Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakipitia kabrasha la
mapendekezo ya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya kanuni za Bunge hilo mjini
Dodoma jana. Kutoka kushoto ni Tundu Lissu, Ismail Jussa, Profesa Ibrahim
Lipumba na Godbless Lema. Picha na Silvan Kiwale
Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi
Ombeni Sefue alilieleza gazeti hili kuwa kwa hali ya mchakato huo ilivyo sasa,
wameshindwa kufikia lengo hilo, lakini hawajakata tamaa kuhusu kupatikana
Katiba Mpya ndani ya mwaka huu.
“Kweli matarajio ya awali yalikuwa
hayo, lakini kama unavyoona hali ilivyo, ni vigumu kusema matarajio mengine,
ingawa majadiliano yaliyofanywa mwaka huu ni lazima Katiba inayopendekezwa
iwasilishwe kwa wananchi na mwakani tutakuwa na Katiba Mpya,” alieleza Balozi
Sefue.
Katika hali isiyoeleweka Balozi Sefue
alisisitiza msimamo wa awali wa Serikali kwamba Katiba itakayopatikana
itatumika kwenye Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.
Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo na
Demokrasia (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, alisema hilo ni fundisho kwa Serikali
kwamba kiburi na jeuri havitakiwi katika masuala yanayohusu umma.
Alisema muda huo wa kupatikana Katiba
Mpya ulipotangazwa, walioanzisha kilio cha kudai Katiba Mpya nchini ambao
aliwataja kuwa ni vyama vya upinzani vya siasa, taasisi mbalimbali za kijamii
walipinga na kutoa ushauri kwa Serikali, lakini walipuuzwa.
Dk. Slaa alisema walipendekeza kwamba
badala ya kupeleka mchakato wa Katiba mchakamchaka, warekebishe kwa mara ya 15
Katiba inayotumika, ili iende na wakati wa sasa ikiwamo Uchaguzi Mkuu ujao kwa
lengo la kutoa muda wa kutosha kwa mchakato wa taifa kupata Katiba Mpya.
“Lakini walitukebehi na kututukana
sana, sasa kiko wapi Aprili 26 hiyo hapo na Katiba haijapatikana na kusema
itapatikana mwaka huu na kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani ni ndoto za
mchana,” alieleza Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisema tukio hilo liwe
fundisho kwa Serikali, wawe wakweli, wanyoofu na wafahamu kuwa nje ya Serikali
kuna watu makini na wanaojua vilivyo mchakato wa Katiba.
Alisema ana taarifa za Bunge Maalumu
kuahirishwa Mei 9, 2014 ili kupisha Bunge la Bajeti. Hivyo mategemeo ya Katiba
Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, yanatia shaka.
“Kwa akili ya kawaida tu isiyohitaji
elimu ya chuo chochote, kutumia Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ni jambo
lisilowezekana kwa hiyo waache kutuletea matumaini yasiyokuwapo, sisi siyo
watoto wadogo,” alieleza Dk. Slaa.
Kauli ya LHRC
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo Bisimba, alisema siyo tu Serikali imeshindwa
kutimiza ahadi ya muda iliyojiwekea, bali hata mchakato wenyewe haueleweki.
Dk. Bisimba alisema kwa hali ilivyo,
hawana hakika ya kupata Katiba na ikipatikana haitakidhi matakwa ya wananchi,
kwa kuwa wanataka Katiba ya watu siyo ya kundi moja la watu.
“Mambo ya nchi hii tunayafahamu,
inaweza ikapatikana kwa nguvu lakini wajue wananchi wataikataa na hata
ikilazimishwa, haitakidhi mahitaji, itaweza kuathiri ustawi wa taifa,” alieleza
Dk. Bisimba.
Alisema hilo waliliona mapema,
wakataka kila hatua ya mchakato ipewe muda wa kutosha kabla ya hatua nyingine,
ili wananchi waelimishwe lakini hawakusikilizwa.
Alisema kuwa katika mazingira
hayohayo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifanya kazi kubwa hadi kufanikisha
maoni ya wananchi kupatikana na kutengeneza Rasimu ya kwanza na ya pili
iliyowasilishwa bungeni Machi 18, 2014, lakini kwa jinsi Bunge Maalumu
linavyoendeshwa, kuna kila dalili kwamba kazi hiyo itaharibiwa.
“Wakichezea Rasimu wajue wanachezea
maoni ya wananchi, wanaoweza kuyakataa kupitia kura ya maoni na hivyo
kusababishia taifa hasara isiyomithilika,” alieleza Dk. Bisimba.
Dk. Bisimba alisema mchakato huo
umegharimu taifa fedha nyingi, muda mwingi, nguvu, akili, afya na hata uhai wa
watu, hautakiwi kufanyiwa mzaha.
Alipotafutwa Waziri wa Katiba na
Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro ili kuzungumzia suala hilo jana hakupatikana,
lakini Naibu Waziri wa wizara hiyo Angela Kairuki, alisema kuwa kwa hali ilivyo
ni dhahiri haiwezekani kupata Katiba Mpya kwa muda huu tofauti na ilivyodhaniwa
awali.
Hata hivyo, Kairuki alisema hawezi
kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika mchakato huo kwani mwenye mamlaka ya
kuzungumzia ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba ni mwenyekiti wake, Samuel Sitta.
“Hata hivyo tunachotakiwa kuzungumzia
ni ubora wa kazi inayofanyika ili kufikia lengo la kupata Katiba itakayoongoza
nchi kwa miaka 50 ijayo,” alisema Kairuki.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment