Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa,Peter Kuga Mziray.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Kuga Mziray, ameonyesha
wasiwasi wake kwamba huenda mvutano mkubwa ukazuka bungeni kesho na Ijumaa
wakati kamati 12 za Bunge Maalum la Katiba zitakapowasilisha taarifa bungeni baada
ya kupitia na kuchambua sura mbili za Rasimu ya Katiba, ya kwanza na ya sita.
Sura ya kwanza inazungumzia Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alama na
Sikukuu za Taifa, Lugha za Taifa na lugha za alama na Tunu za Taifa.
Sura ya sita inazungumzia muundo wa
Muungano, vyombo vya utendaji vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mamlaka ya
serikali ya Muungano, mambo ya Muungano, nchi washirika, mamlaka ya nchi
washirika, mahusiano kati ya nchi washirika, mawaziri wakaazi, mamlaka ya
wananchi na wajibu wa kulinda Muungano.
Akizungumza na NIPASHE jana, Mziray
alisema mambo yalikwenda vizuri katika vikao vya kamati, lakini kujadili sura
hizo mbili ndani ya bunge zima mabishano yataanza.
“Hizo sura mbili ndizo zinaleta ugumu,
ndipo kwenyewe,” alisema Mziray ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge hilo na kuongeza:
“Hali bado siyo nyepesi, bado sura hizo ndizo ngumu na ndizo zinaleta mambo.”
Aprili Mosi, mwaka huu kamati 12 za
Bunge hilo zilitawanyika katika maeneo manne kwa ajili ya kuchambua na kujadili
sura ya kwanza na ya sita ambazo ndizo zenye mvutano mkali.
Miongoni mwa mambo ambayo yalizua
utata katika Sura ya Kwanza ni ibara 1(1)
inayosema Tanzania ni nchi na
Shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo limetokana Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
ambazo kabla ya Hati ya Makubalino ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi
huru.
Katika ibara hiyo wajumbe kadhaa
walitaka neno shirikisho ilitoke badala yake iwe Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya
kamati kukosa theluthi mbili ya kura kutoka katika kila upande wa muungano
ambazo zinatakiwa kwa mujibu kanuni 64 (1).
Eneo lingine lililozua mvutano ni
Ibara 1(3) inayosema Hati ya Makubaliano
ya Muungano iliyorejewa katika Ibara ndogo ya kwanza ndiyo msingi mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba hii kwa kadri itakavyorekebishwa,
itakuwa ni muendelezo wa makubaliano hayo.
Kutokana na hali hiyo, wajumbe kadhaa
walitaka ufafanuzi kuhusu Hati ya Muungano na kutaka kuiona.
Hali hiyo ilisababisha kamati Na 2 na
8 kumuita aliyekuwa Katibu wa Bunge wakati wa Muungano, Pius Msekwa, kwenda
kutoa maelezo. Hata hivyo, suala hilo bado halijapata ufumbuzi hususani mahali
ilipo hati hiyo na madai ya utata wa saini.
Katika hatua nyingine, Mziray alisema
kuwa baraza lake liliandaa mkutano wa dharura wa viongozi wa vyama vya siasa kwa ajili ya kupata mwafaka na kuwekana
sawa kufuatia matukio kadhaa ya mivutano katika Bunge Maalumu la Katiba Jumatatu
iliyopita, lakini uliahirishwa kutokana na uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la
Chalinze na Siku ya Kumbukumbu ya Karume.
Alisema siku inayoweza kupangwa ni
Jumapili ambayo ni rahisi kuwapata viongozi wengi kwa kuwa hakuna vikao vya
Bunge.
Naye Katibu wa Baraza hilo, Jaji
Francis Mutungi, aliiambia NIPASHE kuwa wanauandaa tena mkutano huo ili
ufanyike kati ya Aprili 22 na mwisho wa mwezi.
Jaji Mutungi ambaye pia ni Msajili wa
Vyama vya Siasa, alisema watawawaalika watu wengine wakiwamo viongozi wa dini
na kwamba kabla ya mkutano huo, atakutana na baadhi ya makatibu wakuu wa vyama
vya siasa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment