Dodoma. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema waliokuwa wajumbe wa tume
hiyo hawajawahi kudai malipo ya pensheni ya Sh200 milioni kama inavyodaiwa.
“Wajumbe wa Tume hawajatoa madai ya
kulipwa shilingi milioni mia mbili. Hakuna mjumbe yeyote aliyetoa dai kama hilo
na Serikali inajua,” alisema
Jaji Warioba katika taarifa yake kwa
vyombo vya habari jana, aliyoitoa kupitia Nyalali, Warioba and Mahalu Law
Advocates ali ongeza:
“Nimeona taarifa iliyotolewa na
Serikali kuhusu Tume ya Mabadiliko, nimeshangazwa na maudhui na lugha
iliyotumika,” alisema Warioba akirejea taarifa iliyotolewa na Ikulu juzi
ikieleza jinsi tume hiyo ilivyohitimisha kazi zake.
Wiki hii Jaji Warioba alikaririwa
akilalamika jinsi yeye na makamishna wake walivyoondolewa ofisini na
kunyang’anywa magari kwa haraka bila kusubiri siku waliyopanga kufanya
makabidhiano, lakini Ikulu ilimjibu kwamba shughuli za Tume hiyo zilikoma siku
ambayo Tume ilivunjwa.
Katika taarifa yake ya jana, Jaji
Warioba alisema aliwasilisha Rasimu ya Katiba Machi 18 mwaka huu na Tume
ilivunjwa Machi 19 wakati wajumbe wakiwa bado mjini Dodoma.
“Pamoja na lugha ya kejeli
inayotumiwa na Serikali kuniita mnafiki, busara ya kawaida ilitakiwa kutumika
kufanya maandalizi ya kuwarudisha wajumbe nyumbani na kuandaa makabidhiano,”
alisema.
Alisisitiza kuwa Serikali ilikuwa na
wajibu wa kuwarejesha makwao wajumbe wa tume hiyo, hata kama muda wa kisheria
wa kufanya kazi ulikuwa umepita.
“Niliwasilisha Rasimu Machi 18, 2014.
Tume imevunjwa Machi 19, 2014 wakati wajumbe wako Dodoma. Pamoja na lugha ya
kejeli iliyotumiwa na Serikali na kuniita mnafiki, busara ya kawaida
ingeonyesha umuhimu wa Serikali kujipa muda wa kufanya maandalizi ya
kuwarudisha wajumbe nyumbani,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Hata kama sheria ilitaja muda wa
kuvunja Tume bado ilikuwa ni wajibu Serikali kufanya mipango ya safari ya
wajumbe baada ya kumaliza kazi. Sheria haikuizuia Serikali kufanya hilo. Huo ni
wajibu wa Serikali na utaratibu wa kawaida unaotumiwa na Serikali kwa tume zote
inazoziunda. Inaonekana Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliwekewa utaratibu
tofauti. Kulikoni?”.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment