Mjane wa Abasi Mwila, Judith Mwila akipanga bidhaa katika genge lake lililopo Tabata Liwiti jijini Dar es Salaam jana. Judith ni miongoni mwa watu tisa watakaonufaika na fidia ya Sh672 bilioni baada ya kumpoteza mume wake, Abasi katika shambulio la kigaidi la mwaka 1998 kwenye ubalozi wa Marekani nchini. Picha na Michael Jamson
Dar es Salaam. Baadhi ya wanafamilia
wa waliopoteza ndugu kwenye shambulio la ugaidi katika Ubalozi wa Marekani
jijini Dar es Salaam mwaka 1998, wameelezea kufarijika kutokana na malipo ya
fidia, licha ya kwamba hayawezi kurejesha uhai wa waliokufa.
Wakizungumza na gazeti hili kwa
nyakati tofauti, ndugu hao walisema, licha ya mahakama nchini Marekani kuwapa
fidia lakini pengo la jamaa zao halitazibika.
Wiki iliyopita, Mahakama Kuu ya
Marekani, ilitoa amri ya kuwalipa fidia ya dola za Marekani 957 milioni (Sh1.555
trilioni) waathirika 23 wa shambulio hilo.
Jaji Thomas Bates katika hukumu yake
alisema kati ya fedha hizo, Dola za Marekani 420 milioni (Sh670 bilioni)
watapewa ndugu wa marehemu watano na waathirika wanne wa Tanzania wakati kitita
kilichobaki kitakwenda kwa waathirika ambao ni Wamarekani.
Jaji Bates alisema Serikali za Iran
na Sudan zitawajibika kulipa fidia hizo kutokana na kuhusika na mashambulio
hayo mabaya kuwahi kutokea Afrika Mashariki.
Mmoja wa jamaa waliopoteza maisha
katika tukio hilo, Kulwa Ramadhan alisema anasubiri kuletewa taarifa zaidi
kuhusu taratibu za kupata fidia hiyo.
“Huwezi kuwa umeridhika na fidia kwa
kuwa tumepoteza ndugu zetu lakini pia hata hicho kilichopatikana hatukukitarajia
kupata,” alisema Ramadhan.
Alisema kuna baadhi ya jamaa wa
marehemu watano hawakuingizwa kwenye idadi ya watakaopata fidia kutokana na
kuchelewa kujiandikisha katika kesi hiyo.
“Baada ya tukio uongozi wa Ubalozi wa
Marekani ulituambia tutoe taarifa zetu zote za mawasiliano na kwamba
tusibadilishe namba za simu kwa ajili ya kuwasiliana kinachojiri.
“Lakini kuna baadhi ya jamaa
walibadilisha namba zao na kufanya mawasiliano kuwa magumu hivyo kushindwa
kuingizwa katika idadi ya wadai katika kesi hiyo,” alisema.
Ramadhan aliyempoteza pacha wake,
Dotto Ramadhani alisema baadhi ya jamaa walijitokeza baadaye baada ya hatua
muhimu za kesi kufanyika kitendo ambacho kiliwazuia kushiriki katika kesi.
Waathirika wengine
Naye Judith Mwila aliyempoteza mume wake
kwenye tukio hilo, alisema anashukuru Ubalozi wa Marekani pamoja na mawakili
waliowasaidia kufanikisha kesi hiyo.
“Binafsi nimepata taarifa kamili jana
(juzi) kutoka kwenye gazeti la Mwananchi na sikutarajia kama tungeshinda kesi
hiyo na tukapewa fidia ya fedha kiasi hicho. Hata hivyo tunaendelea kusubiri
taarifa za mawakili wetu kuhusu taratibu zinazofuata kupata fedha hizo,”
alisema.
Aliongeza kuwa iwapo atapata sehemu
ya fedha hizo atashauriana na watoto wake jambo la kufanya ikiwamo kufanya
biashara kubwa. Mwila ana watoto watatu alioachiwa na marehemu mume wake.
Alisema kuwa tangu mchakato wa kesi
ulipoanza mwanzoni mwa mwaka 2001, Ubalozi wa Marekani na mawakili wao,
walimpeleka Marekani mara mbili.
“Kesi hii imedumu muda mrefu. Mara ya
kwanza nilikwenda 2001 kutoa ushahidi na mara ya mwisho ni 2010 na tangu wakati
huo tulikuwa tukipewa tu taarifa juu ya maendeleo ya kesi,” alisema Mwila.
Kwa upande wake, Grace Paulo ambaye
alifiwa na mumewe Elisha Paulo alisema: “Ninamshukuru Mungu kwa sisi kushinda
kesi hii na hivyo tunasubiri mawasiliano na wahusika kufahamu jinsi ya kupata
fedha hizo.
“Tumekuwa tukiishi kwa shida sana,
hivyo hizo fedha zitatusaidia kujikwamua na matatizo yanayonikabili na
mwanangu,” alisema Paulo ambaye aliachiwa mtoto mmoja aitwaye Mary Paulo.
Kwa mujibu wa waathirika hao,
Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Misaada la Marekani (Usaid) liliwapa
msaada wa kuwasomesha watoto pamoja na makazi ili kupunguza makali ya maisha.
Hata hivyo, wengi wao wanaendelea
kufanya biashara ndogondogo kutokana na misaada hiyo kuwekwa katika eneo
maalumu la ada za watoto.
“Kwa sasa ninafanya biashara ya kuuza
nguo za mitumba na nilishaondoka Dar es Salaam mara tu baada ya msiba mwaka
1998 kutokana na maisha ya mjini kuwa magumu.
“Baadaye Ubalozi kupitia taasisi za
kiraia walinitafuta hadi wilayani Mpwapwa ndipo waliponijengea nyumba
ninayoishi sasa,” aliongeza Paulo anayeishi mkoani Dodoma.
Jamaa hao pia walisema kuwa gharama
halisi za kesi hiyo hawazifahamu kutokana na kesi nzima kusimamiwa na Serikali
ya Marekani na mawakili wao.
Hata hivyo, uhakika wa kupata fedha
hizo unabaki mikononi mwa wakili wa jamaa hao, Thomas Fortune Fay ambaye baada
ya hukumu hiyo alisema anafuatilia jinsi ya kupata fedha kwa Serikali za Sudan
na Iran.
Alisema ataangalia jinsi ya
kutaifisha baadhi ya mali za nchi hizo ili kupata fedha za kuwalipa waathirika
hao.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment