Wednesday, April 9, 2014

Mnyika ashupalia sheria ya kuzuia bodaboda

MADEREVA wa pikipiki (bodaboda) jijini Dar es Salaam wamelalamikia kitendo cha Jeshi la Polisi kuwazuia kuingia ndani ya kivuko cha Kigamboni kwa madai ya kuziondoa pikipiki hizo katikati ya jiji.

Wakizungumza kwa jazba jana asubuhi baada ya kuzuiliwa kuingia kwenye pantoni kutoka Kigamboni kwenda Feri, baadhi ya madereva hao walisema hawajatendewa haki kwa kuwa sio wote wanaofanya biashara ya kupakiza abiria, wengine wanazitumia kwa usafiri binafsi.

Bakari Musa, mmoja wa madereva hao, alisema jeshi hilo halikuwapa taarifa ya zuio la wao kuvuka na pikipiki zao hadi watakapokuwa na kibali maalumu.

Alisema kitendo kilichofanywa leo si cha kiungwana kwani kimesababisha wengi wao kuchelewa kazini baada ya kufika Kivukoni na kuzuiwa.

Wakati madereva hao wakilalamikia usumbufu huo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, amesema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick ameudanganya umma kwamba Bunge lilitunga sheria ya kuzuia bodaboda na bajaj kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

“Si kweli kwamba kuna sheria ilipitishwa Machi 12, 2010 kama ilivyoelezwa na mkuu huyo wa mkoa, badala yake tarehe hiyo ni siku ambayo aliyekuwa Waziri wa Miundombinu Dk. Shukuru Kawambwa alitunga kanuni.

“Hata hivyo, kanuni hizo nazo hazikupiga marufuku bodaboda na bajaj kuingia katikati ya jiji bali zilikasimu mamlaka kwa halmashauri za Serikali ya Mitaa kuweka utaratibu wa namna vyombo hivyo vya usafiri vitakavyoingia mjini,” alisema Mnyika.

Alisema kwa kuzingatia maelezo hayo, alimtaka mkuu wa mkoa asitishe agizo lake na halmashauri za jiji hilo ziweke utaratibu kwa mujibu wa kanuni na kuzingatia malengo ya kulinda usalama, kupunguza foleni, kuhakikisha fursa za ajira kwa vijana na usafiri wa gharama nafuu kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Mnyika, sheria ya Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) haikutungwa mwaka 2010 bali ilitungwa mwaka 2001 huku akisisitiza kwamba mwaka 2010 zilitungwa kanuni za Transport Licensing (Motor Cycles and Tricycles) zilizochapwa kwenye gazeti la serikali namba 144 la Aprili 2 mwaka huo.

Hivi karibuni Jeshi la Polisi, Sumatra na viongozi wa madereva, waliwataka madereva wa pikipiki kuendelea kutii amri ya kutoingia mjini kwa pikipiki za miguu miwili (bodaboda) na mitatu (bajaj).

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa operesheni ya kuzuia vyombo hivyo kuingia katikati ya jiji ni endelevu.

“Tutaendelea na operesheni hii, lengo si kuwakomoa bali ni sheria zipo wazi na lazima zifuatwe,” alisema na kuongeza kuwa wanazuia pia kutokana na uhalifu wa kutumia pikipiki uliokithiri hasa maeneo ya katikati ya jiji.


Chanzo: Tanzania Daima

No comments: