Michael Balou (kulia) akijiandaa kuwatoka viungo wa Simba, Jonas Mkude (namba20) na Henry Joseph katika mechi ya Ligi Kuu Bara, jana Jumapili. Simba ilifungwa mabao 2-1 na kusalia kwenye nafasi yake ya nne katika msimamo wa Bara.
KIPIGO cha mabao 2-1 ilichokipata
Yanga jana Jumapili kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga mbele ya Mgambo JKT,
kimewashitua mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa wakidai kwamba kuna mkono wa
mtu.
Mashabiki hao ambao wengi wao
walitoka Dar es Salaam,
walichanganyikiwa zaidi baada kusikia Azam FC imeipiga Simba mabao 2-1
jijini Dar es Salaam na kuwaacha kwa pengo la pointi saba kileleni katika mbio
za kuelekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Azam imetimiza pointi pointi 53
ambazo zimewaweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa
mara ya kwanza tangu iasisiwe Juni 24, 2007.
Yanga imebaki kwenye nafasi ya pili
na pointi 46 huku Mbeya City ikifikisha pointi 45 na kuzidi kujikita nafasi ya
tatu baada ya kuilaza Prisons bao 1-0 pia jana Jumapili na kufufua matumaini ya
kuwania nafasi ya pili.
Pointi 53 zinaweza kufikiwa na Yanga
au Mbeya City pekee. Matokeo ya Azam na Simba, yanawafanya Wekundu wa Msimbazi
kubaki nafasi ya nne na pointi zao 36 baada ya mechi 23.
Katika mchezo huo wa Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam, hali ya hewa ya mawingu na mvua nyepesi iliwazuia mashabiki
wengi kufika uwanjani kwa hofu ya mvua.
Mashabiki wengi wa Yanga walionekana
kuiunga mkono Simba ili iweze kushinda na kuiwekea kiwingu Azam isiweze
kuendelea kujikita kileleni, lakini mambo yalienda kinyume.
Lakini cha kushangaza mashabiki wa
Simba walikuwa hawashangilii timu yao inaposhambulia au hata ilipopiga bao la
kusawazisha kwa madai kwamba walikuwa hawataki kuinyooshea njia Yanga.
Iliwachukua Azam dakika 16 kupata bao
la kwanza lililofungwa na Khamis Mcha baada ya mpira uliopigwa na Kipre
Tchetche kuelekea langoni mwa Simba kurudi uwanjani na wachezaji wa Simba beki
Joseph Owino na Amissi Tambwe walijichanganya katika kuokoa, ndipo Mcha alipofunga.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha
Simba ambao walilishambulia lango la Azam mara kwa mara huku wakimtumia zaidi
winga, Uhuru Selemani ambaye alikuwa akionyeshana kazi na beki, Gadiel Michael.
Inawezekana haikuwa bahati ya Simba,
kwani dakika ya 26 Uhuru alikosa bao la wazi akishindwa kumalizia pasi safi ya
Ramadhan Singano ‘Messi’. Kipa wa Azam, Aishi Manula, aliuwahi mpira na kuokoa.
Messi alipiga mpira kwa juu dakika ya
31 akiwa ndani ya eneo la hatari la Azam, lakini Tambwe alipiga kichwa
kilichotoka nje ya lango. Hata hivyo, Azam waliamka na kufanya shambulizi kali
dakika ya 33 baada ya Tchetche kupiga kupiga krosi safi iliyomkuta Mcha ambaye
alipiga nje.
Simba ilipata bao la kusawazisha
dakika ya 45 lililofungwa kwa kichwa na Owino akimalizia mpira wa adhabu
uliopigwa na William Gallas kutoka nje eneo la hatari la Azam. Mabao hayo
yalidumu hadi mapumziko.
Azam walikianza kipindi cha pili kwa
kasi na kufika langoni mwa Simba mara kadhaa na dakika ya 56 ikafunga bao la
pili kupitia John Bocco. Bocco alifunga akimalizia mpira uliogonga mwamba na
kurudi uwanjani ambao ulipigwa na Gadiel.
Simba ilicharuka baada ya Azam kupata
bao hilo huku ikimtumia zaidi Uhuru kuanzisha mashambulizi, lakini harakati
zake ziliishia kupiga krosi ambazo zilikosa waunganishaji.
Azam ilifanya mabadiliko ya kuwatoa
Mcha na kuingia Kelvin Friday wakati Simba iliwatoa Messi, Henry Joseph na
Harun Chanongo na nafasi zao zilichukuliwa na Ibrahim Twaha, Abdulhalim Humud
na Awadh Juma.
Hata hivyo mabadiliko hayo
hayakubadili matokeo hayo na kumfanya Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic,
kutoamini macho yake kwa kipigo hicho huku timu yake ikionekana kuimarika.
