigwa, wajumbe
James Lembeli na Profesa Juma Kapuya hawakuwapo ukumbini.
Nikiwa bungeni nimepata fursa ya
kuzungumza na Lembeli nikitaka kujua msimamo wake ulikuwa upi kama angekuwapo
bungeni siku hiyo ya kupiga kura na yafuatayo ni mahojiano yetu:
Swali: Mheshimiwa Lembeli, pole na
shughuli za hapa bungeni wakati wa kupitisha kanuni za 38 na 39, sikubahatika
kusikia sauti yako mle ukumbini hivi uliunga mkono kura ipi?
Jibu: Asante, sijapoa maana kazi ndio
imeanza, lakini na ninyi mmeanza uchokozi…(kicheko). Kweli haukunisikia kwa
sababu sikuwepo.
Swali: Kama ungekuwepo kura yako
ilikuwa katika mrengo upi mheshimiwa?
Jibu: Hata siku moja siwezi kula
matapishi yangu. Nimekuwa nikisimamia ukweli na ukweli ndio utakaoniweka huru
siku zote za maisha yangu. Mimi nataka kura ya siri na ndiyo ambayo ningeitaka
siku hiyo bila hofu.
Swali: Kura ya siri inapingwa na
chama chako, ni vipi uendelee kuing’ang’ania kwani huogopi kushughulikiwa
kisiasa?
Jibu: Vijana msipende kutishwa na
jambo la kushughulikiwa. Anayeshughulika na mwanadamu ni Mungu pekee si mtu
mwingine. Hapa tunafanya kazi za kujifurahisha tu jamani.
Ukisikia mtu anasema
atakushughulikia, jiulize mara nyingi anashughulika na wewe kwa namna gani au
juu ya jambo gani, je ni kwa jambo la ukweli au lile la kinafiki.
Swali: Kwa nini unasema hivyo, una
maana chama chako hakina uwezo wa kufanya hivyo?
Jibu: Kinao, lakini najiuliza hivi
mtu anashughulika nami kwa jambo gani? Je, kwa matakwa ya wananchi au kwa lipi
hasa? Mimi nakipenda sana chama changu kuliko wengi wanavyofikiri lakini
nasimamia ukweli ambao chama pia kinautaka.
Swali: Kwa mtazamo wa wengi ni kwamba
Tanganyika uliyokuwa ukiishabikia sasa ndiyo imezikwa rasmi kutokana na wingi
wa kura za wanaopinga rasimu hii, wewe unasemaje?
Jibu: Haiwezi kufa ili mradi watu
wanataka ife. Subirini mle ndani mtatuona, nitaanzia kwenye kamati yangu hadi tutakaporudi
humu ndani. Nasema historia huwa haikarabatiwi.
Swali: Sasa umeshindwa kuonyesha
msimamo wako kwa wapiga kura ambao unasema ndio watu wa kuwaheshimu zaidi. Je,
unawaahidi nini katika mchakato huu?
Jibu:Nasisitiza kuwa msimamo wangu
haupingani na wapiga kura walionituma bungeni na nikipingana kwa kupiga kura ya
wazi hapo watakaponihukumu, lakini nikiwa pamoja na mawazo yao lazima
watanitendea haki.
Swali: Lakini umekuwa na mawazo
kinzani wakati wote kuhusu Rasimu ya Katiba, nguvu ya aina hii unaipata wapi?
Jibu: Siyo mawazo kinzani. Naishi kwa
kujifunza na kuangalia watangulizi wetu walisema nini, mfano Mwalimu Nyerere
aliwahi kusema Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM
wanaweza kutafuta kwingine. Kwa hiyo mabadiliko ni lazima yaanzie kwetu sisi wa
chama tawala.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment