Waasi wakubaliana na serikali ya Libya kuuza mafuta
Makubaliano yameafikiwa kuondoa
kizuizi cha kusafirisha mafuta mashariki mwa Libya. Mauzo ya mafuta katika nchi
za ngambo nchini humo yaliathirika pakubwa katika kipindi cha miezi minane
iliyopita baada ya kufungwa kwa bandari zilizo katika eneo la mashariki
linalotawaliwa na makundi ya wanamgambo.
Katika mkutano wa waandishi wa habari
uliofanyiwa katika jiji la Beghazi, Waziri wa Maswala ya Haki wa Libya, Salah
Al-Maghani, alithibitisha kuondolewa kwa muda kwa vizuizi vya kuuza mafuta. Vituo
vya mafuta vya Hureiga na Zuetina vilivyo na uwezo wa kuzalisha mafuta mapipa
200,000 kwa siku hivi sasa vimesimamiwa na Serikali.
Vituo viwili vilivyo vikubwa zaidi
nchini humo vya Mashariki mwa nchi vya Ras Lanuf na Sidra vitafunguliwa kwa
muda wa majuma machache yajayo, kulingana na Waziri.
Mapatano yaliafikiwa kati ya makundi
ya wapiganaji yaliyosababisha kufungwa kwa vituo hivyo na kundi ambalo Serikali
ililitaja kama "wapatanishi".
Msemaji wa Waziri Mkuu ameambia BBC
kuwa Serikali imekubali kuwalipa mishahara walinzi wa vituo hivyo vya mafuta.
Juhudi za mwezi uliopita za kufikia
mapatano ya kuanza kuuza mafuta tena katika vituo hivyo hazikufaulu.
Wale wanaozuia mafuta kuuzwa katika
vituo hivyo wamekuwa wakilalamika kuwa sekta ya mafuta nchini Libya inakabiliwa
na ufisadi mkubwa, lawama ambayo imekanushwa na maafisa wa Serikali.
Wapiganaji hao pia wamekuwa wakisema
kuwa wakaazi wa Mashariki wanahitaji mapato makubwa zaidi kutoka kwa mauzo ya
mafuta. Waziri wa Haki sasa anasema kuwa Serikali itachunguza lawama za
ufisadi.
Libya imepata hasara ya zaidi ya Dola
Bilioni tisa tangu kufungwa kwa vituo hivyo vya mafuta. Eneo la Mashariki ndilo
linalozalisha kiwango kikubwa cha mafuta.
Chanzo: BBC Swahili
No comments:
Post a Comment