Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
MATOKEO ya 0-0 waliyoyapata Mbeya
City leo hii kwenye mchezo mgumu wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya
Ashanti United katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la
Dar es salaam yamewagharimu na kuwakosha rasmi ubingwa msimu huu.
Ashanti United waliokuwa na lengo la
kupata ushindi leo hii mbele ya Mbeya City wameambulia pointi moja muhimu
kuliko kupoteza mchezo huo.
City wamefikisha pointi 46 katika
nafasi ya tatu sawa na Yanga waliopo nafasi ya pili kwa pointi 46, lakini
kikosi cha Pluijm kina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hii ilikuwa mechi ya 24 kwa Mbeya
City, hivyo wamebakiza mechi mbili nyumbani
dhidi ya Azam fc na Mgambo JKT.
Kama watashinda mechi zote
watafikisha pointi 52 ambazo tayari Azam wameshafikisha kileleni.
Kwa maana hiyo, Mbeya City rasmi
wamejitoa kuwania ubingwa na kuwaacha wanaume wawili, Yanga sc na Azam fc
kuendelea na vita hiyo.
Kilichobaki kwao ni kuisaka nafasi ya
pili, kwani wanaweza kuipata kutegemeana na matokeo watakayopata Yanga SC.
Yanga wamebakiza mechi nne kuanzia ya
kesho dhidi ya JKT Ruvu ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Kama Mbeya City wanataka kuchukua nafasi ya pili wanatakiwa kuwaombea
Yanga mabaya ili wapoteze mchezo mmoja, washinde mmoja na kutoa sare miwili.
Kama matokeo hayo yatatokea, maana
yake Yanga atavuna pointi tano pekee na ukijumlisha na pointi 46 walizonazo
sasa watafikisha pointi 5I ambazo Mbeya City atazivuka endapo atashinda mechi
zote.
Yanga ataanza kazi kesho dhidi ya JKT
Ruvu, baada ya hapo atavaana na Kagera Sugar mechi ya kiporo aprili 9, na
hatimaye atasafiri kwenda Arusha aprili 13 kuwavaa JKT Oljoro na kurejea Dar es
salaam kufunga msimu dhidi ya Simba uwanja wa Taifa aprili 19 mwaka huu.
Kwa mechi alizosaliwa nazo Yanga si
rahisi kutabiri matokeo, lolote linaweza kutokeo, lakini kwa Mbeya City
biashara imewakata kwasababu mambo ya kusubiri mwenzako apoteze inaweza kutokea
au isitokee.
Hata hivo mtandao huu umezungumza na
kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi ambaye amekiri wazi kuwa mchezo wa
leo ulikuwa mgumu sana kwa upande wao.
‘Tunamshukuru Mungu mechi imeisha
salama na tumeambulia suluhu. Ni matokeo mabaya kwetu, lakini huwezi jua
waliopo juu yetu watapata matokeo ya aina gani huko mbeleni. Kimsingi
yametuharibia sana, lakini hatukati tamaa kupambana mpaka dakika ya mwisho”.
“Hata kama itakuwa tofauti na malengo
yetu sio mbaya. Huu ni msimu wetu wa kwanza. Tumejitahidi kadri ya uwezo wetu
na haya ndio mavuno yetu. Tunarudi kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Azam fc”.
Alisema Kocha Maka.
Kocha wa Ashanti United, Abdallah
Kibadeni aliwahofia Mbeya City kwasababu ya ubora wao, lakini amemaliza mechi
kwa kupata pointi moja muhimu.
Kwa matokeo hayo, Ashanti wanafikisha
pointi 22 katika nafasi ya 12 baada ya kushuka dimbani mara 24.
Mchezo ujao watashuka dimbani
kukabiliana na Simba uwanja wa Taifa na watahitimisha kibarua chao msimu huu
dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa sokoine jijini Mbeya.
Kama Ashanti United watashinda
michezo hiyo mitatu watafikisha pointi 31 na pengine kujiweka mazingira mazuri
ya kubakia ligi kuu.
Wakati huo huo Mgambo JKT wapo nafasi
ya 11kwa pointi 22 kama Ashanti, na wamebakiwa na michezo mitatu.
Kama Mgambo watashinda mechi zijazo
dhidi ya Coastal Union, Kagera Sugar na Mbeya City watafikisha pointi 31 kama
Ashanti, na hapo timu moja italazimika kushuka kwa kuangalia tofauti ya mabao
ya kufunga na kufungwa.
Rhino wapo mkiani kwa pointi 13 na
wamebakiza mechi tatu. Kama watashinda zote watafikisha pointi 22 ambazo
zimefikiwa na Ashanti, Tanzania Prisons na Mgambo, huku timu hizi zikiwa na
mechi tatu mkononi.
Oljoro JKT wapo nafasi ya 13 kwa
pointi 15 na wakishinda mechi zao tatu zilizosalia watafikisha pointi 24 ambazo
zinaweza kupitwa na Ashanti United, Prisons na Mgambo JKT.
Hivyo kwa mazingira haya, Rhino
Rangers na JKT Oljoro zina asilimia kubwa ya kushuka daraja, huku Ashanti,
Mgambo na Prisons zikipambana kwa nguvu kukwepa kuungana na timu hizi mbili za
mwisho.
Mchezo mwingine umepigwa katika dimba
la Kaitaba ambapo wenyeji wa uwanja huo wamewakaribisha wekundu wa Msimbazi
Simba sc.
Mechi hiyo imemalizika kwa sare ya
bao 1-1.
Simba walikuwa wa kwanza kuandika bao
la kuongoza katika dakika ya 45 kipindi cha kwanza kupitia kwa Zahor Idd Pazzi akipokea krosi
kutoka kwa nahodha wao, Nassor Masoud Cholo.
Kagera walisawazisha bao hilo dakika ya 51 kipindi cha pili
kupitia kwa mshambuliaji wao hatari, Them Felix `Mnyama`.
Kwa matokeo hayo, Simba sc
wamefikisha pointi 37 katika nafasi ya 4 baada ya kushuka dimbani mara 24.
Kagera Sugar wamefikisha pointi 34 katika
nafasi ya 5 baada ya kushuka dimbani mara 23.
Mechi ya Kaitaba haikuwa na ushindani
mkubwa kwani timu zote hazikuwa na cha kupoteza, kwa maana ya kutotafuta
ubingwa wala nafasi ya pili.
Timu zote zilikuwa zinashambuliana
kwa zamu, lakini Kagera Sugar walipata nafasi nyingi zaidi ya Simba.
Hata hivyo ubutu wa safu za
ushambuliaji kwa timu zote ,kumeamuru matokeo yawe 1-1 mpaka dakika 90
zinamalizika.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi
kadhaa kupigwa katika miji tafouti.
Jijini Dar es salaam, Yanga watakabiliana
na JKT Ruvu na ushindi ni muhimu kwa timu zote.
JKT Oljoro watawakaribisha maafande
wa Tanzania Prisons katika dimba la Shk. Amri Amri Abeid Kaluta jijini Dar es
salaam.
Rhino Rangers watakuwa dimba la Ali
Hassan Mwinyi kuumana na Mtibwa Sugar kutoka Morogoro.
Nao wagosi wa Kaya watawakaribisha
ndugu zao, Mgambo JKT katika dimba la CCM Mkwakwani, Jijini Tanga.
Chanzo: Shafii Dauda
No comments:
Post a Comment