WANAWAKE katika Kitongoji cha
Makupani, Kijiji cha Saadani chumvi, wanalazimika kusafiri umbali wa kilomita
12 kwa kutumia trekta kufuata huduma ya
kujifungua hospitalini.
Wakizungumza katika mkutano wa
kampeni za mgombea ubunge wa Chalinze kwa tiketi ya CCM, Ridhiwani Kikwete,
wakazi hao walisema wamekuwa wakikabiliwa na mazingira magumu
kutokana na kukosekana kwa usafiri wa uhakika.
Walisema pindi mama mjamzito anapohitaji
huduma hiyo nyakati za usiku, mwekezaji wa Kampuni ya Seasalt ndiye
anayewasaidia trekta hilo kwa ajili ya kumsafirisha mgonjwa, hali ambayo ni ya
hatari kwani kuna uwezekano wa kujifungua njiani.
Wananchi hao walimuomba mbunge
atakayechaguliwa kuhakikisha anawapatia usafiri wa uhakika ili waweze
kuondokana na kero hiyo.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho,
Mohamed Salum, alikiri kuwepo na changamoto hiyo na kusema inachangiwa na
viongozi wa ngazi za juu kutotembelea eneo hilo.
Kwa upande wake, Ridhiwani aliwaomba
wananchi hao wamchague ili waweze kushirikiana kutatua changamoto
mbalimbali jimboni humo.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment