Tuesday, April 1, 2014

MICHEZONI: Yanga yavunja rekodi kali ya Simba Bongo

            Yanga ilikaribia kuivunja rekodi hiyo msimu uliopita, lakini iliishia kuifikia tu kwa kufunga mabao 47 na iliruhusu mabao 14 

MABAO 50 yaliyowekwa kibindoni na Yanga mpaka sasa katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara yametosha kuvunja rekodi ya kufunga mabao mengi iliyowekwa na Simba msimu wa mwaka 2011/2012.

Katika msimu huo unaokumbukwa zaidi kwa Simba kuifunga Yanga mabao 5-0 kwenye mechi ya mwisho ya ligi, Wekundu wa Msimbazi hao walifunga mabao 47 na waliruhusu mabao 12 tu kutikisa nyavu  zao. Msimu huo Yanga ilifunga mabao 41 na nyavu zake zilitikiswa mara 30.

Yanga ilikaribia kuivunja rekodi hiyo msimu uliopita, lakini iliishia kuifikia tu kwa kufunga mabao 47 na iliruhusu mabao 14. Msimu huo uliopita, Simba iliporomoka na kufunga mabao 38 tu na ikaruhusu mabao 25 kuingia kwenye nyavu zake.

Hata hivyo, msimu huu Yanga imeonyesha uwezo mkubwa na kabla ya mechi yake ya jana Jumapili dhidi ya Mgambo JKT ilishakuwa na mabao 50 na kuruhusu mabao 12 tu kuingia kwenye nyavu na bado ina mechi nne mkononi.

Simba nayo kabla ya mechi yake ya jana Jumapili dhidi ya Azam FC ilikuwa imefunga mabao 38 na kufungwa 22. Sasa imebakiza mechi tatu.


Azam haiko nyuma kwenye upachikaji mabao kwani katika misimu mitatu mfululizo imeweza kuweka kibindoni zaidi ya mabao 40. Msimu uliopita ilifunga mabao 47 wakati msimu huu kabla ya jana Jumapili kucheza na Simba ilikuwa na mabao 43 na imesaliwa na mechi nne. Chanzo: Mwanaspoti

No comments: