Nigeria imekuwa taifa kubwa zaidi
kiuchumi barani Afrika, na kuipiku Afrika Kusini, baada ya takwimu mpya
kupandisha pato la jumla la ndani la taifa hilo hadi kufikia dola za marekani
zaidi ya bilioni 500.
Wakala wa takwimu wa Nigeria
ulitangaza pato jipya la taifa hilo linaloongoza kwa uzalishaji mafuta barani
Afrika kuwa ni dola za Marekani bilioni 509.9, karibu mara mbili ya kiwango
kilichokuwa kinakadiriwa kabla ya kukokotolewa upya. Thamani hii mpya ya pato
la ndani la Nigeria inajumlisha sekta kama vile mawasiliano, habari na
teknolojia, muziki, biashara za mtandaoni na fillamu za Nollywood, ambazo
hazikuwepo wakati mahesabu ya mwisho yalipofanyika mwaka 1990.
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan.
Wakati huo kulikuwepo na simu za
mezani 300,000. Hivi sasa Nigeria ina watumiaji wa simu za mkononi milioni 100.
Takwimu hizo mpya zinazingatia ukuaji katika sekta za kilimo na utalii, ambazo
zimekuwa kwa kiasi kikubwa tangu nchi hiyo iliporejea kwenye mkondo wa
demokrasia mwaka 1999, na kukomesha miongozo kadhaa ya utawala wa kidikiteta.
Afrika Kusini yaachwa mbali
Nigeria sasa imeipiku Afrika Kusini
ambayo pato lake la jumla la ndani la dola za Marekani bilioni 353 ndiyo
lilikuwa linahesabiwa kuwa kubwa zaidi barani, na ambayo ndiyo nchi pekee ya
Kiafrika mwanachama wa kundi la mataifa 20 yaliyoendelea kiuchumi G20.
Meneja wa uwekezaji Kevin Daly kutoka
shirika la usimamizi wa mali la Aberdeen la nchini Uingereza, na ambalo
linawekeza Nigeria, alisema mafanikio ya Nigeria ni ukumbusho kuwa Afrika
inasonga mbele licha ya changamoto inazokabiliana nazo kwa sasa. Daly
alibainisha kuwa ni bilionea wa Kinigeria Aliko Dangote, ambaye anajenga
kiwanda kikubwa zaidi binfasi cha kusafisha mafuta barani Afrika.
Wawekezaji watavutiwa na ukweli
kwamba, wakati mafuta yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato ya serikali, kwa
asilimia 80, uzalishaji wa mafuta unapungua wakati sekta za kilimo na huduma za
mawasiliano zinazidi kushamiri.
Nigeria imekuwa mpokeaji mkubwa zaidi
wa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni barani Afrika licha ya matatizo mengi
yanayoikabili, kuanzia rushwa iliyokithiri na wizi wa mafuta vinavyoigharimu
nchi karibu dola milioni 20 kila siku, hadi kwenye uasi wa kundi la Kiislamu
kaskazini-mashariki, ambao umewaua watu zaidi ya 1,200 mwaka huu peke yake, na
umeme usiyo wa uhakika, unaozifanya biashara zitegemee majenereta.
Waziri wa fedha Ngozi Ikonjo-Iweala
aliuwambia mkutano wa waandishi wa habari jana kuwa takwimu hizo mpya
zinaifanya Nigeria kuwa nchi ya 26 kwa uchumi mkubwa duniani, na zinapandisha
pato lake la mtu mmoja mmoja hadi kufikia dola za Marekani 2,688, na kushika
nafasi ya 121 duniani kutoka 135.
Maskini hawanufaiki
Hata hivyo kiwango hicho bado ni
kidogo ikilinganishwa na Afrika kusini ambayo pato lake la mtu mmoja mmoja ni
dola za Marekani 7,336 kwa wakaazi wake milioni 48. Mchambuzi wa masuala ya
fedha Bismark Rewane aliyaita marekebisho hayo kuwa ni majivuno tu, na kwamba
maisha ya raia hayataboreka kesho kwa sababu ya tangazo hilo.
Licha ya mafanikio ya kiuchumi, Nigeria bado inakabiliwa na changamoto kubwa zikiwemo miundombinu duni
Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa
kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Nigeria kilipanda kutoka asilimia 12.7
mwaka 2007 hadi asilimia 23.9 mwaka 2011, wakati benki ya dunia ikisema ukosefu
wa ajira miongoni mwa vijana ni asilimia 38, lakini wachambuzi wanasema
kinakaribia asilimia 80 katika maeneo mengi ya nchi.
Mwandishi: Iddi Ismail
Ssessanga/ape,rtre,afpe
Mhariri: Hamidou Oummilkheir.
No comments:
Post a Comment