Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili (DW) Andrea Schmidt.
Jambo hilo lisingelipaswa kutokea:
Mauaji ya halaiki mbele ya macho ya ulimwengu! Hata watoto wachanga na vikongwe
waliuwawa. Wanamgambo waliteketeza hata nyumba za ibada ambapo watu walikuwa
wamejihifadhi.
Katika kipindi cha siku 100 serikali
ya wakati huo na wanamgambo wake waliwauwa zaidi ya watu 800,000. Hususan
walioandamwa walikuwa ni watu wa jamii ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa
wastani ambao walikuwa wamejaribu kuwasaidia majirani na marafiki zao.
Lakini suala ni kwa nini hakuna mtu
aliechukuwa hatua licha ya kutolewa kwa tahadhari na mapema?Takriban miezi
mitatu kabla ya kuzuka kwa mauaji hayo,mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha
Umoja wa Mataifa(UNAMIR) nchini Rwanda Romeo Dallaire alituma ujumbe kwa wakuu
wake walioko New York ambapo alionya katika kile kinachojulikana kama "Fax
ya Mauaji ya Halaiki " yenye kufafanuwa mipango ambapo kwayo wanamgambo
wakiwa kwenye makundi ya kuanzia watu 40 wanaweza kuuwa zaidi ya watu 1,000
katika kipindi kisichozidi dakika 20.
Wakati mauaji hayo yalipokuwa
yamepamba moto,Dallaire alituma tena ujumbe wa dharura kwa Umoja wa Mataifa wa
kuisihi itume wanajeshi zaidi wa kulinda amani na kuwapa mamlaka thabiti ya
kulinda wananchi.Badala yake Umoja wa Mataifa ukaanza hata kupunguza vikosi
vyake vilioko nchini humo yumkini kutokana na hofu ya kuja kukabiliana na balaa
la kushindwa kama lile lililowakuta wakati ilipoingilia kati nchini Somalia na
wakayafumbia macho mauaji hayo na kukataa kukiri juu ya ouvu huo uliokuwa
ukitokea.
Wakati huo huo Ufaransa iliendelea
kuipelekea silaha serikali ya nchi hiyo hadi mwezi wa Juni yaani badala ya
kuchukuwa hatua ya kuingilia kati kijeshi kwa "Operesheni ya
Turquoise(Takwaz)" ili kuwalinda raia,jeshi la Ufaransa liliwachilia
wanamgambo waliohusika na mauaji ya halaiki kuondoka na silaha zao na
kukimbilia Congo iliokuwa ikijulikana kama Zaire wakati huo.
Wajibu mpya wa kulinda wananchi
Hususan Umoja wa Mataifa ulikuwa
umefedheheka kwa kushindwa kutimiza wajibu wake.Lakini wamejifunza nini
kutokana na hilo?Kutokana na kuboronga huko Rwanda,Umoja wa Mataifa na juhudi
zake za Kuwajibika kutowa Ulinzi hapo mwaka 2005 umebuni mfumo mpya ambapo
mataifa yanawajibishwa kulinda wananchi wake dhidi ya ukiukaji mkubwa wa haki
za binaadamu, mauaji ya halaiki na kuangamiza jamii.Iwapo nchi inashindwa
kutimiza wajibu huo wa kutowa ulinzi jumuiya ya kimataifa inaweza kutimiza
wajibu huo na kuingilia kati kijeshi.
Lakini msimamo wa uadilifu pekee
hautoshi.Umoja wa Mataifa haukuzuwiya mauaji ya raia wakati wa vita vya wenyewe
kwa wenyewe nchini Sri Lanka .Hata hivi sasa kuna maeneo ya vita ambayo ni
changamoto kwa jumuiya ya kimataifa kuthibitisha kile ilichojifunza kutokana na
Rwanda.Kwa mfano maangamizi ya jamii yanayofanyika Jamhuri ya Afrika ya Kati au
hali ya machafuko nchini Sudan Kusini.
Lakini kwa nini shughuli za kulinda
amani za Umoja wa Mataifa bado zinakosa mamlaka thabiti ya kutekeleza majukumu
yake?Changamoto ni pamoja na umuhimu wa kuzingatia tahadhari zinazotolewa na
mapema kama vile matumizi ya nguvu kupita kiasi.Kuweka viashiria kabla ya hali
kuwa mbaya,wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wawe wamepatiwa
mafunzo vizuri, kupatiwa silaha na kuwa tayari kukabiliana na hali hiyo kwa
ufanisi na uwajibikaji.
Congo ni mfano
Kikosi cha Umoja wa Mataifa kilioko
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kinaweza kutumiwa kama mfano wa mambo yote kwa
matatizo na njia zinazoweza kutumika kwa ufumbuzi katika shughuli za kulinda
amani.Kwa miaka mingi kikosi hicho kimekuwa kikishutumiwa kwa ukosefu wake wa
ufanisi na moja kwa moja kuchukiwa na wananchi wa nchi hiyo.Kutokana na
kutokuwa na mamlaka thabiti ya kutekeleza majukumu yake mara nyingi hujifanya
hawaoni wakati watu wanapouwawa na wanawake kubakwa. Hata hivyo hapo mwaka 2013
kutokana na kuwepo kwa kikosi kipya cha kuingilia kati haraka cha wanajeshi
kutoka Afrika chenye mamlaka mpya hali hiyo imebadilika.
Hususan shughuli za kulinda amani za
Umoja wa Mataifa hazipaswi kushindwa kutokana na ukosefu wa fedha na
rasilmali.Jumuiya ya Kimataifa lazima ijitolee kwa kila hali kutowa msaada kwa
haraka na kuwa na ufanisi hususan kulinda haki za binaadamu katika nchi
husika.Matumizi mabaya kutokana na sababu za kisiasa au za kiuchumi lazima
yaepukwe.
Jumuiya ya Kimataifa hapo mwaka 1994
ilitenda kosa kubwa sana.Lazima isifumbie macho tena uhalifu wa aina
hiyo.Mauaji ya halaiki yamegharimu maisha ya watu 800,000 nchini Rwanda. Watu
wengine milioni tatu wameuwawa katika vita vya Congo ikiwa ni matokeo ya mauaji
hayo ya halaiki.Jambo hilo pia halipaswi kusahauliwa.
Mwandishi: Andrea Schmidt/Mohamed
Dahman
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
No comments:
Post a Comment