“Tumecheza vizuri lakini hatukutumia
vyema nafasi sita za mabao ya wazi, naamini tumecheza vizuri kwa asilimia zaidi
ya 60, makosa ya mabeki ndiyo yaliyotugharimu,” alisema Logarusic.
Kocha wa Azam, James Omog alisema:
“Nimefurahi kuwa ushindi huu, ni kama nilivyosema awali kuwa lengo letu ni
kushinda kila mechi iliyo mbele yangu.”
Mgambo yaisimamisha Yanga
Yanga imejiweka katika nafasi ngumu
ya kutetea ubingwa wake kwa kipigo cha jana Jumapili mjini Tanga. Yanga
imecheza mechi 22. Mgambo yenyewe imejiimarisha katika kuhakikisha haishuki
daraja kwa kufikisha pointi 22, ijapokuwa imeng’ang’ania nafasi yao ya 11.
Bao la kwanza la Mgambo lilifungwa
dakika ya kwanza na Fully Maganga ambaye alitumia vyema makosa ya kipa wa
Yanga, Juma Kaseja na beki Kelvin Yondani waliojichanganya wakati
wakirudishiana mpira. Mfungaji aliugonga na kufunga kirahisi.
Yanga ilijitahidi kutafuta bao la
kusawazisha, lakini kila mbinu yake haikufanya kazi ipasavyo na Mgambo kwenda
mapumziko ikiwa mbele.
Yanga ilifanikiwa kusawazisha bao
hilo dakika ya 53 kwa njia ya penalti baada ya beki wa Mgambo, Novart Lufungu,
kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. Penalti hiyo ilifungwa na Nadir Haroub
‘Cannavaro’.
Mgambo ikafunga la pili dakika ya 65
kwa penalti iliyopigwa na Malimi Busungu. Penalti hiyo ilisababishwa na beki
Kelvin Yondani kumvuta jezi mchezaji mmoja wa Mgambo. Katika mchezo huo,
mchezaji wa Mgambo Mohamed Neto alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 30 baada ya
mwamuzi Alex Mahaji kumhisi amevaa nguo zaidi ya moja wakati wa mchezo.
Awali Neto alikuwa na kadi ya njano
baada ya kumchezea faulo mchezaji wa Yanga. Baadhi ya mashabiki walihusisha
uvaaji wa mchezaji huyo na imani za kishirikina wakiamini kuna kitu.
Mbeya City mwendo mdundo
Kwenye Uwanja wa Sokoine jijini
Mbeya, Mbeya City ilitumia dakika mbili tu kuinyoosha Prisons kwa kuilaza bao
1-0. Bao pekee la Mbeya City lilifungwa na Paul Nonga dakika ya pili baada ya
Mbeya City kufanya shambulizi la kushitukiza langoni mwa Prisons.
Mabeki wa Prisons na viungo wake
walikuwa wamepanda kushambulia, lakini walijisahau kurudi haraka kuzuia ndipo
Nonga alipofunga.
Kwa kipigo hicho, Prisons imebaki
nafasi ya 10 ikiwa na pointi 22.
JKT Ruvu yaizima Rhino
Rhino Rangers ya Tabora imezidi
kujiweka katika mazingira ya hatari ya kushuka daraja baada ya kufungwa mabao
3-1 na JKT Ruvu katika mechi iliyopigwa
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Mbagala, Dar es Salaam.
Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) bado ipo mkiani mwa ligi hiyo ikiwa na pointi 13
katika mechi 23 ilizocheza.
JKT Ruvu ipo nafasi ya tisa
ikifikisha pointi 28 katika mechi 23 ilizocheza.
Mabao ya JKT yalifungwa na Idd Mbaga
dakika 24, Emmanuel Swita dakika 34 kwa njia ya penalti baada ya Sosthenes
Manyasi kuangushwa eneo la hatari. Bao la tatu la JKT lilifungwa na Samwel
Kanute dakika ya 82.
Bao pekee la Rhino lilifungwa dakika
ya 48 kwa njia ya penalti na Jerome Gervais baada ya Omary Mtaki wa JKT
kumchezea rafu Rajab Twaha.
Mtibwa yaimaliza Coastal Union
Mtibwa Sugar iliutumia vizuri uwanja
wake wa nyumbani wa Manungu uliopo Turiani, Morogoro baada ya kuifunga Coastal
Union mabao 3-1. Mabao ya Mtibwa yalifungwa na Mussa Mgosi, Mohammed Mkopi na
Jamal Mnyate. Bao pekee la Coastal lilifungwa na Behewa Sembwana.
Katika mchezo mwingine uliochezwa
Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar ilitoka suluhu na Ruvu Shooting.
Chanzo: Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment