WAKATI serikali ikidai kuwa hati
halali za Muungano zipo Umoja wa Mataifa (UN), umoja huo umeikana kwa kuweka
wazi kuwa hakuna ushahidi wa jambo hilo.
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima
Jumapili kutoka kwa Ofisa wa Masuala ya
Sheria na Mikataba wa UN, Andrei Kolomoets, zilibainisha kuwa hakuna ushahidi
wa sekretarieti ya umoja huo kuzisajili hati hizo.
Kolomoets alibainisha kuwa kama hati
hizo zingekuwa zimesajiliwa na Umoja wa Mataifa kungekuwa na kumbukumbu zake.
Sakata la hati za Muungano liliibuka
bungeni wiki iliyopita ambapo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walionyeshwa
hati ya sheria ya kuridhia mkataba wa Muungano zilizokuwa na saini walizodai
zimeghushiwa.
Saini za Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, hayati Julius Nyerere na aliyekuwa Katibu wa Bunge, Pius
Msekwa, zilionekana zina utofauti mkubwa, jambo lililozusha mtafaruku miongoni
mwa wajumbe.
Baadhi ya wajumbe walizipinga sheria
hizo za hati za Muungano wakidai saini za Nyerere na Msekwa zimeghushiwa, kwa
sababu zinatofautiana
zikionekana kufanyiwa utaalamu wa
kompyuta.
Mathalani katika hati ya Tanganyika
No. 22 ya 1964, herufi mbili za jina la Julius (us) zinatofautiana na herufi
nne za mwanzo (Juli) wakati kwenye hati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania No.
18 ya 1965 herufi zote
zimeandikwa kwa ufanano.
Utata mwingine upo kwenye herufi ‘K’
ya jina la katikati la Kambarage, ambapo hati ya mwaka 1964 herufi hiyo
inatofautiana na ile ya mwaka 1965.
Hata saini ya aliyekuwa Katibu wa
Bunge la Jamhuri wakati huo, Pius Msekwa, zinatofautiana kwenye hati hizo,
hivyo wajumbe kadhaa kutaka iletwe halisi (original) badala ya nyaraka za
sheria zilizoidhinisha Muungano.
Nyaraka hizo za sheria za kuridhia
hati za Muungano zimepingwa na wajumbe wengi wa Bunge wakidai zina shaka
kutokana na kuridhiwa na upande mmoja wa Bunge la Tanganyika bila Baraza la
Mapinduzi kuridhia.
Mkorogano huo ulizidi baada ya
Mwenyekiti wa kamati namba mbili inayoongozwa na Shamsi Vuai Nahodha, kudai
kuwa aliambiwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kuwa hati halali za Muungano
zipo Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar aliiambia kamati namba mbili kuwa hajawahi kuiona hati ya kisheria ya
Zanzibar kuridhia mkataba wa Muungano, ila kwa nafasi yake anaamini ipo.
Nahodha alisema mwanasheria huyo
hakuwahi kuitafuta kwakuwa hakukuwa na matatizo ya kimuungano yenye kuhitaji
azionyeshe hati hizo.
Vuai alisema hati hizo zilipelekwa
Umoja wa Mataifa, kwakuwa kabla ya Muungano uliofanyika Aprili 26, 1964
Tanganyika na Zanzibar kila mmoja alikuwa na kiti cha uwakilishi katika umoja
huo.
Alisema kutokana na Muungano huo
kulilazimika Tanzania kuwa na kiti kimoja, hivyo hati hizo zilipelekwa Umoja wa
Mataifa kuthibitisha Muungano huo.
Maelezo hayo yanaonekana kukinzana
na yaliyotolewa na Katibu wa Bunge
Maalumu, Yahya Hamis Hamad, aliyesema kuwa hati halali ya Muungano ipo na
wanaangalia uwezekano wa kutoa nakala (kopi).
Alisema kopi hiyo itapelekwa
mahakamani kwa ajili ya kuidhinishwa kisheria ili ipelekwe kwa wajumbe wa Bunge
Maalumu.
Hamad hata hivyo alisema jambo hilo
ni lazima walifanye kwa umakini mkubwa, kwakuwa hati hiyo inaweza kupotea.
Msekwa aitwa
Katibu wa zamani Bunge la Jamhuri ya
Muungano aliyekuwa mmoja wa watu waliosaini nyaraka za sheria ya kuridhia hati
hizo, Pius Msekwa, wiki iliyopita aliitwa kwenye kamati kutoa ufafanuzi ambao
hata hivyo ulipingwa na baadhi ya wajumbe.
Pia saini za Msekwa na Rais wa Kwanza
wa Tanganyika, Julius Nyerere, kwenye nyaraka hizo zinatofautiana kati ya mwaka
1964 na 1965, hatua iliyowafanya wajumbe kuomba ziletwe hati halisi za
Muungano.
Katika ufafanuzi wake kwa wajumbe wa
Bunge Maalumu, Msekwa alisema hati ile inasema kutakuwa na serikali ya
Tanganyika na Zanzibar pamoja na Bunge la Jamhuri na Baraza la Mapinduzi, hivyo
ni serikali mbili.
Kuhusu nyaraka za kisheria za Baraza
la Mapinduzi kuridhia hati ya Muungano, Msekwa alisema hajawahi kuziona, bali
aliona picha za kikao cha kuridhia suala hilo.
Pia Msekwa alikiri kuwa saini yake na
ile ya Nyerere kwenye nyaraka za mwaka 1964 na 1965 ni sahihi, na kwamba hazijaghushiwa kama
inavyodaiwa.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment