Mhariri Mkuu wa DW Alexander Kudascheff .
Rwanda ilikuwa ni nchi yenye makovu
mazito. Anasema hivyo Mhariri Mkuu wa DW Alexander Kudascheff ambaye alikuwako
Rwanda mwaka 1994 akiwa mwandishi wa kwanza wa DW kurepoti baada ya mauaji ya
halaiki nchini humo
Katika mahojiano na Dirke Köpp wa DW
anazungumzia juu ya fikra zake kuhusu mauaji hayo na dhima ya jumuiya ya
kimataifa wakati huo na hivi sasa. Muda mfupi baada ya kutokea kwa mauaji hayo
ya halaiki Kudascheff aliripoti kutoka Rwanda kwa ajili ya Deutsche Welle
ambapo alizunguka nchini kote kwa kutumia gari na hadi Goma mashariki mwa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakati huo ikijulikana kama Zaire kuona hali ya
wakimbizi.
Wakati huo waandishi wengi wa habari
wa kigeni walikuwa hawako Rwanda bali walikuwa wakirepoti juu ya kile
kilichokuwa kikitajwa kama balaa la wakimbizi huko Goma. Wale waliokuwa Rwanda
utashi wao mkubwa ulikuwa msako wa wauaji wa Kihutu ambao walikuwa wamekimbilia
mafichoni.
Akiwa na dereva wake kutoka Uganda
wameitembelea nchi nzima na hadi hii leo jambo moja limekuwa na mvuto wa kudumu
kwake:kwamba Rwanda ni nchi zuri ajabu na kujuwa kwamba watu wake ni wa
kupendeka kweli licha ya kuwa kwenye hali ya kuathirika vibaya.
Umegunduwa kwamba watu nchini humo
walikuwa wanapendeka ....jambo ambalo wasafiri wengi wamelizungumzia. Lakini
wakati huo huo Wanyarwanda wengi wakati wa mauaji ya halaiki walidiriki kutenda
unyama usiosemeka Uliweza kuitafakari vipi hali hiyo?
Yumkini tulikutana na wale waliokuwa
wahanga.Kwa vyo vyote vile ni vigumu pia hata kufahamu vipi Wajerumani
walithubutu kuwapeleka watu milioni sita ili wakauwawe kwenye vyumba vyenye
gesi ya sumu.Nafikiri wakati huo nililiona jambo hilo kama aina fulani ya
mripuko wa machafuko na wakati ulipomalizika watu walirudi tena kwenye fahamu
zao.
Rwanda ilikuwa ni nchi yenye makovu
mazito.Wakati unapozunguka na gari unapishana na mrundiko wa mabufuru na
unawasikia watu wakizungumzia juu ya jinsi ndugu zao walivyokufa au
kuuwawa.Kila unapokuweko unagunduwa kwamba watu walikuwa wakitaka kuzungumzia
juu ya kile kilichowakumba. Ulikuwa ukiona kile kiliomo mawazoni
mwao,mchanganyiko wa furaha na aibu kwa kuweza kunusurika halikadhalika hofu
juu ya mustakbali wao.Kipi kiko mbele yetu ?
Hata hivyo wakati wa mauaji hayo ya
halaiki macho ya ulimwengu yalikuwa hayako kwa Rwanda. Pia kwa kuangalia
yaliyopita kama mwandishi habari, mtu inabidi aone aibu kwa kutoweka nadhari
kubwa juu ya kile kilichokuwa kinatokea nchini humo wakati huo.Lakini walioko
kwenye nafasi za uwajibikaji wakati huo wana sababu ya kuona aibu zaidi:hususan
Umoja wa Mataifa ambayo ilishindwa kabisa kuchukuwa hatua.Lakini vivyo hivyo
kwa mataifa ya magharibi,Jumuiya ya Kujihami ya NATO na hasa Ubelgiji mkoloni
wa zamani wa Rwanda.Ubelgiji ina uhusiano wa muda mrefu na Rwanda na pia
walijiuliza wapi tulipokosea?Kwa nini hawakuweza kuyakomesha mauaji hayo ya
halaiki au angalau kuyazwiya?
Paul Kagame amekuwa rais wa Rwanda
tokea mwaka 200. Amekuwa akijaribu kuleta upatanishi,miongoni mwa mambo mengine
kwa kupiga marufuku watu kujitambulisha kwa misingi ya ukabila. Una fikra gani
kuhusu mtizamo huo?
Nakubaliana na fikra ya msingi
kutofikiria kwa kuzingatia makundi ya kikabila.Kwa njia hii mtu huondokana na
mila za kibaguzi. Lakini je hiki ni kitu kinachoweza kuamrishwa kutoka juu
kwenda chini?Nchi za Kisoshalisti zimelijaribu jambo hilo mara kwa mara bila ya
mafanikio kwa sababu mara tu ujamaa unapokuwa umeondoka matatizo yote ya utaifa
huibuka upya.
