JUMLA ya watu 92,939 wanatarajiwa
kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa Chalinze utakaofanyika Jumapili ijayo.
Takwimu hizo zilitolewa wilayani hapa
juzi na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva,
katika mkutano wa maandalizi ya uchaguzi huo uliohudhuriwa na vyama mbalimbali
vya siasa.
Alisema tofauti ya idadi ya wapiga kura waliopo katika daftari la
kudumu la wapiga kura kwa mwaka 2010 na daftari lililohakikiwa mwaka huu ni
watu 80.
Alisema daftari la kudumu la wapiga
kura kwa Jimbo la Chalinze lilikuwa na wapiga kura 92,859 kwa uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010.
Jaji Lubuva alisema wapiga kura
waliokuwa wanaonekana katika daftari zaidi ya mara moja majina yao yameondolewa
na wapiga kura walioandikishwa na wana kadi
ya mpiga kura lakini hawaonekani katika daftari wameingizwa.
“Sababu zilizochangia wapiga kura
kujitokeza mara nyingi ni wapiga kura kujiandikisha zaidi ya mara moja au
wapiga kura kubadili taarifa zao wakati wa zoezi la uboreshaji wa daftari,”
alisema.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius
Mallaba, alisema siku ya uchaguzi ni
marufuku kwa mgombea, chama cha siasa au
wakala kufanya kampeni na kusema kwa
mujibu wa sheria mwisho wa kufanya kampeni ni siku moja kabla ya siku ya
uchaguzi yaani Aprili 5, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment