Wanne wahukumiwa kifungo jela kwa kosa la kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja nchini Misri
Mahakama moja nchini Misri
imewahukumu watu wanne kifungo cha hadi miaka minane jela kwa kosa la vitendo
vya kufanya mapenzi ya jinsia moja.
Watu hao wanashutumiwa kuhudhuria au
kupanga tafrija za vitendo vya ngono, na kuvaa mavazi ya kike na kujipodoa.
Sheria ya Misri haitamki kupiga
marufu vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, lakini waendesha mashitaka wametumia
sheria ya Misri inayokataza mambo fulani kufanyika hadharani kuwahukumu wapenzi
wa jinsia moja.
Hukumu hiyo imeshutumiwa na
wanaharakati wa haki za binadamu.
Mmoja wa watu hao amehukumiwa na
mahakama mjini Cairo, kifungo cha miaka mitatu jela na kazi ngumu.
Kikundi cha kutetea haki za binadamu
chenye makao yake nchini Marekani, Human Rights First , kimesema hukumu hizo
zinasikitisha na kukatisha tamaa.
"Misri ni taifa linalobadilika
katika eneo la nchi za Kiarabu; kinachotokea Misri kinaweka hali ya kuenea
katika ulimwengu wote wa nchi za Kiarabu," kimesema kikundi hicho katika
taarifa yake.
Kikundi hicho kimesema tangu
kung'olewa madarakani Rais Mohammed Morsi mwezi Julai 2013 kumekuwa na ongezeko
la watu kukamatwa kwa misingi ya jinsia zao.
Hukumu ya sasa inakumbushia kesi ya
mwaka 2001 ya watu 52 kushutumiwa kwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na
makosa mengine chini ya sheria ya Misri.
Watu ishirini na watatu walihukumiwa
kifungo cha kufikia miaka mitano jela pamoja na kazi ngumu, hukumu ambayo
ilishutumiwa kimataifa.
Kikundi kimoja cha kutetea haki za
binadamu nchini Misri kimesema adhabu kali zilizotolewa kwa watu hao Jumatatu
ni sehemu ya msako unaoendelea dhidi ya uhuru binafsi.
Chanzo: BBC Swahili
No comments:
Post a Comment