Ningelichukuwa mtizamo tafauti kwa
Paul Kagame.Kwa upande mmoja sera yake za kiuchumi ni za mafanikio makubwa.Kwa
upande mwengine yeye ni kiongozi kutoka mojawapo ya makundi ya kikabila na sio
rahisi kwa wengine kumkubali. Katika mahojiano niliyofanya na Kagame miaka
mitano au sita iliopita alinipa hisia kuwa ni mtu mwenye amani na nafsi yake.
Alionekana kuwa ni mtu ambaye yumkini alihisi kuwa yeye pia alikuwa amefanya
makosa lakini aliamini kwamba sera zake zilikuwa muhimu na sahihi. Aidha hii
iwe ndio hali ilivyo au iwapo makundi mawili ya kikabila yameondokana na
tafauti zao ni jambo ambalo yumkini likadhihirika katika kipindi cha baada ya
Kagame.
Wakati ilipokabiliwa na mauaji hayo
ya halaiki hapo mwaka 1994 Jumuiya ya Kimataifa ilishindwa vibaya sana
kuyakabili. Kutokana na kushindwa huko kukaibuka kanuni ya wajibu wa kutowa
ulinzi.Kwa kiasi gani Jumuiya ya Kimataifa hivi sasa inatimiza wajibu huo?
Haitimizi wajibu huo. Kibahati
sambamba na mauaji hayo ya halaiki tulikuwa na mzozo huko Balkan ambapo
tulijiuliza masuali hayo hayo.Tamko mashuhuri la Katibu Mkuu wa zamani wa NATO
Manfred Wörner kufuatia shambulio la kuvizia lililofanyika kwenye uwanja wa
soko huko Sarajevo - "Wakati wa kuchukuwa hatua umefika" imekuja
kuzama kwenye mawazo ya watu wengi.
Kiuadilifu nafikiri hakuna chochote
cha mjadala hapa.Ilibidi kila kitu kifanyike kuwasaidia watu hao.Pia
tulijiuliza wenyewe suala hili kwa kuangalia nyuma historia yetu. Je majeshi ya
Muungano yalipaswa kushambulia njia za reli zinazoelekea kwenye kambi ya mateso
ya Auschwitz?
Ukiniuliza kama mwandishi habari
mwangalizi kwa kutumia busara kutowa maoni ya dhati iwapo nafikiri kuingilia
kati kungelisaidia na kuwa na maana kwa kuzingatia kipindi cha muda mrefu au
kwa hatua ya kujenga taifa ingelinibidi niseme 'Hapana siamini ingelisaidia'.
Unaweza kuingilia kati kwa muda mfupi kujaribu kutuliza hali, kujaribu kuzuwiya
mripuko wa volkano wenye maafa.Lakini baada ya hapo inabidi uondoke haraka
kadri inavyowezekana ili kwamba wale wanaoishi kwenye volkano hiyo waweze
kukabiliana na hali hiyo wao wenyewe.Mwanzoni mambo yalikwenda vizuri
Afghanistan na hata kwa wafanya kazi wa misaada lakini baadae katika mwaka 2004
au 2005 hali ilibadilika kabisa.
Kulikuwa na hatua za kuingilia kati
zilizoshindwa kabisa kama vile Somalia na nyengine kushindwa kwa kiasi fulani
kama vile Bosnia na mahala pengine ambapo matokeo yake bado hayako wazi mfano
Kosovo.Hatuwezi kusema mambo yatakuwaje Jamhuri ya Afrika ya Kati au nchini
Mali.
Baadae Jumuiya ya Kimataifa ilikuja
kuendeleza uchunguzi kuhusu mauaji ya halaiki na kurudisha haki kwa kupitia
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa ajili ya Rwanda. Nchini Ujerumani na hata
Ufaransa kesi za mauaji ya halaiki zimekuwa zikiendeshwa. Una mawazo gani juu
ya majaribio haya yaliochelewa kukabiliana na kile kilichotokea?
Nafikiri ni vyema kwa dunia hii
kwamba watu wanaohusika na uhalifu wa ukubwa huo wanakuwa hawana sababu ya
kuamini kuwa wanaweza kuachiliwa bila ya kuadhibiwa.Hiyo ndio sababu kwa mfano
kwa nini nafikiri kwamba mlinzi wa zamani wa kambi ya mateso ya Auschwitz
mwenye umri wa miaka 90 bado anapaswa kushtakiwa.Kwani wakati fulani aliwahi
kuwalazimisha hata watoto wadogo wa miaka miwili wakauliwe kwenye vyumba vya
gesi ya sumu ........kwa hiyo kwangu mimi umri haujalishi.Kwa hiyo fikra ya
kuwepo kwa Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu kuona kwamba dunia
haitomuachilia mtu akwepe kuhukumiwa kwa uhalifu wa aina hiyo ni sahihi.
Aidha mahakama hiyo ni ya mafanikio
au la hilo ni suala jengine.Kwa vyovyote vile wengi wa wahalifu hao wako huru
na wanakwenda watakako tena chini ya uwezo wa Jumuiya ya Kimataifa kuwatia
nguvuni. Wengi hawashtakiwi hadi pale hali zao zinapodoofika. Wengine katu
hawakuwahi kabisa kufunguliwa mashtaka.
Mwandishi : Dirke Köpp/Mohamed Dahman
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
No comments:
Post a Comment